Posho, kivuko vyaiweka CCM njia panda

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,080
nape-jukwaani.jpg
Katibu wa CCM Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye​
SUMAYE AMVUTIA PUMZI NDUGAI
Waandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimebaki njia panda baada ya kushindwa kuchukua hatua au kutoa tamko kuhusu mivutano na vita ya maneno inayoendelea sasa baina ya makada wake kuhusu masuala mawili makubwa yanayoigusa jamii.Masuala hayo ni nyongeza ya posho kwa wabunge ambayo imewaingiza katika vita ya maneno, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Suala jingine ni lile linalohusu ongezeko la nauli katika Kivuko cha Kigamboni ambalo limezusha malumbano baina ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na wale wa CCM.

Jana, CCM Taifa kupitia kwa Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kimetaka kisihusishwe katika misuguano hiyo ya posho na nauli za kivuko kwa sababu hoja zinazojadiliwa si za kiitikadi.

Wakati CCM Taifa ikisema hayo, chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, kupitia Kamati ya Siasa, kimetoa tamko la kumtaka Dk Magufuli aombe radhi kutokana na msimamo wake mkali wa kutetea kupanda kwa nauli.

CCM Dar es Salaam wamekwenda mbali zaidi pale Mwenyekiti wake, John Guninita iliposema kuwa tayari wamefanya mawasiliano na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kukubaliana naye kwamba suala hilo linaweza kupatiwa suluhu.

“Nimeongea na Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) mambo haya yanazungumzika nawataka tu wananchi wawe na subira kwa wakati huu,” alisema.

Huku CCM mkoa ikitoa msimamo huo, wabunge wa Dar es Salaam wamepanga kukutana tena leo kujadili hatua za kumchukulia Dk Magufuli wakidai makali ya kupanda kwa nauli za kivuko tayari yamejitokeza kwa bei ya bidhaa eneo la Kigamboni kuongezeka.

Kwa upande mwingine, Sumaye ametoa msimamo wake jana kwamba anamvutia pumzi Ndugai juu ya hoja zake alizotoa kuwa yeye (Sumaye) hana usafi wa kupinga ongezeko la posho za wabunge.

Hali hiyo tete inakifanya chama hicho tawala kujikuta kikiwa na kauli zinazojichanganya kuhusu msuguano unaoendelea kama ni kukua kwa demokrasia au ni utovu wa nidhamu wa kutozingatia kupingana kupitia vikao vya chama.

Kauli ya Nape
Nape alisema jana kuwa kukitaka chama hicho kutoa kauli juu ya hoja zinazobishaniwa ni kutokitendea haki. Alisema hoja hizo ni za msingi na haziwahusu tu wabunge wa CCM, bali hata wa vyama vya upinzani. “Haya ni mambo ya msingi msiyatafutie itikadi.”

Alisema katika suala la posho, wapo wabunge wa Chadema wanaounga mkono na wanaopinga na vivyo hivyo kwa CCM.

Alitoa mfano akisema yeye alipinga posho kwa wabunge sawia na msimamo uliotolewa na viongozi wa Chadema ingawa ndani kulikuwa na wabunge wanaoupinga hoja ya uongozi huo.

Kuhusu suala la vivuko, Nape alisema wabunge waliotoa msimamo, ndani yake yumo wa Chadema, John Mnyika: “Hivyo katika suala hili chama hakipo.”

CCM Dar
Wakati Nape akisema hayo, CCM Mkoa wa Dar es Salaam walikuwa kwenye mkutano na waandishi wa habari kutoa msimamo kuhusiana na mvutano uliopo baina ya wabunge wake, wengi wao wakiwa ni wa CCM na Dk Magufuli.

Katika mkutano huo, Guninita alimtaka Dk Magufuli awaombe radhi wakazi wa Kigamboni kwa kauli yake aliyotoa hivi karibuni kuwa wanaopinga kupanda kwa gharama za kivuko; wapige mbizi wakati wa kuvuka bahari badala ya kutumia kivuko.

Guninita alisema kauli hiyo imejaa dharau, kejeli na siyo ya kiungwana... “Chama kimepokea kwa masikitiko makubwa juu ya kauli zilizotolewa na Mheshimiwa Magufuli kwa wananchi wa Dar es Salaam, hususan wakazi wa Kigamboni kuwa kama hawawezi kulipa nauli mpya basi wapige mbizi.”

Pia alilaani kauli ya Dk Magufuli dhidi ya Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndungulile kuwa kama anawaonea huruma wananchi wanaotumia kivuko hicho basi anunue boti itakayoitwa "kwa jina lake au la chama chake.”

Alisema: “Kauli kama hiyo haijengi mshikamano na ushirikiano kati ya uongozi wa CCM na Serikali. Hata kama malalamiko ya wananchi hao hawezi kuyasikia … asingetumia maneno hayo.”

Kwa sababu hiyo wakamshauri; "Tunamtaka awe kiongozi aliye tayari kushirikiana na kushauriana na viongozi na wananchi wakati wa kutekeleza Ilani ya CCM, jambo ambalo haliwezi kuathiri katiba na kanuni za taratibu za majukumu ya wizara na nchi kwa ujumla.”

Guninita ambaye alikuwa akizungumzia ripoti ya kikao cha Kamati ya Siasa ya Halmashauri ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam iliyokaa juzi, alisema wanaungana na wabunge wa mkoa huo kuwa mabadiliko yaliyofanywa ni makubwa.

“Hebu ona Guta ambalo ndicho chombo kinachoendeshwa na mlalahoi kabisa linapandishwa nauli kutoka Sh200 hadi Sh1,800! Haya ni mabadiliko makubwa,” alisema.

Sumaye
Jana Sumaye alisema anajipanga kumjibu Ndugai juu ya hoja zake alizotoa kuwa, kiongozi huyo mstaafu wa shughuli za Serikali hana usafi wa kupinga kuongezwa kwa posho za wabunge. Alisema yupo safarini kurejea Dar es Salaam na akifika ndipo atakapojua ni jinsi gani atakavyomjibu Ndugai.

Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, Januari 3, mwaka huu Sumaye alisema hatua ya Bunge kujipandishia posho ya kikao kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku haiingii akilini na kwamba inakiuka utaratibu uliowekwa na Serikali katika kulipa gharama kwa maofisa wake.

Kauli hiyo ndiyo iliamsha hasira za Ndugai ambaye alisema Sumaye hana uadilifu wa kuzungumzia posho za wabunge kwani akiwa Waziri Mkuu, alifanikisha kupitishwa sheria ya malipo kwa viongozi wakuu wastaafu ili kujinufaisha.

“Kwa sasa analipwa asilimia 80 ya mshahara wa Waziri Mkuu aliyepo madarakani. Ni fedha nyingi kuliko hata mshahara wa Naibu Spika (Ndugai kwa sasa), wakati sheria hii inapitishwa alikuwa kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni (Waziri Mkuu), alikuwa anajiandalia mazingira ya kustaafu,” alisema Ndugai.

Habari hii imeandaliwa na Leon Bahati, Zacharia Osanga na Fredy Azzah.
Chanzo. Posho, kivuko vyaiweka CCM njia panda
 
Back
Top Bottom