RAIA MWEMA; Bunge laambiwa nchi iko hatarini - Zitto akumbushia vita ya Kagera

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Waandishi Wetu
Toleo na 19


january-zito.jpg

  • Zitto akumbushia vita ya Kagera
  • Kilango: Serikali ichukue hatua
  • ​Makamba: Itasababisha vurugu
  • Mnyika: Kuna rushwa kubwa
WAKATI kukiwa na taarifa za kuwapo mkono wa baadhi ya wanasiasa katika kuhujumu Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, tatizo la mafuta nchini limeelezwa kuwa linahatarisha usalama wa Taifa huku wabunge wakisema litazua vurugu na kwamba ni kana kwamba nchi iko vitani.

Maoni hayo ya wabunge yalitolewa jana bungeni mara baada ya kuwasilishwa kwa hotuba za bajeti za Wizara ya Viwanda na Biashara ambazo majadiliano yake yaliahirishwa ili kutoa nafasi ya kuzungumzia suala la mafuta ambalo kuanzia wiki iliyopita limekuwa kero kubwa katika miji karibu yote mikubwa nchini.
Aliyeanzisha mjadala kwa kuwasilisha hoja ya kutaka tatizo la nishati ya mafuta lijadiliwe bungeni kwa utaratibu wa dharura, alikuwa ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), Januari Makamba.

Akizungumza kama mwanzilishi wa hoja hiyo Makamba ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini alisema tatizo la mafuta "ni kiama" na linaweza kusababisha watu kufanya vurugu.

Alisema tatizo la mafuta ni kubwa na halipaswi kuachwa liendelee bila kufanyika kwa uamuzi kwa Serikali kuingilia kati.

Alisema Makamba: "Haihitaji maelezo kujua kwamba nchi iko kwenye dharura. Kuna mgawo wa umeme kwa muda mrefu, lakini kwa maendeleo ya usalama na amani, nishati ya mafuta ni muhimu kuliko umeme."

Alisema kwamba kuna udhaifu katika usimamizi wa sheria kutokana na kuwapo kwa taarifa ya kushusha bei bila ya kuwapo maandalizi ya kutosha katika kusimamia sheria.
"Sawa tumeshusha bei, sasa hivi watu wananunua Sh 3,000 hadi Sh 5,000 na kuna foleni kubwa sana. Ukikaa kwenye foleni mtu anakuja na dumu la lita 25 anakwambia nipe Sh 25,000.

" Watu wanapata adha, hatuoni tamko, hatuoni hatua, tunaomba wenzetu wa Serikali kuonyesha nchi jinsi mafuta yalivyo nyeti katika usalama na nchi, watu wanaweza kuingia barabarani," alisema.

Kwa upande wake, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, alifananisha hali ya sasa na nchi kuwa vitani kwa kutaka wauzaji mafuta wapewe agizo la kuuza mafuta mara moja la sivyo wafungiwe leseni zao.

Alisema imezoeleka kwa wafanyakazi kugoma kupigania haki zao, lakini haijawahi kutokea wafanyabiashara wakagoma kama ilivyotokea sasa kwa wauzaji wa mafuta.

"Katika hali ya kawaida tumezoea wafanyakazi kugoma wanapodai maslahi yao. Hatujawahi kuona wafanyabiashara kugoma. Tulipoamua kufungua uchumi wa soko kutoa haki kwa wafanyabiashara kufanya biashara kwa mujibu wa kanuni za soko, hatukuondoa uwajibikaji wa Serikali.

"Bado Serikali inao wajibu wa kulinda raia wake. Wafanyabiashara (wa mafuta) kwa kutumia cartel yao wamemua kukiuka agizo la Serikali. Hatupaswi kutumia maneno matamu dhidi yao, lazima kuonekane kuna dola kulinda raia, sheria ya EWURA imetoa haki ya kulinda walaji tena walaji wa hali ya chini," alisema na kuongeza:


"Leo wananchi wetu, Dar es Salaam na miji mingine wanahangaika, hata daladala zimepandisha bei, Kigoma leo siku ya nne hakuna umeme kwa sababu hakuna mafuta, wanaiweka nchi katika hatari, hatuwezi kukubali."


