Paschally Mayega - Wananchi wanataka majibu

sulphadoxine

JF-Expert Member
Nov 1, 2010
2,257
645
RAIS wangu, moyo wangu hauna amani. Laumu imeuvunja moyo wangu nami nimelegea sawa na utete dhaifu usukumwao na maji ya mkondo yaendayo kasi.
Niionapo nchi yangu ikiwekwa rehani moyo wangu husukwasukwa kama mwale wa mshumaa unavyosukwasukwa na upepo mkali. Kila nikimtazama wakuisikitikia simwoni. Machozi yangu ndiyo yamekuwa chakula changu. Nami si mtu tena bali mdudu, naweza hata kuhesabu mifupa ya mwilini mwangu.
Nchi yangu inapukutika huku wananchi wenzangu wakizidi kusokomezwa katika kilindi cha umaskini licha ya nchi yao kujaliwa kila aina ya utajiri. Raslimali za taifa zinawanufaisha wageni kuliko wenye mali.
Makampuni makubwa kama mahoteli na makampuni ya simu yamekuwa yakibadilika majina kila muda wa msamaha wa kodi unapoisha. Watanzania tuulizane haya yote yanafanyika kwa faida nani? Nchi yetu haina viongozi? Au ndiyo haohao? Bila mkono wa viongozi haya yanawezekana vipi?
Watanzania bado wanayakumbuka majina makubwa kama Tritel, Celtel, Zain, Mobitel, Buzz, Sheraton, Royal Palm, Movinpic na mengine mengi. Yalipokwisha kufaidi muda wao wa msamaha wa kodi wananchi waliambiwa yameuzwa! Wanachokiona wananchi kuwa kimebadilika ni jina tu! Ni kodi kiasi gani inayopotea?
Kama kingewekwa kipengele kinachoilazimisha kampuni iliyonufaika na msamaha wa kodi wa miaka mitano kuendelea na biashara japo kwa miaka mingine mitano ili serikali nayo inufaike kwa kodi. Au kampuni nunuzi irithi msamaha wa kodi uliotolewa.
Kama Zain inanunuliwa na Airtel au Buzz inanunuliwa na Tigo, vivyo hivyo kama Movinpic inanunuliwa na Serena mnunuzi arithi msamaha wa kodi katika mkataba wa mauziano yao. Vinginevyo muuzaji afunge kila kilicho chake aende. Tutaendelea kuona mabadiliko ya majina tu mpaka lini?
Mitambo ni ileile, majengo ni yaleyale, vitendea kazi ni vilevile na wafanyakazi ni walewale. Je, wafanyakazi ukiacha meneja mkuu hufutwa kazi wakapewa mafao na kampuni inayoondoka? Lini kampuni nunuzi (mpya) iliwahi kutangaza nafasi za kazi?
Kama serikali ingedhibiti hili na ikakusanya kodi stahili mwalimu gani angekuwa bado anaidai serikali? Migomo ya Wanafunzi wa vyuo vikuu wanapodai mikopo waliyokubaliwa ingetokea vipi? Watoto wa shule za msingi wangesomea vipi mavumbini wakati baadhi ya shule zao zimezungukwa na misitu ya mbao? Wafanyakazi wa kima cha chini katika nchi hii wangeendelea kunyanyasika kwa mishahara duni?
Rais wangu viongozi wetu hawalijui hili? Hakuna wanaonufaika na ufisadi huu? Wananchi wanaona utajiri mkubwa walionao baadhi ya viongozi wetu na familia zao.
Watawatofautisha vipi na dhambi hii? Kama baba hukusimama kukomesha dhuluma hii nani ataliokoa Taifa? Kuliacha taifa liangamie ni kujiangamiza sisi wenyewe.
Alhamisi iliyopita nilibahatika kukutana uso kwa uso na wanawema Rashid na Masawe wawili kwa mara ya kwanza. Pamoja na mzaha alioutoa Rashid kuwa Kitabu cha Mwalimu Mkuu wa watu kina CD4 za uraia nyingi sana, lakini nilipowatazama usoni niliweza kuuona uchungu uliokuwamo ndani ya mioyoni yao kuhusu mustakabali wa nchi yao.
