Polisi kukukubali kuzidiwa mbinu na wauaji wa albino ni aibu!

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
Habari za kutekwa kwa kijana mwenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini na kisha kusafirishwa kwenda nchini Burkina Faso, zimestua na kuibua upya hofu iliyoanza kutoweka dhidi ya maisha na uhai wa albino.

Taarifa za kutekwa kwa kijana huyo, ziliripotiwa na gazeti dada la NIPASHE, la The Guardian, katika toleo lake la Mei 22, mwaka huu.

Habari hiyo iliyoongoza katika ukurasa wa mbele, gazeti hilo lilimkariri Muasisi na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Under The Same Sun (UTSS) ya jijini Dar es Salaam, Peter Ash, akiwaeleza waandishi wa habari kwamba, kijana huyo alitekwa na watu watatu wenye asili ya Afrika wanaozungumza lugha ya Kifaransa.

Ash alisema taarifa za kutekwa kwa kijana huyo alizipata kutoka kwa Dk. Pius Kamau aliyeshuhudia tukio hilo katika Uwanja wa Ndege wa Nairobi, nchini Kenya, wakati watekaji wakijiandaa kuondoka naye kwenda Burkina Faso.

Dk. Kamau ambaye ni mmoja wa watumishi katika kampuni ya ndege ya Kenyan-American National, alikaririwa na Ash akisema kuwa utekaji huo uligundulika katika ukaguzi wa nyaraka za safari, ambapo kijana huyo hakuwa na hati yoyote ya safari.

Ni tukio linalostua sana. Kwani linaibua upya hofu miongoni mwa wananchi, hasa albino ambayo ilianza kutoweka.
Hofu ya mara ya kwanza ilitokana na mauaji yaliyokuwa yamekithiri kwa albino katika baadhi ya maeneo nchini katika siku za nyuma.

Mauaji hayo yalitokana na imani za kishirikina. Yalikuwa makubwa na ya kusikitisha, kwani yaliwasibu ndugu zetu hawa (albino) wengi.
Mauaji hayo hayakuishia tu kuleta hofu. Bali pia yalitoa taswira mbaya ya nchi katika Jumuiya ya Kimataifa. Pia yaliathiri ustawi wa kijamii na kiuchumi.

Kama nilivyotangulia kusema, hofu kuhusu mauaji dhidi ya ndugu zetu albino ilikuwa imeanza kutoweka.
Ilianza kutoweka kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na serikali na vyombo vyake vya dola za kupambana na ukatili huo dhidi ya albino.

Watuhumiwa wengi walikamatwa, baadhi walifikishwa mahakamani na wengine walihukumiwa adhabu kali.
Kwa hakika, juhudi hizo zimesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya kuuawa kwa ndugu zetu albino nchini.

Mbali na watuhumiwa kuhukumiwa adhabu kali, viongozi wakuu wa serikali walitembelea na kujionea hali halisi inayowakabili ndugu zetu hawa (albino).

Hatua hiyo ilikwenda sambamba na viongozi kuzungumza nao pamoja na wadau wengine ili kuzidisha mapambano dhidi ya wahalifu hao wachache.
Katika juhudi hizo, itakumbukwa Machi 2009, serikali iliratibu zoezi la wananchi kupiga kura za siri ili kubaini wale wote wanaojihusisha na mauaji hayo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akihutubia katika sherehe za kufunga mafunzo ya awali ya askari polisi na uhamiaji katika Chuo cha Polisi (CCP) mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Aprili 18, 2009, alisema zoezi hilo lilifanyika vizuri nchini kote.

Mbinu hiyo ya serikali ilisaidia kutuliza hali ya hofu juu ya maisha na uhai wa ndugu zetu albino. Hali hiyo ikawa imeanza kuwa shwari.
Kwani matokeo ya wapigakura yalitumiwa na polisi kufanya upelelezi, kukusanya ushahidi na kuwakamata wote waliotajwa na kuwafikisha mahakamani, ambako sheria ilichukua mkondo wake.

Hatimaye, habari kuhusu uhalifu dhidi ya albino muda mrefu sasa zikawa nadra kusikika kama ilivyokuwa huko nyuma.
Lakini hali ya hofu ile inaonekana kuanza kurudi. Hiyo ni kutokana na wahalifu kubuni mbinu mpya ya kuendeleza dhuluma dhidi ya albino! Sasa wanawateka na kuwapeleka kwenda kuwaulia nje ya nchi!

Mimi naliamini sana jeshi letu la polisi. Linajitahidi sana kufanya kazi kwa kiwango cha kuridhisha. Kukukubali kuzidiwa mbinu na wauaji wa albino itakuwa ni aibu kubwa kwa jeshi hilo!

Kwa hali hiyo, linapaswa sasa kubuni mbinu mpya kutokomeza uhalifu huo mpya dhidi ya albino.
Mbinu ya kwanza, iwe ni kutoa elimu kwa jamii ili ione umuhimu wa kuachana na vitendo vya kikatili. Ya pili, kutoa elimu ya stadi za maisha kwa albino au kwa watu walio katika hatari.

Elimu hiyo itolewe kwa kuwapa albino mbinu za kuwatambua wanaojihusisha na vitendo vya kikatili dhidi yao na kufundishwa mbinu za namna ya kukabiliana na watu hao au kuomba msaada.

Kwa mfano, polisi wanaweza kuwapa albino ‘mbiu’ maalum kama filimbi za kupiga wanapowaona waovu wanawakaribia.
Kadhalika, kupitia polisi jamii, jeshi la polisi liimarishe ulinzi katika maeneo ambayo ni hatarishi kwa albino. Pia liweke namba maalum kwa ajili ya albino na watu wengine watakaoshuhudia vitendo hivyo ili kutoa taarifa zitakazowawezesha polisi kuchukua hatua mapema.
Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Simu: 0717055551 au 0755925656. muhibu72@yahoo.co.uk

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
polisi wamejifunza kuzuia maandamano ya kudai haki lkn sio mbinu nyingine ujinga sana huu ingekuwa mataifa mengine yanamoishi binadam ?
 
Back
Top Bottom