Prof. Ibrahim Noor na historia ya Zanzibar

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,912
30,253
Kubadilisha masomo ya taarikh iliyopotoshwa sana si kazi nyepesi kwani kuna wachache wenye nguvu ambao wanaing'ang'ania na kuilinda kwa nguvu zao, na za wakoloni wa leo wakiwa nyuma yao, kuwalinda kwa mirututu ya bunduki na risasi za moto ambazo wako tayari kuzitumia wakati wowote kuwauwa Wazanzibari. Si umeona aina ya vifaa vilivyoteremshwa visiwani wakati wa "uchaguzi"! Na si umeona vile walivyouendesha huo "uchaguzi" uliokataliwa na wengi!

Jambo moja ukishalitia katika bongo za vijana wakati wangali watoto wadogo na kuendelea nalo mpaka kumaliza masomo yao, huwa ni shida kubwa sana kulirakibisha; nalo ni kufundisha chuki, hata chuki hizo zikiwa hazina msingi wala ukweli ndani yake. Si unaona vile tunavyopata taabu kuwailimisha waliojazwa chuki hizo tokea utotoni mwao! Bila ya hizo siasa na masomo ya chuki yenye ukweli finyu na uwongo mwingi akina fulani hawatakuwa tena na madaraka na nyadhifa za juu, na hapa ndipo penye matatizo yote. Kwani wako tayari kuiuza nchi na uhuru wa wananchi wao kulinda matumbo yao. Potelea mbali raia wafe na njaa...

Juzi nilikuwa nazungumza na mhishimiwa mmoja na akaniambia: "tafadhali njoo utembee kwenu, siku nyingi hujaja. Nakuhakikishia hakuna lolote litalokukuta. Utakuja uondoke salama." Mimi nikamjibu: "Hakuna lolote linalonistua katika huu umri wangu. Kwani, nini kubwa watakaloweza kunitenda? Hakuna kubwa kama kuuwawa. Na hili pia halinistui. Kwani nikidhulumiwa roho yangu, watakaonidhulumu si watajitwika wao madhambi yangu wakifanya hilo? Linalonifanya nisitake kuzuru kwetu ni kuwa kila nikija nilikozaliwa huwa naondoka na majonzi mapevu sana kuona vile hali za watu zilivyodidimia vibaya sana. Ukiangalia unagundua kuwa mtu na aila yake kupata mlo mmoja wa kisawasawa kwa siku ni shida pevu sana. Ukiangalia hali ya masomo unatokwa na machozi. Ukiangalia hali ya matibabu unataka kulia. Kwa ufupi, kama wewe una hisia na watu wako na ni mtu mwenye huruma, haya onayoyaona hayaachi kukutia katika dhiki kubwa sana ya moyo.

Zanzibar kumetendwa dhambi kubwa sana zilizokemewa na Mola Subhana waTaala, za kuuwa watu kama nguruwe mwitu bila ya haqi, kuraruwa wanawake, kuwafunga na kuwaadhibu raia bila ya sababu, kudhulumu haqi za raia na kumetendwa na madhambi mengi mengineyo, na ikisha kumkejeli Mwenyezi Mungu kila mwaka kwa kuyasherehekea maovu yote hayo, na zaidi, kuviita vitendo viovu vyote hivyo: "Matukufu"! Nandika haya huku nalengwa na machozi nikifikiria vipi wanaosema kuwa wao ni Waislamu na wengine Wakristo wanavyojiandikia na kujipalilia wenyewe Moto, si wa Qiyama tu, bali tunaoneshwa tungali papa hapa Duniani malipo ya kumkejeli Mwenyezi Mungu kwa kusema na kutenda ya dhulma. Nani katika sisi wenye umri wa miaka sabini na zaidi tulifikiria kuwa hali ya Wazanzibari itafikishwa hivi ilivyo? Na bado inaendelea kudidimia. Kwa fikra zangu, hakuna njia ya kutokana na janga hili ila umma kutubia tawban nasuha na kumuomba Mwenyezi Mungu atuswamehe. Atuteremshie Rehma Zake. Vinginevyo ni kuwafurahisha wachache ambao hata na wao hawana raha ya Dunia na huko Akhera watajijua wenyewe.

Siachi kukutakieni nyote kila la kheri
Alichoandika Salim Msoma:
Mohamed Said: ZANZIBAR: THE AGONY OF ITS HISTORY BY SALIM MSOMA
 
Back
Top Bottom