Ombamba maarufu, Matonya, afariki dunia

Friday, 24 August 2012 23:38

000000000001aamatonya.jpg
Mzee Paulo Mawezi maarufu kama Matonya akiwa na mwanae Elizabath wakiwa katika Kijiiji cha Mpamantwa Tarafa ya Bahi Mkoani Dodoma. Picha hii ilipigwa 2010 wakati alipokwenda kwa mapumziko ya sikukuu ya Krismas. Picha na Maktaba

Habel Chidawali, Bahi
LICHA ya umaarufu mkubwa aliokuwa nao na kufahamika katika miji mingi nchini, ombaomba Paul Mawezi maarufu kwa jina la Mzee Matonya, amefariki dunia na kuzikwa katika mazingira ya ufukara mkubwa.Matonya alizikwa jana kijijini kwake Mpamantwa, Wilaya ya Bahi, Dodoma akiwa amevishwa nguo moja nyeusi, huku mwili wake ukibebwa na watu wasiozidi 20, waliotumia ngozi kuu kuu ya ng’ombe.
Matonya aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kikohozi tangu Mei mwaka huu, alifariki dunia juzi usiku na kuzikwa jana saa saba mchana mita tatu kutoka katika nyumba yake ya tembe alimokuwa akiishi.
Ndugu na jamaa zake wa karibu walisema Matonya ambaye umri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 90, hakuwahi kwenda kutibiwa hospitali kutokana na ukosefu wa fedha.
Mwandishi wetu alishuhudia idadi ndogo ya waombolezaji nyumbani kwa Matonya, huku watoto wake watatu waliokuwapo msibani hapo kati ya watano aliowaacha hai, wakisema kuwa baba yao amefariki kutokana na umaskini na ufukara.
“Hatukuweza kumpeleka hata hospitali kupata vipimo kwani hatukuwa na uwezo wa kwenda mjini Dodoma kutokana na kukosa hata nauli, ndiyo maana tumekuwa kimya hadi Mungu alipomchukua,’’ alisema mmoja wa watoto hao, David Paulo.
Umaarufu wa Matonya
Umaarufu wa Matonya ulitokana na staili yake ya kuomba kwa kulala chali barabarani, huku akiwa ameinua kopo juu bila ya kujali jua au mvua.
Kwa nyakati tofauti alipinga mpango wa Serikali wa kumrejesha kwao Bahi na mara kadhaa alimweleza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusufu Makamba kuwa yeye ni mtoto wa mjini hivyo asingemuweza. Aliingia Dar es Salaam kwa mara ya kwanza Desemba 7, 1961.
Katika siku za karibuni, alikuwa gumzo kwa Serikali na viongozi huku akipachikwa jina la Komandoo na Kiboko ya Makamba.
Baada ya kuondolewa Dar es Salaam, aliweka makazi yake mapya ya kuomba mkoani Morogoro hususan eneo la Darajani, ambako aliendeleza staili ya kuomba akiwa amelala chali na kuinua kopo juu kwa muda mrefu bila kuchoka.
Iliwahi kuvuma kwamba ombaomba huyo alikuwa na utajiri mkubwa, jambo ambalo mtoto wake mkubwa, Elizabeth Paulo alilipinga na kusema kwamba halina ukweli na hakuacha chochote.
Mke wa Marehemu Paulina alisema walitengana na Matonya zaidi ya miaka 37 iliyopita na wakati huo alikuwa na mali nyingi (ng’ombe).
“Tulipotengana tu, mimi nilirudi kwetu na watoto wangu walikuwa bado wadogo na bahati mbaya mdogo wake aliyekuwa akitunza ng’ombe (wa Matonya) alifariki dunia na huo ukawa ndiyo mwanzo wa kumaliza mifugo yote kwani watu waliwaiba wote,’’ alisema Paulina.
Matonya alirudi kijijini kwake Mpamantwa kwa ajili ya mapumziko ya Krismasi Novemba, 2010 akitokea Morogoro kama ilivyokuwa kawaida yake na tangu wakati huo hakurudi tena.

Makamba, Mashishanga wamlilia
Akizungumzia msiba huo, Makamba ambaye alifanikisha mpango wa kumwondoa Matonya Dar es Salaam, alisema amesikitishwa na kifo hicho cha mtu aliyemtaja kuwa alikuwa rafiki yake mkubwa.
“Nasikitika nimempoteza rafiki mkubwa… Mimi nilimpenda lakini inaonekana Mungu amempenda zaidi,” alisema Makamba jana kwa simu.
Alisema urafiki wao ulianzia pale alipomwondoa Dar es Salaam na kumrejesha nyumbani kwao Dodoma, lakini baadaye akahamia Morogoro... “Alipokwenda Morogoro (Matonya) alisema ‘naipenda CCM, lakini simpendi Makamba.’ Waandishi waliponifuata wakaniuliza nikasema mimi nampenda,” alisema Makamba.
Alisema kauli yake ya kumpenda inathibitishwa na mkakati wake wa kutaka kumwondoa katika mazingira ya dhiki na jua kali wakati wa kuombaomba katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kumpeleka kwao Dodoma, ambako angeweza kutulia na kuishi vizuri na ndugu zake.
“Alikwenda huko, lakini kwa bahati mbaya kama Waswahili wasemavyo, mazoea yana tabu, akarejea kwenye kazi yake mkoani Morogoro,” alisema Makamba.
Makamba ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM kabla ya kustaafu, alisema Matonya alikuwa mmoja wa makada wanaokipenda chama hicho tawala, hivyo licha ya kusikitika kupotelewa na rafiki, pia anasikitishwa na chama kumpoteza mmoja wa wakereketwa wake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro mstaafu, Stephen Mashishanga alisema, Matonya alikuwa mzee maarufu na hakuwa mtu aliyependa makuu kwani kila alipotakiwa kuondoka mjini alitii.
Alisema kifo chake kimemsikitisha kama binadamu mwenzake hasa akikumbuka kuwa hakuwahi kumnyanyasa, akisema alikuwa ombaomba aliyependa kukaa eneo moja na kila aliyemwonea huruma alitoa sadaka yake.
“Alipotakiwa kuondoka, aliondoka lakini baadaye alirudi mahali ambako kuna masilahi; Hata ng’ombe hukimbilia mahali ambako anajua kuna nyasi za kutosha,” alisema Mashishanga.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
 
Serikali itunge sera ya dhati kwa makundi maalum,wazee,yatima,magongwa sugu/critical isiwe hisani ya chombo cha habari ama mtu.Bali jukumu rasmi la wa tz wote via serikali.Rest in peace mzee Matonya.
 
Matöya umetutoka kimwili kiroho tuko nawe . Tutakukumbuka milele kwa makeke yako R.I.P MZEE MATONYA
 
mkubwa ubarikiwe, lakini Mungu aliyesema kila nafsi itaoonja mauti, siyo sawa na MUNGU aliyesema watu kutokuonja mauti. They are two GODS, in which one stand for ever

He said i thirst yet he made the rivers, He said i thirst yet he made the seas. I thirst.....! said the KING of the Ages, in his great thirst he brought life to human kind.
 
Ni rahisi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuuona ufalme wa mbinguni Huyu alikuwa omba omba low class... Bado si kama yule wa V.I.P
 
Back
Top Bottom