Paschally Mayega : Rais wangu Kikwete,Wabunge Makini hutafakari hoja zinazotolewa

mwankuga

JF-Expert Member
Aug 30, 2010
334
120



RAIS wangu, maandiko yanasema amtumaye mpumbavu hujikata miguu na kunywa hasara. Wananchi wamewatuma wawakilishi wao bungeni wakawawakilishe. Bunge linaendelea na vioja vya kibunge navyo vinaendelea huku nchi ikitetereka kwa kukosa muhimili imara.


Watu wanatembea na nguo zao za ndani juu ya vichwa vyao huku wakidhania kuwa eti kuna watu wanaweza wakawaheshimu.
Ndugu Rais, wabunge wanaowawakilisha wananchi wanatoa hoja zao bungeni. Wabunge makini wanatafakari hoja zilizotolewa bungeni. Mavuvuzela huzomea hata Bungeni huku wakiwa wamebeba vichwa vyao vya nazi.


Nazi haifikiri, kwa sababu hiyo naamini ingepewa mdomo ingezomea kila kitu. Hawa ndiyo wawakilishi wa wananchi! Kazi kweli kweli! Maandiko yanasema: “Mwana mwenye akili ni fahari kwa babaye bali mwana mpumbavu ni mzigo kwa mamaye!


Ndugu Rais kinachogombaniwa hapa siyo ukubwa wala udogo wa posho! Kinacholaaniwa hapa ni uharamu wa posho hizo. Mtu anapokuja na sababu kuwa mbona hata serikalini posho ni kiwango hicho hicho ni wakumhurumia! Mpofu huyu! Wanaozikataa hawakatai kiwango wanakataa wizi, dhuluma na ufisadi wa posho hizo.


Kwa mawazo yake, wabunge wana haki ya kula uchafu eti kwa sababu tu hata serikalini wanakula uchafu huohuo! Haelewi kuwa somo lililopo hapa ni kuondoa posho au haramu au uchafu au wizi huu popote zinapotolewa iwe ni kwa wabunge, serikalini au kwingineko.
Waziri mkuu anapotetea haramu au ufisadi huu, ‘mimi napata taabu sana!’ Lakini hawa ndiyo viongozi wetu!


Mwanamwema ambaye hakuniandikia jina lake aliniuliza: “Kaka Mayega hivi kauli tata hizi zinazotolewa na viongozi wetu kuhusu posho za wabunge kati ya Ikulu, waziri mkuu, Spika na wabunge tujifunze nini?” Nikamwambia yakujifunza hapa ni mengi lakini cha muhimu hapa nyinyi kufanya kwanza utafiti msije mkajikuta siku moja mnatawaliwa kihuni.


Ikulu haina maana nyingine yoyote zaidi ya Rais. Rais akisema sikusaini ongezeko la posho, kauli ya mkuu wa nchi lazima iheshimiwe. Spika Anne Makinda anaposema hapana, rais alisaini wakati rais amesema hakusaini, anacholiambia taifa Spika ni kuwa rais ni mwongo. Nchi haiwezi kuwa na rais mwongo.


Anayemfanya rais aonekane mwongo mbele ya watu wake lazima awajibishwe! Wengine hatukubali rais wetu adhalilishwe kwa kiwango hiki.
Waziri Mkuu anasema rais alisaini. Wananchi wamkubalie nani? Kwa hakika mmoja au wawili kati ya watatu hawa atakuwa anasema uongo.


Anataka wananchi wamwamini yeye kuwa ndiye anasema kweli na kwamba Rais anakataa tu? Rais huyu ataonekanaje mbele za watu wake? Kwa nini rais wetu asiwachukulie hatua watu wanaotaka aonekane kigeugeu? Na kwanini wakubwa zetu hawa wanabishana hadharani?


Baba ile taarifa kuwa eti ulisema watumie busara zao ndiyo inayoharibu kila kitu. Nchi inatakiwa iongozwe na busara ya Rais! Mkuu wa nchi hata anapotegemea busara za wengine huwa haiwekwi hadharani kama hivi!


Uongozi wa nchi haui hivi. Tamko la Rais kwa masuala kama haya yanapaswa kuwa elekezi. Hapa fanyeni hivi na hapa msifanye hivi, fullstop! Huyu aliyetoa tamko hilo awajibishwe.

