PISTO LERO
JF-Expert Member
- Mar 8, 2011
- 2,819
- 1,454
UCHUNGUZI wa kifo cha Mwenyekiti wa Chadema, Kata ya Usa River, Msafiri Mwambo (32) umefanyika jana kwa kushirikisha, maofisa polisi na ndugu na jamaa wa marehemu , akiwapo Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari. Akizungumza na Mwananchi jana baada ya uchunguzi huo, Nassari alisema walitarajia taarifa ya kitaalamu ya chanzo cha kifo hicho ingetolewa jioni ili waanze taratibu za mazishi. "Tupo hapa Mount Meru Hospitali, uchunguzi wa kifo cha Mwenyekiti wetu unaendelea na tunaimani tutapewa taarifa za kitaaluma kuhusu chanzo cha kifo chake,"alisema Nassari. Nassari alisema wameamua uchunguzi wa kitaalamu ufanyike na taratibu za kisheria zifuatwe licha ya Mwambo kuonekana kwamba alikuwa amechinjwa kabla ya kufariki dunia. Alisema baada ya uchunguzi huo ,walitarajia jana jioni kufanya kikao na wanafamilia ili kupanga taratibu za mazishi. "Tutakuwa na kikao jioni na wanafamilia ili kupanga taratibu za mazishi leo (jana), nadhani baada ya hapo tutakuwa na maelezo zaidi,"alisema Nassari. Katika hatua nyingine, aliyekuwa Meneja Mwenza wa Kampeni katika jimbo hilo, wakati wa uchaguzi, uliofanyika April Mosi, mwaka huu Vicent Nyerere na Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini amewasili jana mjini hapa kwa ajili ya taratibu za mazishi ya marehemu huyo. Akizungumza na gazeti hili, Nyerere alisema ameamua kurejea Arumeru kuungana na wakazi wa jimbo hilo katika msiba huo kwa kuwa aliahidi katika kampeni kwamba watakuwa pamoja na wakazi wa jimbo hilo katika shida na raha. "Muda huu naelekea msibani, kifo hiki kimetusikitisha sana"alisema Nyerere. Mwenyekiti huyo, aliuawa juzi usiku kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana baada ya kumpigia simu akiwa katika eneo la Mji Mwema akitazama taarifa ya habari. Lakini muda mfupi baadaye alikutwa jirani na Shule ya Mukidoma akiwa amefariki dunia hata hivyo, wauwaji hao, waliondoka na simu yake pekee na kuiacha pikipiki aliyokuwa akiiendesha. Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema ameunda kikosi maalumu kinachoongozwa na Naibu Kamishina wa polisi, Isaya Mngulu kuchunguza kasi ya mashamba ya wawekezaji kuvamiwa na wananchi. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Mngulu ambaye tayari timu yake imeanza kazi alisema pamoja na mambo mengine, watachunguza kiini cha matatizo ya uvamizi wa mashamba. Hivi tuanavyozungumza tayari maofisa wa vitengo mbalimbali kutoka makao makuu wako Arumeru kukusanya taarifa za kiintelijensia zitakazo saidia kutatua tatizo hili, alisema Naibu Kamishina huyo. Aliwataka wananchi wenye tatizo la ardhi kutumia njia sahihi kudai mashamba kutoka kwa viongozi na serikalini badala ya kuvamia mashamba yanayomilokiwa kihalali na wawekezaji. KWA HISANI YA MWANANCHI |