Polisi, CUF ‘vita’ Dar es Salaam

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
266
ILIKUWA kama filamu kwa wakazi wa Dar es Salaam jana wakati baadhi ya viongozi na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), walipolizidi maarifa Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wanafanikiwa kupeleka mapendekezo ya rasimu ya Katiba Mpya, huku risasi za moto zikitumika kujaribu kuwatawanya.

Awali juzi, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, lilizuia kufanyika kwa maandamano hayo kwa madai ya kuwapo kwa mkanganyiko wa taarifa ya namna ya uwasilishaji wa rasimu hiyo iliyotumwa kwenda Jeshi la Polisi na Wizara ya Katiba na Sheria.

Kwa mujibu wa Kova, taarifa waliyoituma CUF kwenda Wizara hiyo, haikutaarifu kuwa wangepeleka mapendekezo hayo kwa njia ya maandamano huku iliyotumwa kwenda Polisi, ikisema kuwa wangepeleka kwa njia hiyo, jambo alilosema lilikuwa na tofauti ya maana.

Saa tatu asubuhi jana, wanachama wa CUF walianza kukusanyika katika Ofisi za Makao Makuu zilizopo Buguruni, Ilala, ili kuanza maandalizi ya maandamano hayo ambayo kimsingi yalikuwa kinyume cha sheria.

Wakiwa hapo, wanachama hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali na kutumbuizwa na muziki uliokuwa ukipigwa na magari mawili ya matangazo ya chama hicho huku wakizifuatisha, ukiwamo wa ‘kama noma na iwe noma sikubali leo narivenji mimi’ ulioimbwa na msanii wa kizazi kipya, Kaka Man.

Ilipofika saa nne, magari matano ya Polisi huku yakiwa na askari wa kutuliza ghasia, yalifika hapo na kuwataka wanachama hao kusitisha maandamo kama vile ilivyoagizwa; lakini agizo hilo lilipuuzwa na wanachama hao na kusisitiza kutimiza azma yao ya kuandamana hadi wizarani.

Ilipofika muda huo, maandamano hayo yalianza, lakini yakiwahusisha wanachama peke yao waliokuwa wakitembea kwa miguu na kubeba mabango mbalimbali huku viongozi wao, akiwamo Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Julius Mtatiro, wakikwepa kuungana na wanachama hao na kutumia magari mawili kuondoka eneo hilo na kwenda wizarani eneo la Barabara ya Sokoine karibu na Magogoni.

Aidha, maandamano hayo yaliyokuwa yakipita katika Barabara ya Uhuru, yalipofika Buguruni Malapa yalikutana na ulinzi mkali wa askari hao na ghafla umati huo ulitawanyika na kukimbilia mitaani baada kuliona gari maalumu la Polisi Namba PT 0886, lililokuwa limebeba maji ya kuwasha.

Baada ya kukimbilia huku na huko, baadhi ya wanachama hao walikutana na kuungana tena katika Mtaa wa Kilwa na kuendelea na maandamano hayo, hali iliyowafanya askari Polisi kufyatua risasi za moto zaidi ya saba hewani ili kuwatawanya.

Kutokana na hali hiyo, waandamanaji hao walikimbia kuelekea maeneo mbalimbali huku magari ya Polisi zaidi ya 10 yakikatiza katika mitaa hiyo ya Ilala kwa lengo la kuwatawanya wanachama hao ambapo pia ilifanikiwa kuwakamata wanachama wanne waliopelekwa katika Kituo cha Polisi cha Karume.

Akizungumza baada ya kukabidhi rasimu hiyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Oliver Mhaiki, Mtatiro alisema rasimu hiyo yenye sura 36, Ibara 130 na kurasa 88, aliyosema iliandaliwa kwa miaka minne, imezingatia mahitaji ya Watanzania wa sasa, hivyo ni wajibu wa Serikali kuipitia na kuifanyia kazi ipasavyo.

Alidai Watanzania wamechoshwa na Katiba yenye viraka inayowaongoza kwa sasa, hivyo rasimu iliyotolewa na CUF imezingatia mahitaji yote muhimu na kwamba ndiyo mkombozi kwa maisha ya Watanzania masikini.

Alidai chama hicho kinajiandaa kulidai Jeshi la Polisi Sh milioni 10 sambamba na kuandaa maandamano mengine kwa ajili ya jeshi hilo kwa kile alichodai kuwa limevuruga maandamano yao licha ya kulipatia taarifa tangu Desemba 21, mwaka huu kuwa litafanya maandamano hayo.

Akipokea rasimu hiyo, Katibu Mkuu Mhaiki alisema atayawasilisha mapendekezo hayo kwa Waziri wake, Celina Kombani, kama ambavyo chama hicho kilivyokusudia kufanya huku akiwaomba viongozi hao kuwa watulivu wakati taratibu zingine zikiendelea kufanywa na Serikali.

Kwa upande wake, Kova akizungumza jana juu ya tukio hilo, alisema Polisi hawana ugomvi na chama hicho wala hawakuwazuia kupeleka rasimu hiyo, isipokuwa walitaka wapeleke kwa njia ya kawaida na siyo maandamano kama walivyofanya jana.

Alisema Serikali ilishazungumza suala la Katiba Mpya kuwa linazungumzika na linafanyiwa kazi, kwa hiyo maandamano ya chama hicho cha upinzani hayakuwa na tija yoyote.

Alisema wametumia nguvu za wastani kuwatawanya wana CUF na watu tisa wanashikiliwa na jeshi hilo na hakuna aliyejeruhiwa katika maandamano hayo, na Polisi kupitia Idara yake ya Upelelezi inafuatilia suala hilo ili kuangalia hatua gani itachukua kutokana na kukiukwa kwa amri yao.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom