Halisi
JF-Expert Member
- Jan 16, 2007
- 2,802
- 613
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo anazungumza katika mazishi ya Askofu Mayala Mwanza ambako anazungumzia ufisadi na maovu mengine, lakini anaonekana kukemea ufisadi huku akionekana kuwabeza wanaopambana na ufisadi. Iko live Star TV.
Yuko JK na Mkapa
Yuko JK na Mkapa
Na Betty Kangonga
Tanzania Daima
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewashukia makamanda wanaopigana vita dhidi ya ufisadi kwa kuwataka wawe na dhamira ya kweli katika kukabiliana na ufisadi nchini.
Kardinali Pengo, alisema bila dhamira ya kweli, vita hiyo haiwezi kufanikiwa kwani wanaopiga kelele bila kusukumwa na dhamira ya kweli, wataonekana kama wana wivu kwa kukosa fursa ya kuwa mafisadi.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa ibada ya kumuaga Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Anthony Mayala (69), aliyefariki dunia Agosti 19 na kuzikwa jana katika Kanisa la Mtakatifu Epifania, Parokia ya Bugando, jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana jana jijini Dar es Salaam, Pengo alisema Watanzania wengi wanaokemea ufisadi, wanaongeza hasira kwa jamii, kwani uovu huo bado unaendelea kufanywa na mafisadi kwa vile wapiganaji wenyewe hawana dhamira ya kweli.
"Wote tunalalamika na kulaani matendo ya ufisadi, kama kweli tungekuwa tunalaani kutoka ndani ya mioyo yetu, basi vita hivi vingepungua ama kuisha kabisa nchini kwetu.
"Kupigia kelele ufisadi, bila dhamira ya kweli kunaonyesha hisia tu na ni bora kuacha kulizungumzia suala hilo kwani linaongeza hasira kwa wananchi na hata kusababisha amani iliyokuwepo nchini kutoweka," alisema.
Pengo alisema, makamanda wa ufisadi, lazima wajiulize kwanza wao binafsi wamechangia kwa kiasi gani katika kuwaibia wananchi, ndipo waanze kupiga vita ufisadi kwa kuwa hawana makosa.
"Hakuna aliye mkamilifu, wengi wetu tumekuwa tukiwapinga mafisadi, huku sisi tukijiona wema wakati kwa upande mwingine bado wanafanya ufisadi na kuwaibia watu, ndiyo maana vita hii kamwe haiwezi kuisha,'' alifafanua Kardinali Pengo.
Bila kutaja majina ya watu, Kardinali Pengo alisema baadhi ya wapiganaji wa ufisadi, wanafanya hivyo kwa kuwa wamekosa nafasi ya kuwa mafisadi, hivyo wanawaonea wivu wenye nafasi ya kufanya ufisadi.
Aliwageukia maaskofu wenzake kwa kuwataka wawe imara na wasiwe tayari kuyumbishwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, kwani dini na siasa kamwe haviwezi kwenda pamoja.
"Mambo yanayoendelea kutokea katika nchi yetu hatuelewi yanatupeleka wapi, kwani tunashangazwa na chama kuingilia masuala ya maaskofu ambayo ni mema, kwani yana lengo la kusaidia jamii iwe na viongozi wenye maadili.
"Leo unafikia hatua ya kumwambia askofu haruhusiwi kufanya jambo lolote mpaka akutane na chama na kupewa ruhusa ya kujua namna ya kuandika waraka huo, huko ni kutaka kuingilia mamlaka ya Kimungu na kamwe haitawezekana.
"Waacheni maaskofu wafanye kazi zao na wasifundishwe kazi, kwa maana kuandika waraka huo ni mamlaka kutoka kwa Mungu na si kwa uwezo wao, vyama visilazimishe kuwa lazima vitoe ushauri, huo ni upuuzi na inaonyesha kuchanganyikiwa," alieleza Kardinali Pengo.
Ingawa Kardinali Pengo hakumtaja mtu, lakini kwa kauli hii ni dhahiri kuwa alimlenga mkongwe wa siasa nchini, Mzee Kingunge Ngombale- Mwiru ambaye siku za hivi karibuni, alijitokeza hadharani kuupinga waraka wa Kanisa Katoliki, kwamba unaweza kuhatarisha amani na utulivu nchini.