Alipendekeza Serikali itoe amri kwa wafanyabiashara wote kuanza kuuza mafuta jana Jumatano jioni na kwamba ambaye atakiuka agizo hilo anyang'anywe leseni na wananchi wajiandae kukubali athari za hatua zozote ili kulinda maslahi yao.

"Inawezekana ikawaletea shida wananchi lakini haitakuwa mara ya kwanza.

Tulikwenda vitani bila silaha kubwa tena bila ya kuungwa mkono na wakubwa. Tukamng'oa Nduli Iddi Amini. Tulipata shida na kwa hili wananchi lazima watapata shida lakini lazima tutoe nafasi ya kutekeleza sheria.


"Wafanyabiashara wa mafuta wana maneno matamu. Wakati tumepandisha mafuta ya taa hawakutueleza faida zao lakini sasa wanadai faida itapotea. Kama wafanyabiahara …. wanataka kutumia jeuri yao ya fedha, wajue Watanzania ni masikini jeuri," alisema Zitto ambaye alitoa pendekezo la vyombo vy ulinzi kusimamia utekelezaji wa agizo la Serikali.


Zitto alisema ikibidi Jeshi liingilie na kusimamia kufunguliwa kwa vituo ili wananchi wapate mafuta wakati wataalamu wa uchumi wanafanya uchambuzi wa kibiashara.


Kwa upande wake Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa alisema tatizo ni kwa Serikali kutotekeleza maagizo ya Bunge ya kutaka kuimarishwa kwa Shirika la Petroli la Taifa (TPDC) ili liweze kufanya biashara ya mafuta na kuweka akiba.

Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango aliunga mkono wazo la Zitto la kutoa agizo kwa wauzaji wa mafuta kuuza mafuta kuanzia jana jioni na kuwataka wafanyabiashara kujali zaidi maslahi ya wengi badala ya kujali kupata faida.
Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage, yeye alisema tatizo lililipo limetokana na ukimya wa Serikali kutokana na tatizo kuanza kujulikana mapema bila hatua wala tamko lolote kutoka serikalini.

"Tatizo, haya mambo yanakwenda ovyo ovyo. Tumeonyesha kuna kasoro hatujaambiwa wamepata kiasi gani, pamoja na maamuzi ya Bunge, tuwaite hapa, watuonyeshe….

Kama wamekiuka watuonyeshe, kama watendaji wamekosea tuchukue hatua… simbembelezi mtu… kanuni za mahesabu aliyekiuka achukuliwe hatua," alisema Mwijage.


Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, yeye alitoa shutuma nzito kwa kusema anao ushahidi wa kuwapo baadhi ya watendaji waliokula rushwa kwenye sakata la mafuta na kutaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati kwa kutumia madaraka yake kutatua tatizo la mafuta nchini.


"Nina ushahidi baadhi ya maofisa wa Serikali kuhongwa katika suala hili. Sisi (Watanzania) tunamiliki asilimia 50 ya hisa ya BP na wao wanaleta kiburi. Kampuni tunayomiliki inakataa kuuza mafuta!? Tunamiliki asilimia 50 ya TIPPER serikali iko wapi hadi tukose mafuta?" alihoji Mnyika.


Mnyika alifikia hatua ya kupendekeza hata ikibidi serikali izuie mafuta yanayopitishwa nchini kwenda nje ya nchi na kuuzwa nchini kufidia uhaba uliopo.

Mbunge wa Muheza (CCM) Hubert Mntangi yeye alisema wauzaji wa reja reja hawana makosa maana wanategemea zaidi mafuta kutoka kwa wauzaji wakubwa ambao ndio wanaopaswa kubanwa ikiwamo BP ambalo serikali wana hisa ya asilimia 50.
 
Kwanini wasianzishe Transparency WebSite? Itaonyesha kila Waziri Mali walizonazo na Mali wanahisa... Hii itakuwa rahisi kwa wananchi kujua wapi pa kushinikiza na wakati wa Uchaguzi wasiwachague watu hao

Africa Kusini wanafanya hivyo; Tunaweza kufanya hivyo kama hautaki unajivua ubunge mwenyewe...

Oh labda tunahitaji katiba mpya then... AZIMIO LA ZANZIBAR liliivunja Rasmi Matakwa ya Viongozi YA LILE AZIMIO LA ARUSHA...
 
Back
Top Bottom