Viongozi wetu lazima kila mara wakumbuke kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pale aliposema, “Ukipewa kazi ya kuongoza nchi lazima ujiheshimu. Kazi za kihuni ziko tele. Uende ukafanye uhuni wako kule”


Rais wangu tunakoelekea ni kubaya. Huko nyuma tulikotoka wengine hatukuwahi kusikia Rais anaweza kumwita mtu halafu eti mtu yule akatae mwito huo. Asiende, halafu rais naye hasemi kitu! Hapana! Lazima tuikatae hali hii. Wananchi wameambiwa wabunge CCM wagoma kukutana na Kikwete. Wajipanga kukwamisha muswada mabadiliko ya katiba. Huu ni mgongano wa mihimili miwili ya nchi. Hapa ndipo nchi ilipofikishwa Mpaka wengine wanatishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais wake mwenyewe!


Kama CCM na serikali yake ingekuwa ni nguo basi imebaki ni midabwada. Tambara lililoruka ambalo kushonwa kwake karibu haiwezekani.
Rais wangu nimevutiwa na ziara ya kichama aliyoifanya mlezi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Abdulrahman Kinana hivi karibuni. Makamu wa Rais Gharib Bilali amekuwa akienda kila mahali siku hizi. Ziara zake nyingi ni za kukagua miradi ya maendeleo. Kinana aliwaendea wanachama (wananchi) wenyewe na kukaa nao akawasikiliza shida zao. Kasoro kubwa ya uongozi tulionao, hakuna kiongozi aliyetayari kukaa na wananchi na kusikiliza shida zao. Wengi ni viongozi wa kukagua miradi. Utafikiri ni ‘masupavaiza’.


Ndugu Rais nimepata bahati ya kuisoma risala ya Katibu wa Mkoa wa Dar es Salaam –CCM, Abilahi Mihewa, aliyomsomea Kinana.

Katika baadhi ya sehemu ilisomeka hivi; “Tunakushukuru kwa ziara yako hii ya kutuamsha, kutuhamasisha, kutuelimisha na kututia nguvu. Umewatembelea wanachama na wananchi huko waliko katika mashina na matawi na kuwasikiliza juu ya kero zao na kuchukua hatua za kuzishughulikia.


Wanachama wamepata nafasi kubwa ya wewe kuwasikiliza na kupokea waliyoyasema kwa kukosoa na kushauri na umewapa maelezo ya ufafanuzi katika baadhi ya mambo hayo. Umewapa matumaini makubwa kwa kuahidi kuyafikisha kwenye ngazi za juu (vikao) na kwa Mwenyekiti wa chama. Aidha umewajaza imani na matumaini makubwa pale ulipowaahidi kuwa utawarejeshea maamuzi ya hatua zitakazochukuliwa na mamlaka husika.


Umeamsha ari, matumaini na msisimko mkubwa wa uhai wa chama kwenye mioyo ya wanachama wetu wa CCM jumuiya na wapenzi wa CCM. Kwa hakika umewasha moto wa uhai wa chama na jumuia zake mkoani Dar es Salaam. Tunakuahidi kuwa moto huu hautazimika, utaendelea kuongezwa kasi ya kuwaka kama vile unavyomwagia petroli kwenye moto unaowaka.”


Risala ilijumuisha kero lukuki zinazowakabili wanachama (wananchi) ikiwa ni pomoja na mfumuko wa bei wa vyakula. Ikasema: “Hali hii inafanya wananchi wa Dar es Salaam sasa kula mlo mmoja kutoka milo miwili ya awali, tena milo ya kupunguza makali ya njaa tu Siyo milo inayowapa afya njema. Serikali iliishatoa maelekezo ya wananchi kuuziwa mahindi na unga kwa bei ya sh 500 kwa kilo. Mahindi hayo hakuna, wala unga hakuna na hadi sasa serikali haijatoa maelezo kwa nini hilo halijatekelezwa.”


Mimi si mwanachama wa CCM kwa sababu mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Kwa hili napenda kuwatahadharisha wapinzani kuwa kama aliloliibua Kinana litafanyiwa kazi, basi kazi ya upinzani itakuwa ngumu sana. Mtaani wanasema ‘hapendwi mtu, pochi lako tu’. Hapa napo hakipendwi chama bali utendaji mahiri katika kutatua kero za wananchi na hivyo kuwapunguzia ugumu wa maisha. Utendaji mbovu wa serikali ndiyo kwa kiasi kikubwa umeupaisha umaarufu wa wapinzani.


