Raia anaweza kumfungulia rais kesi ya madai

Yona F. Maro

R I P
Nov 2, 2006
4,202
218
SHERIA inaruhusu mtu yeyote ambaye ana madai dhidi ya Rais wa nchi kufungua kesi ya madai hayo, ili aweze kupatiwa haki yake.
Ni wazi kuwa mtu anaweza kujiuliza je, inawezekana vipi kwa raia kumfungulia kesi ya madai Rais wake?
Jibu la swali hili limewekwa wazi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mbalimbali.
Kifungu cha 46 Ibara Ndogo ya Pili (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kinaeleza kuhusu ufunguaji wa kesi ya madai dhidi ya Rais kwa jambo lolote alilofanya katika uwezo wake kama raia wa kawaida yaani, "Institution of Civil Case in respect as an ordinary citizen."
Katiba kinaelekeza suala zima la ruhusa ya kumshitaki Rais kwa kosa la madai, yaani "a civil wrong," .
Katika sheria juu ya shughuli au mambo ya Rais, yaani, "Presidential Affairs Act, CAP9." Taratibu zimewekwa kuhusu suala zima la kufungua kesi ya madai dhidi ya Rais wa nchi.
Mahakama ambayo inaruhusu kupokea mashitaka hayo ya madai, katika, Kifungu cha Tano (5) cha sheria hiyo kinaeleza kuwa hakuna kesi yoyote ya madai inayofunguliwa dhidi ya Rais itaruhusiwa katika mahakama yoyote isipokuwa mahakama kuu pekee yaani, "No Civil Proceedings which may be instituted against the President shall be instituted in any court other than the High Court."
Hivyo endapo una madai dhidi ya Rais wako, basi mahakama inayotakiwa kufungua madai hayo ni Mahakama Kuu pekee.
Kifungu cha Sita (6), Kifungu Kidogo cha kwanza (1) cha sheria ya shughuli au mambo yanayomhusu Rais (Presidential Affairs Act), kinasema, mtu yeyote ambaye anakusudia kufungua kesi ya madai dhidi ya Rais ni lazima atoe notisi ya siku Thelathini (30) kwanza kabla ya kufungua kesi hiyo.
Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 46 Ibara ya (2) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika Kifungu Kidogo cha Kwanza (1) (9) cha Kifungu cha Sita (6),inaelezwa kuwa, notisi ya mashitaka ya madai dhidi ya Rais ni lazima iambatane na Hati ya madai. Yaani "Plaint"
(b) Notisi na hati hiyo ya madai itatumwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi au kwa Katibu wa Kudumu au binafsi wa Rais au Notisi na Hati hiyo itatumwa kwa Rejesta iliyolipiwa kabla, kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu kupitia njia ya posta.
Kifungu Kidogo cha Pili (2) kinaeleza kuwa, endapo mahakama itaridhika kuwa kesi dhidi ya Rais imefunguliwa na kwamba mdai, yaani "Plaintiff" ana haki dhidi ya Rais, Mahakama hiyo haitatoa hukumu au agizo dhidi ya Rais isipokuwa kwa kuarifu kwa njia ya maelezo ya kisheria kuwa kuna madai dhidi ya Rais yaliyothabiti, yaani "By way of declaratory order."
Lengo la utaratibu huu ni kumfahamisha Rais, ili aweze kukidhi matakwa hayo na wala si kumwamrisha, kama inavyokuwa kwa watu wengine wanapofunguliwa kesi za madai.
Kwa upande wa amri ya kukamatwa (arrest), Kifungu cha Nane (8), Kifungu Kidogo cha Kwanza (1) kinaeleza kuwa, Rais ana kinga dhidi ya kukamatwa yaani, "The President shall be immune from arrest."
Kifungu Kidogo cha Pili kinasema hakuna amri yoyote itakayo tolewa kwa Rais na mahakama yoyote au mtu au mamlaka yenye uwezo wa kutoa amri ya;-
(a). Kumtaka Rais au kumlazimisha kufika mahakamani iwe kwa uwezo wake kama Rais au hata katika uwezo wa kawaida.
(b). Kumtaka au kumlazimisha Rais kumleta mtu au kutoa kitu chochote mahakamani.
Kifungu Kidogo cha Tatu (3) kinasema endapo upande katika kesi unaomba ruhusa ya kuitwa mahakamani kwa Rais kama shahidi katika kesi hiyo au kumtaka Rais amlete mtu au kitu chochote mahakamani hapo, mahakama itatakiwa kumfahamisha Rais juu ya maombi hayo, lakini mahakama hiyo haitatoa amri nyingine au kutoa wito juu ya maombi hayo.
Kifungu cha Tisa (9) kifungu kidogo cha kwanza kinasema kuwa, hati ya kuitwa shaurini (Summous) ni marufuku kupelekwa Ikulu, au nyumba za kupumzikia wageni au katika viwanja vya Ikulu au katika makazi mengine yoyote maalumu ya Rais, isipokuwa mpaka yatolewe maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi juu ya utekelezaji wa utaratibu huo wa ki-mahakama.
Katika kifungu cha Saba (7) Kifungu Kidogo cha Kwanza (1) kuhusu utaratibu wa kisheria dhidi ya Rais anaposhitakiwa, sheria inasema taratibu nyingine zote zielekezwe kwa Mwanasheria Mkuu yaani, "The Attorney General," isipokuwa kwa zile zilizoelekezwa katika Kifungu cha 46 cha Katiba Ibara ya Pili (2) kama tulivyoona hapo awali.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom