RAI: Idara za Uhamiaji, Kazi zawabania Watanzania; kuwaleta 'wataalamu' wa Kihindi

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Imeandikwa na Justin Damian na Deo Kishombo
Alhamisi, Juni 28, 2012 09:52
*Kamal Group yawatumia uhamiaji kuwaleta 'wataalamu' wa Kihindi
*Kiwanda kilifunguliwa na OSHA, lakini hakikufanyiwa marekebisho
*Ofisa wake anyang'anya vitendea kazi vya mwandishi wa habari

NI waza kwamba kuna kisichoeleweka katika Idara za Uhamiaji na Idara ya Kazi, kuhusu mchezo unaofanywa na baadhi ya kampuni za kigeni kuleta wafanyakazi kutoka nje kwa kisingizio cha uwekezaji.

Huku maelfu ya vijana nchini wakiwa wanashinda vijiweni kwa kukosa ajira, baadhi ya makampuni ya kigeni yanaleta watu kutoka nje kwa kisingizio kwamba watu hao ni wataalamu wa kiufundi.

Pamoja na kuingia nchini na kupewa vibali vya kufanya kazi, Rai limegundua udanganyifu unaofanywa na kampuni za Kamal za jijini Dar es Salaam.

Kampuni hizo kwa ujanja wa makusudi, huzuia nafasi za kiufundi katika viwanda vyake vyote na kuleta wafanyakazi wa Kihindi kutoka India, huku Watanzania wakisota mitaani.

Lakini Rai imegundua pia kwamba kuna udhaifu wa kiutendaji katika Idara ya Uhamiaji, ambayo haifuatilii na kuthibitisha kwamba ‘wataalamu’ walioombewa vibali, wanafanya kazi zilizoanishwa kwenye vibali vyao.

Uhamiaji pia inatuhumiwa kwamba imeshindwa kufuatilia ajira za wageni katika sehemu nyingi za kazi, kiasi kwamba wafanyakazi wachache wa Kitanzania wanao ajiriwa na kampuni za kigeni, wanadhani kuna mchezo mchafu unafanyika.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua kundi la makampuni ya Kihindi linalojulikana kama Kamal Group of Companies, ambalo limeweza kuutumia udhaifu wa ufuatiliaji wa Idara ya Uhamiaji na kuingiza wafanyakazi kutoka India kwa mwamvuli wa wataalamu.

Wahindi hao wanafanya kazi katika kampuni za Kamal Gases, Kamal Angro Ltd, Kamal Refinery Ltd na Kamal Steels Ltd.

Rai limefanikiwa kupata majina ya wafanyakazi hao pamoja vibali vyao vya kazi, ambapo baadhi vinaonyesha kwisha muda wake wakati wahusika wakiwa bado nchini

Vyanzo vya uhakika ndani ya kampuni hiyo, vililiambia gazeti hili kuwa, wakurugenzi wake ambao wote ni Wahindi, wamekuwa wakicheza mchezo mchafu na Idara za Serikali ikiwamo Idara ya Uhamiaji, pale wanapoona mambo yao hayaendi sawa, ili kuhakikisha kuwa wanafanikisha malengo yao hata kama ni kwa kuvunja sheria.

“Hawa Wahindi wana mtandao mkubwa sana serikalini. Mwezi Machi, mwaka huu, kiwanda chao kilifungiwa baada ya kupewa notisi ya wiki mbili na Mamlaka ya Usalama na Afya Sehemu za Kazi (OSHA), kuhakikisha inaboresha hali, lakini wiki mbili ziliisha bila kufanyika marekebisho hayo.

Mamlaka hiyo ilikifungia lakini siku ya pili yake tu kilifunguliwa kwa amri za wakubwa serikalini.

Wafanyakazi wa Kihindi ambao wapo kinyume cha sheria, Uhamiaji wakijifanya hawaoni kinachoendelea, wanalipwa mishahara minono na kupewa vivutio kama usafiri, chakula na malazi, wakati Watanzania wanafanya kazi ngumu bila vifaa vya usalama na katika mazingira magumu, wakilipwa kama vibarua ,” chanzo kilisema.

Nyaraka ambazo gazeti hili zinazo zinaonyesha kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi walioingia nchini kama wataalamu wa mifumo ya kompyuta (Computer programmer), lakini wanafanya kazi kama wasimamizi wa upakiaji wa mizigo kwenye magari.

Wafanyakazi wengine walioingia kama wakurugenzi, wanafanya kazi ya uhasibu, huku walioingia kama wahandisi wa mitambo, wameajiriwa kama wakaguzi wa vyuma chakavu, wapima uzito wa vyuma, pamoja maafisa mauzo.