Sijui kama kazi hii anayoifanya Kinana moyoni mwake ni kutaka kusaidia chama chake au wanachama wa chama chake. Ingekuwa ni ndani ya serikali tendaji hii ndiyo kazi ya waziri mkuu aliye mtendaji. Na wakati fulani ni kazi ya Waziri wa Mambo ya ndani. Tumeyaona haya ya utendaji mahiri uliotukuka wakati wa awamu ya kwanza waziri mkuu akiwa hayati Edward Moringe Sokoine. Tumeyaona haya ya utendaji mahiri uliotukuka wakati wa awamu ya pili Waziri wa Mambo ya Ndani akiwa Augustine Lyatonga Mrema. Tumeyaona haya ya utendaji mahiri uliotukuka mwanzoni mwa awamu ya nne Waziri Mkuu akiwa Edward Ngoyai Lowassa. Walichomshinda Kinana hawa, ni kwamba wao walikuwa na mamlaka ya kutoa siku saba. Kinana hana mamlaka hayo. Kinana anategemea maamuzi ya kunakohusika, maamuzi ya vikao na hasa maamuzi ya Mwenyekiti wake ndugu Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ndiye Rais. Hapa ndipo kazi njema aliyoifanya Kinana inapofanana na ziwa linaloingiwa na luba.


Rais wangu kama Abdulrahman Kinana angekuwa na mamlaka ya kutoa siku saba halafu akatenda haya anayotamani yatendwe maisha bora kwa kila Mtanzania yangewezekana tena kwa muda mfupi. Lakini je atasikiwa ndani ya chama chake? Watendaji ndani ya chama cha mapinduzi na ndani ya serikali wako ‘bize’ na mafisadi wa kuchonga. Mafisadi waliochukua mahindi ya serikali kwa bei poa ili unga kwa mwananchi uwe bei poa nao wakachakachua hawaguswi.


Kwa wapambanaji wa ufisadi hawa si mafisadi. Wanalindwa! Waziri mkuu wa sasa aliagiza kilo ya sukari iuzwe kwa wananchi si zaidi ya sh 1,700 lakini leo wananchi wananunua kilo moja kwa zaidi ya sh 2,400 na waziri mkuu yupo kama hayupo. Yuko ‘bize’ bungeni anatetea posho zao. Waziri mkuu huna mtu wa kukwambia achana na hizi posho haramu

zinapunguza hadhi? Shughulikia agizo la rais wako la mahindi yake ili unga kwa mwananchi uwe sh 500/= kwa kilo! Kama agizo lako mwenyewe la sukari kuwa sh 1,700 limekushinda uambie umma utumie nguvu yake! Kweli aliyeshiba hamjui mwenye njaa! Nikifikishwa hapa, ‘Napata taabu sana’. Huko huko kwa watu walewale ndiko mwanamwema Abdulrahman Kinana anakotegemea utekelezaji wa yale aliyoyaibua. Mawe! Sikukatishi tamaa Kinana kwa sababu hata mafuriko yaliyoikumba Dar es Salaam yalikuwa hayajawahi kutokea kwa kipindi chote cha miaka 50 iliyopita! Kazi uliyoiibua kwa watendaji waliopo ni ngumu sawa na kupasua jiwe.

Lakini pamoja na imani yako jifariji kwa maneno ya Kristu, alipoona wanafunzi wake wamekata tamaa baada ya kuwaambia kuwa tajiri kuingia mbinguni ni sawa na Ngamia kupita katika tundu la sindano aliwapoza kwa kuwaambia kuwa Mungu akipenda kila kitu kinawezekana. Nakupoza, kama Mwenyekiti (Rais) wako atakusikia akazingatia na kuyafanyia kazi yote utakayomwambia Tanzania yenye maziwa na asali inawezekana!

Ndugu Rais alichokiibua Kinana kikipata mtendaji mahiri aliyetukuka kinaweza kuifanya ile ndoto ya mchana ya CCM kutawala kwa miaka 100 kuwa kweli.


Huyu amerudi kwa mwananchi wa kawaida. Shida kuu ya mwananchi wa kawaida ni ugumu wa maisha si chama cha siasa. Vijana wetu hawana ajira na serikali ya CCM haionyeshi kujali. Hata wale waliojiajiri kwa biashara ndogo ndogo kama saluni, kuuza maji baridi, kuchomelea nakadhalika, bado wanakwamishwa na tatizo sugu lisilokwisha la ukosefu wa nishati ya umeme.