Rashid aliniambia mambo mawili ambayo yananifikirisha hadi sasa. La kwanza akasema, “Mwalimu, kasoro kubwa inayowakabili baadhi ya viongozi wetu ni kwamba wameondoa woga wa uwepo wa Mwenyezi Mungu”.
Nikamkumbuka Adamu Malima, Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Huyu alipata kusema, “Bei ya umeme lazima ipande kulingana na hali ya maisha.”
Kuna ulazima wa kuongeza gharama. Ongezeko la umeme ni kwa watumiaji wakubwa tu na si kwa watumiaji wadogo, watumiaji wadogo lazima waachwe ila mahoteli, viwanda vikubwa lazima vipandishiwe”.
Ndugu Rais, kwa ufahamu wa Waziri Malima anadhani bidhaa kama simenti, mabati na nyingine zinazozalishwa na viwanda vikubwa watumiaji ni viwanda vyenyewe? Si mabati hayohayo na simenti hiyo hiyo ndiyo wanayotumia watumiaji wadogo kujengea nyumba zao?
Kama viwanda vikubwa vikipandisha bei ya bidhaa hizo kutokana na bei kubwa ya umeme ambayo TANESCO imeomba kuongeza kwa aslimia 155 muathirika wa bei hiyo ni nani kama si mtumiaji wa mwisho wa bidhaa hizo ambaye ni mwananchi maskini?
Ni kweli hili ni gumu kuingia katika ufahamu wa waziri, au ni kweli kama alivyosema mwanamwema Rashid kuwa ‘viongozi wetu wamekosa uwoga wa uwepo wa Mwenyezi Mungu? Unadanganya wananchi wenye uelewa mdogo wanadhani kuwa serikali inawajali, kitu ambacho si kweli.
Akaona haitoshi akaongeza kusema kuwa bei isipopanda kama ambavyo Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) lilivyoomba, kutakuwa na athari kubwa ya kukwamisha hata sekta binafsi kuingia katika sekta ya umeme. Kauli hii haikubaliki hata kidogo kwani hata yeye mwenyewe anajua ukiritimba uliopo serikalini.
Naibu waziri aache visingizio visivyokuwa na maana kwa sababu anajua kuwa mkoani Singida kuna mradi mkubwa wa umeme unaotumia upepo, lakini umeshindwa kuanza kwasababu TANESCO ilikuwa na kigugumizi cha kuingia makubaliano ya kuanza kazi ya kuzalisha umeme. Maneno haya marehemu Ebo aliyaita maneno ‘bofu, bofu’. Hayastahili kutoka katika kinywa cha mteule wa rais.
Rais wangu tafakuri ya kukosekana woga wa uwepo wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa viongozi wetu ikanipeleka mpaka kwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri. Huyu ametangaza kuwaongezea posho wabunge kwa maelezo kuwa hali ya maisha ya wabunge Dodoma ni ngumu sana. Hakuwaeleza wananchi hali ya maisha ya Wagogo na wananchi wengine wasio wabunge waishio Dodoma ikoje.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa uchungu mkubwa amesema kiongozi anayejali maisha ya watu kamwe hawezi kijifikiria mwenyewe, lakini katika tukio la posho za wabunge ameshangazwa na uamuzi wa Spika wa kuongeza posho za wabunge.
Akionyesha kuchomwa sana moyoni alisema: “Hivi karibuni tumesikia wabunge wetu wameongezewa marupurupu ya posho wakidai hali ya maisha imekuwa ngumu wala hawakujali ugumu wa maisha waliyonayo wananchi wanaowaongoza. Najiuliza huyu kiongozi ni wa namna gani anayejifikiria yeye kwanza kabla ya wengine?”
Mwadhama hana shida ya chakula wala mavazi kama alivyo Spika Anne Makinda. Lakini ni nini kinachowafanya wawili hawa wawe tofauti; mmoja aonyeshe kujali utu wa mwanadamu na mwingine ajionyeshe kuwa ni mbinafsi wa kupindukia? Mmoja wao lazima atakuwa amepoteza woga wa uwepo wa Mungu.
