Polisi wajigeuza watoza nauli ndani ya treni

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
ASKARI wa kikosi cha reli cha Jeshi la Polisi wamebuni njia mpya ya kujipatia kipato kwa kuwatoza abiria fedha za nauli na faini ndani ya treni huku wale wanaokosa wakipigwa na kufungwa pingu katikati ya maungio ya mabehewa.

Mbali na askari hao kuwatoza abiria fedha za nauli pia wamekuwa wakiwanyanyasa abiria wanaokuwa na fedha pungufu ndani ya treni kwa kuwatukana, kuwapekuwa mbele za watu, kuwapiga makofi pamoja na kuwafunga pingu katikati ya maungio ya mabehewa.

Hayo yalibainika katika uchunguzi uliofanywa na Mwananchi ndani ya treni hiyo ya abiria ya kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma kwa muda wa siku tano.

Wakizungumza na Mwananchi ndani ya treni hiyo, baadhi ya abiria walisema kuwa askari hao wamekuwa wakiingilia kazi za mkaguzi wa treni ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuhakiki tiketi na nauli ndani ya treni.

Ramadhani Tambwe na Yusuf Bakari waliofungwa pingu katika maungio ya mabehewa baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh2,000 kwa kosa la kupanda treni bila ya tiketi, walisema hiyo ni mara yao ya kwanza kupanda treni na hawakufahamu kuwa kuna utaratibu wa kutozwa faini.

“Wametufunga pingu hapa wakaondoka ingawa tumewalipa nauli halali, lakini wamesema kuna faini kwa sababu hatukukata tiketi kabla ya kupanda treni na walipotuomba hiyo faini hatukuwa nayo,” alisema Bakari.

Abiria mwingine, Zainabu Punguza, ambaye ni mwanafunzi, alisema polisi mmoja wa kike aliyevaa kiraia alimpiga makofi baada ya kukosa faini ya Sh1,000 ingawa aliwaeleza kuwa hakufahamu utaratibu huo kwa kuwa ni mara yake ya kwanza kupanda treni.

“Amenipiga makofi mbele za watu na kunipekua kwa kukosa Sh1,000... nimemuomba TT akanisamehe, lakini hawa polisi wamekataa kabisa kumsikiliza,” alisema Punguza.

Abiria aliyejitambulisha kwa jina la Ally Manyovu alisema askari wameacha kazi zao na kuingilia kazi za mkaguzi huyo wa treni za kukata tiketi badala ya kumlinda mkaguzi huyo pamoja na kulinda abiria na mali zao.

“Kwanza wanachukua fedha kwa abiria na kuwaficha Toilet wakati TT anapita na wakati mwingine wanawaficha katika behewa la chakula ndani ya treni ili wasikutane na TT,” alisema Manyovu.

Wakati jeshi la polisi reli likirundikiwa lundo la tuhuma, Kamishina Msaidizi wa Polisi Reli Ruth Makelebo alisema jeshi lake limeanza kufuatilia suala hilo na tayari mmoja wa askari aliyedaiwa kukiuka maadili ya kazi yake amekamatwa na kuwekwa rumande.

“Hatuwezi kuvumilia tabia hiyo na tayari askari mmoja aliyesafiri na treni anashikiliwa na polisi mkoani Tabora kwa ajili uchunguzi zaidi,” alisema Makelebo.

Naye meneja usafirishaji wa Dar es salaam aliyesafiri na treni hiyo, Joshua Mluzya alisema hana taarifa za vitendo hivyo vya polisi na kuahidi kuzifuatilia kiundani zaidi.

Polisi wajigeuza watoza nauli ndani ya treni

Askari Mzee Kova wanavyofanya vitu vyao ndani ya Treni,ama kweli mwenye nguvu mpishe apite hiyo ndio bongo yetu ehh Kasheshe kweli.
 
Back
Top Bottom