Nguvu kubwa inayotumika na askari mgambo nduli dhidi ya vijana wetu wa kimachinga ingetumiwa kuwakabili majambazi, nchi hii isingekuwa na jambazi hata mmoja.
Wanasulubiwa kama wahalifu huku wakiporwa hata kile kidogo walichokipata baada ya kujinyima sana. Waziri wa Mambo ya Ndani anaagiza vijana waliomzomea wakamatwe, hajiulizi kwa nini amezomewa. Kuna baadhi ya viongozi wetu wanadhani usultani unawezekana katika nchi yetu. Wanajitengenezea mazingira ya kuzomewa au hata kupigwa mawe.


Rais wangu, natoa angalizo kwa ndugu Kinana, mzigo aliojitwisha ni mzito lakini ni kwa ajili ya Wananchi wote wa nchi hii. Unga utakapopungua bei dukani utapungua kwa wote. Kama hutamsikiliza, usiyafanyie kazi aliyopewa na umma,
basi Kinana rudi kwa wananchi. Pita tena kote ulikopita ukawahakikishie wananchi waliokutuma kuwa ulimfikishia Mwenyekiti matatizo yao naye hakuyafanyia kazi. Acha umma uamue!
CHANZO :TANZANIA DAIMA 08/02/2012 (Tanzania Daima - Sauti ya Watu)


 
Mwankuga,
Mkuu wangu ukisoma risala hii vizuri utangundua kuwa ni hadithi za Abunuasi.. Abrahman Kinana ni kiongozi wa chama hatupo ktk uongozi wa serikali hivyo hizo ahadi ama kuwasikiliza watu tena wanachama wa CCM haimsaidii kitu huyu Pascal Mayega kwa sababu Kinana alichofanya ni kuwapa matumaini hewa wanachama wake na mlengwa sio wewe mwananchi usiyekuwa na chama.. Hoja kubwa ktk ziara hizi ni kurudisha imani ya chama kwa wananchi jambo ambalo CCM imeshindwa kulifanya kwa vitendo..

Hata huyo makamu wa Raisa kutemebela miradi ilokwisha jenga ni sawa na kukagua gwaride..Sioni haja jambo moja linalonigusa mimi ikiwa sii mwanachama wa CCM kwa sababu nina hakika Kinana mwenyewe anayafahamu watatizo ya wananchi hata kabla hatawafikia. Na alipanga uongo unaokubalika kuwapumbaza zaidi wananchi wakati chama chake kikiendelea kutowathamini wananchi kwa vitendo - Mkono mtupu haulambwi!..
 
Mwankuga,
Mkuu wangu ukisoma risala hii vizuri utangundua kuwa ni hadithi za Abunuasi.. Abrahman Kinana ni kiongozi wa chama hatupo ktk uongozi wa serikali hivyo hizo ahadi ama kuwasikiliza watu tena wanachama wa CCM haimsaidii kitu huyu Pascal Mayega kwa sababu Kinana alichofanya ni kuwapa matumaini hewa wanachama wake na mlengwa sio wewe mwananchi usiyekuwa na chama.. Hoja kubwa ktk ziara hizi ni kurudisha imani ya chama kwa wananchi jambo ambalo CCM imeshindwa kulifanya kwa vitendo..

Hata huyo makamu wa Raisa kutemebela miradi ilokwisha jenga ni sawa na kukagua gwaride..Sioni haja jambo moja linalonigusa mimi ikiwa sii mwanachama wa CCM kwa sababu nina hakika Kinana mwenyewe anayafahamu watatizo ya wananchi hata kabla hatawafikia. Na alipanga uongo unaokubalika kuwapumbaza zaidi wananchi wakati chama chake kikiendelea kutowathamini wananchi kwa vitendo - Mkono mtupu haulambwi!..
Mkuu Mkandara, mara nyingi nimecomment humu, kuwa ignorance ya Watanzania ni mtaji mkubwa wa ushindi wa CCM ndio maana Kinana anaweza kupanga uongo mtakatifu kuzidi kuwapumbaza Watanzania. Huyu ni miongoni mwa ma think tanks za CCM na kwa sasa wanausoma upepo vizuri ili 2015 waje na ilani itakayofukia mashimo yanayozidi kutoboka huku wakijiaminisha akili za Watanzania sio dynamic bali ziko static hivyo wataendelea kushinda kwa nyimbo zile zile, mbinu zile zile na watu watakaopiga kura ni wale wale walioaminishwa CCM iliumbwa kutawala Tanzania milele!.
 
Back
Top Bottom