Rais wangu kama CCM walipanga kumweka mwanamke awe Spika wa Bunge la Jamhuri kwa kutumia kigezo kimoja tu kuwa ni mwanamke walifanya makosa makubwa sana.
Madhali mbio za urais zimeanza, Watanzania lazima wajipange kujibu mapigo kama CCM watakuja na hoja kuwa rais ajaye lazima awe mwanamke. Mwanamke atakayekubali kwa kigezo tu kuwa ni mwanamke ajue hatufai! Kujali uwepo wa Mwenyezi Mungu iwe ndiyo kwanza.
Neno la pili, ndugu Rais aliloniambia ndugu Rashidi, alisema: “Mwalimu Mkuu ulipoandika kuhusu Edward Lowassa baadhi ya wenzetu waliniambia kuwa Mwalimu Mkuu naye amenunuliwa na mafisadi.
Lakini baada ya Edward Lowassa kumvika gamba mwenye gamba lake (sikuelewa mara moja alimaanisha nini) wote katika umoja wetu tulikubaliana kuwa Mwalimu mkuu ni kionambali. Uliona mbali kabla yetu katika hili.”
Baba, dakika saba alizotumia Edward kueleza hali ilivyokuwa wakati wa pilikapilika za Richmond zililipasua kabisa lile pazia jeusi lililokuwa limefungwa na baadhi ya watu hasa genge la mafisadi waliojiita wapambanaji katika vita hewa ya ufisadi kwa lengo la kuupotosha umma. Ukweli umewekwa hadharani sasa wananchi wameelewa.
Wanachongoja ni majibu. Tunaelewa kuwa nchi yetu haina miiko hata maadili kwa viongozi, lakini tunapaswa kutawaliwa kistaarabu.
Ustaarabu kama uungwana ulivyo ni kanuni. Kanuni lazima zifuatwe. Muungwana akikosea hupisha shari. Ukurasa wa 47 katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa: “Ndugu Rais, ukweli unapotuumbua tuukubali. Tuwe radhi kuadhibiwa maana binadamu wote tumeumbwa na mapungufu.”
Katika Richmond tulifanya dhambi kubwa na tulipotaka kujinasua kwa hila tukatenda dhambi kubwa zaidi kwa kuwatwisha uchafu wetu waja wa Mwenyezi Mungu ambao hawakuwa na hatia yoyote kwa dhambi hii.
Mwanamwema Daniel kutoka Mbeya aliniandikia akasema: “Mayega: Mungu akupe upeo na maono uweze kutufunulia mengi yaliyojificha. Suala la Lowassa na akina Sitta umelizungumza muda mrefu sana na sasa yametimia. Ni aibu kwake…. na kwa taifa, mimi mpaka natetemeka. Sijui safari yetu mwisho wake ni wapi”
Ndugu rais msimamo wangu uko wazi, kuusimamia ukweli siku zote za maisha yangu. Sitajali kama kwakufanya hivyo nitaonekana namchukia malaika au namtukuza shetani. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye tegemeo langu. Naye hataniacha hata wakati wa shida!
Kwa katiba yetu Rais wa nchi hii ni mmoja tu, Jakaya Mrisho Kikwete. Wote lazima tumheshimu Rais wetu na tumsaidie.
Baba, utufundishe kusali. Tufundishe kuomba dua kwa Mwenyezi Mungu ili wenyewe kwa wenyewe sisi tupendane kwa maana tu wana wa mama mmoja Tanzania.
Kwa muda mrefu tumeisononesha na kuitia simanzi mioyo ya wenzetu wasio na hatia. Wanaoasisi na kuendeleza siasa za chuki binafsi washindwe na walegee. Sisi siyo malaika. Kama tulijikwaa tupishe, ili kujiepusha na laana ya kisasi!
Tanzania ni ya Watanzania wote! Ni kwa uungwana tu tunaweza kuidumusha amani ya kweli katika nchi hii aliyotujalia Muumba wetu katika umoja wetu. Yakikutokea yakutokea, ogopa uwepo wa Mwenyezi Mungu! Kisha, pima mwenyewe!
 
Back
Top Bottom