Pinda aivalia njuga katiba mpya

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameamua kulibeba suala la madai ya katiba mpya, akisema kuwa atamshauri Rais Jakaya Kikwete kuunda timu ya kushughulikia suala hilo.Pinda alitangaza uamuzi huo jana katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam katika kipindi ambacho kilio cha katiba mpya kinaongezeka kila kukicha.Tangu Chadema ilipoamua kususia matokeo ya uchaguzi wa rais kwa kutoka nje wakati Jakaya Kikwete akitoa hotuba ya kuzindua Bunge na kuanza harakati za kudai katiba, suala hilo limezungumwa kwa kina na watu wa kada tofauti ambao wametahadharisha kuwa nchi inaweza kuingia matatizoni iwapo serikali haitashughulikia uandikaji wa katiba mpya.

Rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wa zamani, Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Jaji Mkuu Agustino Ramadhan, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jophn Tendwa na majaji wengine wamezungumzia umuhimu wa katiba mpya na kuungwa mkono na wanasiasa na viongozi wa dini.

Tendwa, ambaye ni mtumishi wa umma, ndiye aliyeenda mbali zaidi baada ya kueleza bayana kuwa katiba ya sasa inampa madaraka makubwa rais na kuonya kuwa kama katiba mpya haitaundwa, kuna hatari ya nchi kuharibikiwa baadaye.
Jana, Pinda alilazimika kuzungumzia suala hilo katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari.
“Isije watu wakadhani serikali ina kigugumizi; hapana. Sasa mjadala umeiva na ni vizuri lizungumzwe kwa utaratibu. Nipo tayari kuzungumza na rais. Nitamshauri mzee (rais) na nitaweka nguvu zangu huko... hilo halitawezekana tusipoweka ‘initiative’ (juhudi),” alisema Pinda.

"Watu wasifikiri wala kuona kuwa serikali haioni kama madai ya katiba mpya kuwa si ya msingi.
“La pili, tunataka kuzungumza machache, lakini kubwa ni hili la katiba mpya. Kumekuwa na maelezo mengi, marefu, mjadala mkali;
sasa hili nataka niseme tusione kama madai ya katiba si ya msingi sana; hapana. Ni ya msingi. Kwa serikali mabadiliko ya katiba ni utaratibu wa kawaida kwani ni jambo lililo ndani ya katiba,” alisema Pinda.

“’All along’ Watanzania wameendelea kuibuka na kudai tume huru ya uchaguzi na katiba mpya. Tulipofikia tunaulizana 'kuna ugumu gani kukaa na kuandika katiba mpya?"
Aliongeza kusema: "Mimi binafsi sioni tatizo kwa hilo kufanyika, lakini kama serikali zipo namna mbili za kulishughulikia. Moja ni kutafuta utaratibu wa kumshauri rais aunde kamati ya watu wangalie maeneo gani ya kuingiza katika katiba hata ikibidi wananchi waulizwe yatoke ya kuwekwa mezani kwa kuhusisha vyama vya siasa na wanazuoni.”
Pinda aliitaja njia ya pili kuwa ni rais kuunda timu yake ya kiserikali itakayoangalia mapendekezo ya tume zilizoundwa awalikuangalia marekebisho ya katiba na kuchukua mapendekezo yaliyojirudia yatakayoonekana kufaa kuingia katika katiba.

“Tume zote zina viporo vya kuanzia na kuchukua kuliko hali ilivyo sasa ambayo kila mmoja anasema lake kuhusu katiba,” alisema Pinda.
Alisema kutokana na tume hizo yapo yaliyotekelezwa na yale ambayo yaliahirishwa akisema kuwa pengine ni kutokana na wakati. Hata hivyo alisema ni bora kuruhusu tume itakayokuwa pana na kuyatazama mapendekezo ya tume za awali, kuangalia na kushauri akisema kuwa huenda ikaona mambo mengine.

“Ni bora kuruhusu tume pana ya kutazama, tushauri na kuangalia, pengine tukiyaona ya utawala si katiba mpya bali kitu kingine. Katika katiba yapo mema mengi tusiangalie ubaya tu, katiba hiyo ndiyo imetufikisha hapa taifa likiwa na sifa za utawala bora na mambo mengine,” alisema Pinda.

Katiiba ya kwanza ya Tanganyika iliundwa na mkoloni mwaka 1920 na mwaka 1961 ikaundwa katiba mpya baada ya uhuru na ikadumu mwaka mmoja baada ya katiba ya Jamhuri kuundwa mwaka 1962. Katiba ya Jamhuri ilidumu hadi mwaka 1964 wakati Tanganyika ilipoungana na Zanzibar na hivyo kuwa na katiba ya Muungano.

Katiba ya Muungano haikuandikwa upya hadi mwaka 1977 na baada ya hapo kumefanyika marekebisho 13, yakiwemo ya mwaka 1992 wakati serikali iliporejesha mfumo wa vyama vingi, lakini wanazuoni wameyapachika jina marekebisho hayo kuwa ni viraka.

Kuhusu mabadiliko ya katiba ya Zanzibar kusigana na katiba ya Muungano, Pinda alisema mapendekezo yaliyozaa marekebisho hayo ndiyo yaliyozaa maridhiano na kwamba katiba lazima ilenge maridhiano.
“Kuhusu Zanzibar tusizue maneno. Mapendekezo ya wenzetu ndiyo yaliyozaa maridhiano, katiba lazima ilenge maridhiano,” alisema Pinda.

Hata hivyo alisema kuwa kazi iliyobaki ni ndogo ambayo alisema ni kuichukua katiba ya Zanzibar na kuioanisha na ya Muungano ili mtiririko wake uende vema bila kuathiri upande mmoja.
“Ukienda hivyo ugomvi utaisha, kazi hiyo tayari tumeianza,” alimaliza Pinda.
 
Back
Top Bottom