Ole wao wanaotishia kwa sms- DCI Manumba

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
Ole wao wanaotishia kwa sms- DCI Manumba

Mwandishi Wetu Oktoba 1, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni vitendo

MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba amesema ya kuwa tabia inayojitokeza katika jamii kutumia simu za mkononi kutuma ujumbe wa vitisho, unyanyasaji au mambo ya ngono ni uhalifu na Jeshi la Polisi limejizatiti kukabiliana nayo.

Akizungumza na mtandao wa habari wa klhnews.com wa Marekani, Jumapili, uliokaririwa nchini, Manumba alisema ya kuwa kumekuwapo ongezeko la malalamiko kutokana na baadhi ya watu kupata ujumbe wa mfupi wa simu (sms) wa vitisho kutoka kwa maadui zao au hata watu wasiowajua na kwamba vitisho hivyo vingi vinahusu “masuala ya binafsi na ugomvi wa kawaida”.

Kuhusu suala la vitisho kwa viongozi kama ilivyolalamikiwa na Spika Samuel Sitta, Manumba alisema: “Vitisho kwa viongozi ni nadra sana, mara nyingi vinawalenga watu wa kawaida, lakini vyote tunavipa uzito mkubwa”.

Alisema kuwa “kitisho ni kitisho iwe kwa kiongozi au mtu wa kawaida na kwa ajili hiyo vyote tunachunguza”.

Akijibu swali kama Jeshi la Polisi lina vifaa na uwezo wa kisheria kufuatilia wale wanaotumia simu za mkononi kutoa vitisho kwa watu wa kawaida na viongozi, alisema kuwa hadi sasa suala hilo linashughulikiwa katika pande mbili; upande mmoja ni suala la vifaa vya kisasa vya kuwezesha Jeshi la Polisi kuweza kukusanya na kufuatilia vitisho hivyo na hilo liko katika mipango ya maendeleo ya jeshi hilo.

“Suala la pili ni suala la kisheria kwamba namna gani tutaweza kuziangalia hizo taarifa (sms) na jinsi gani zinakubalika kisheria bila kuingilia mambo binafsi ya watu au mambo ya usalama wao,” alisdema.

Aliuambia mtandao huo maarufu wa Watanzania wanaoishi nje ya kuwa Serikali iko katika mazungumzo na makampuni yanayotoa huduma za simu za mkononi katika kuleta ushirikiano wa kufuatilia usalama wa matumizi ya simu hizi na kuwalinda watumiaji na suala la usalama wa Taifa.

Kwa mujibu wa Manumba “sababu ya kuwa na ushirikiano huo ni kuwa suala hili haliwadhuru watumiaji wa simu tu bali pia wenye makampuni hayo kama wafanyabiashara kwani linaweza kuwaharibia biashara zao”.

Kuhusu matumizi hayo ya simu yanavyoweza kuhatarisha usalama wa Taifa, Manumba alisema kuwa mara nyingi Watanzania ni wepesi kutoa simu zao zitumiwe na mtu wasiyemjua kwa ukaribu au aliyezoeana naye kwa muda mfupi bila kujua mtu huyo anatumia simu hiyo kwa malengo gani.

“Tuwe waangalifu, unajua sisi bado ni wageni sana katika teknolojia hii na watu hawajui kuwa simu zao zinaweza kutumiwa na wahalifu na wao (wamiliki) kuhusishwa na uhalifu wasiohusika nao” alisisitiza.

Kuhusu suala la viongozi na watu maarufu kupewa vitisho kwa njia ya sms au mitandao ya kiintaneti Manumba aliwataka wasipuuzie, “ watambue kuwa huu ni uhalifu; kutishiwa ni uhalifu au matumizi ya teknolojia hii kwa malengo mabaya yote ni uhalifu”.

Aliwahakikishia wananchi kuwa “ Polisi tunaweza kupambana na wahalifu hao” akiongeza kwa kutoa wito kwa wananchi kushiriki katika kupambana na uhalifu kwani kazi hiyo si ya Polisi tu.

“Wananchi wasiwe na hofu, tunashirikiana na taasisi nyingine duniani zenye uzoefu katika teknolojia hii, tunaomba watupe ushirikiano wote ili tuweze kupambana na uhalifu huu. Tusiuache uote mizizi kwenye jamii yetu”.
 
Back
Top Bottom