Chanzo chetu ndani ya kampuni hiyo kilituambia: “Uhamiaji huwa wanakuja hapa na sidhani kama hawajui hili, japokuwa sina uhakika sana. Lakini hata utoaji wa vibali unagubikwa na utata, hivi kweli Tanzania hatuna mafundi wa kuchomea vyuma (welders), mpaka mafundi hao waje kutoka India? Hawa Wahindi wanaziba nafasi zetu za kazi na Serikali inawafumbia macho,” alilalamika.

Waandishi wa habari hizi walipokwenda makao makuu ya kiwanda hicho kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa tuhuma hizo, walipishana na wakurugenzi wa kampuni hiyo waliokuwa ndani ya gari aina ya Land Cruser VX wakiingia getini.

Walipofika mapokezi walipokelewa vizuri na kukaribishwa katika chumba cha wageni na kuambiwa wasubiri kidogo.

Baada ya muda mfupi, aliingia dada aliyejitambulisha kwa jina la Brenda Sylvester, Afisa Masoko Mkuu wa Kamal Gases na kusema kuwa wakurugenzi hawapo na wamemwagiza kuongea na waandishi kwa niaba yao.

Brenda alikanusha zote na kusema siyo kweli. Baada ya waandishi kumtolea ushahidi, alishtuka na kutaka atajwe tuhuma hizo na kuziandika, kisha kuwapelea wakurugenzi.

Baada muda alirudi na kusema: “Nimewapelekea wakurugenzi wamesema tuhuma hizi ni nzito na inabidi mpange muda mje kuonana na mkurugenzi mkuu. Ni mtu mzuri sana na wala hana shida hata kidogo. Naamini mtafurahia ufafanuzi atakaowapatia,” alisema.

Waandishi walipomuuliza mbona mwanzoni alisema kuwa wakurugenzi hawapo, Brenda hakujibu. Waandishi walipomwambia kuwa hakukuwa na umuhimu wa wao kuonana na mkurugenzi kwa kuwa yeye alikwisha toa maelezo kwa niaba ya wakurugenzi. Dada akawa mkali na kufunga mlango kisha akamnyang’anya mmoja wa waandishi kamera na noti buku.

Dada huyo aliwatisha waandishi kuwa kama wataandika alichosema watamtambua kwa kuwa yeye si msemaji wa kampuni.

Aliendelea kufoka mpaka alipoingia mfanyakazi mwenye asili ya Kihindi na kumtuliza.

Yule mfanyakazi Muhindi aliwaambia waandishi kuwa wangepigiwa simu kesho yake kwa ajili ya kukutana na mkurugenzi mkuu. Hadi tunakwenda mitamboni, hakuna simu iliyopigwa.

Vyanzo vyetu ndani, vilituambia kuwa mara baada ya waandishi kuondoka, kiliitishwa kikao cha menejimenti kutaka kujua nani alivujisha taarifa kwa waandishi.

Kikao kiliazimia kuwa akijulikana aliyefanya hivyo basi atafukuzwa kazi mara moja.

Rai lilitaka kupata ufafanuzi Uhamiaji.

Mbaraka Batenga, kwa niaba ya msemaji wa Idara, alisema kuwa wao hutoa vibali vya kazi baada ya kupata maelekezo kutoka Wizara ya Kazi na kwamba endapo watapata taarifa zozote za utata juu ya watu wanaoombewa vibali, wanaweza kusitisha zoezi la kuwapatia.

“Ni kweli kuwa kama huyo mwekezaji unayemsema analeta watu kama wataalamu lakini hawafanyi kazi kulingana na kile kilichoonyeshwa kwenye vibali amefanya makosa. Bado tunalifuatilia hili na likikamilika tutawataarifu,” alisema.

Batenga alisema kuwa Uhamiaji haitasita kumchukulia hatua kali mwekezaji huyo endapo atabainika kuwa amekuwa akikiuka sheria.

Alipoulizwa kwa nini hawawafuatilii waliopewa vibali, badala ya kuletewa badala taarifa, alijibu kuwa huwa wanafuatilia, lakini mara nyingi wawekezaji hawawapi taarifa za kweli.

Rai lilipomuuliza kama Uhamiaji wamefuatilia kwa karibu na kufika kiwandani hapo na kuongea na uongozi wa kampuni, alijibu kuwa ufuatiliaji bado unaendelea.

 

Tuna Taaluma lakini hatupewi Kazi kwenye Makampuni haya ya Wahindi ni Sababu ya rangi yetu? na Uhamiaji wanapewa

chochote hawajali wanwapa work permit, hawatujali sisi wazalendo tukihangaika kutafuta kazi...

Wakati wa Nyerere nilikuwa sijui Work Permit; Sasa hivi Nazijua ziko Nyingi kweli, hadi wazungu na hawana kazi

Ni kuzurura na kutafuta cha kuiba kupeleka kwao
 
Back
Top Bottom