Ofisi za wabunge zaichaganya serikali

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,173
Ofisi za wabunge zaichaganya serikali
Saturday, 04 December 2010 22:43

Fredy Azzah na Eveline Kijumbe
SUALA la wabunge wa CCM walioangushwa katika uchaguzi mkuu uliopita kuondoa samani na vifaa vingine walivyokuwa wakivitumia katika ofisi za wabunge, limeivuruga serikali ambayo imekiri kuwa inatoa fedha kununulia samani. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema ofisi yake ndiyo inayohusika na kutoa fedha kwa ajili ya kufanya marekebisho katika ofisi za wabunge na kuwa fedha hizo hupitishwa kwa Afisa Tawala wa Mikoa (Ras) wa mikoa.
“Mngewauliza Ma-Ras au Ma-Das kuwa wamenunua vifaa gani kwa ajili ya ofisi ya mbunge kupitia fedha hizo, fedha za ukarabati wa ofisi hizo hupitia kwao, na mimi najua bidhaa ya serikali hata kama imechakaa huwezi kuiondoa kuna utaratibu wa kuziondoa na mpaka zihakikiwe,” alisema Lukuvi. Hata hivyo, alisema baadhi ya wabunge hununua vifaa mbalimbali ambavyo wanadhani vinaendana na hadhi yao na kuviweka katika ofisi zao hizo.
“Lakini kama ni mali ya serikali imechukuliwa na mbunge, basi huo ni uzembe wa Ras kwa sababu anajua nini serikali imenunua katika ofisi husika,” alisema. Katibu wa Bunge Dk David Kashilila, aliiambia mwananchi Jumapili kuwa yeye hawezi kuzungumzia suala hilo kutokana na kile alichosema kuwa ofisi yake haishughuliki na masuala ya ofisi hizo.
Naye pia Naibu Spika wa Bunge Jobu Ndugai, alililiambia gazeti hili kuwa ofisi yake haihusiki moja kwa moja kutoa fedha za samani kwa ajili ya ofisi za wabunge. Hata hivyo aliwataka wabunge wapya kufanya mawasilino na Ma-Ras ili wawape maelezo zaidi kwani wao ndio wanaohusika na ununuzi wa samani za ofisi hizo ambazo nyingi zimo ndani ya ofisi za Wakuu wa Wilaya na Mikoa. “Inawezekana kabisa kuwa wabunge wapya wananunua baadhi ya vifaa kwa fedha zao, lakini mimi nawashauri wabunge wajaribu kuwasiliana na Ras ili awape ufafanuzi zaidi,” alisema Ndugai. Hata hivyo, maafisa hao wanaotuopiwa mzigo huo, nao pia wanaonekana kutokuwa na majibu ya suala hilo baada ya katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Gidion Mwinami kusema ofisi yake haijawahi kufanya tathmini kujua ndani ya ofisi ya mbunge wa jimbo la Iringa Mjini kulikuwa na nini ndani yake.
“Sifahamu kulikuwa na nini na sisi hapa hatujaletewa oda kwamba ofisi ya mbunge inahitaji kuwa na nini. Kama kweli vifaa vilivyokuwepo alinunu mbunge aliyepita, ni haki yake,” alisema. Alisema kuwa anachofahamu yeye ni kwamba ofisi hiyo ya mbunge inapaswa kuhudumiwa na serikali na kwamba meza moja sambamba na makochi ndivyo vilivyokuwepo, lakini hajui kama kulikuwa na kitu kingine zaidi ya hivyo.
“Kulalamika ni hulka ya mtu, nyie mmefika na kuona kuwa hapo kuna upungufu wa kitu gani; kama pazia pisi ngapi hazipo? Sisi hatujafanya tathmini kubaini hili ila tutafanya hivo,” alisema Katibu Tawala mkoa wa Mwanza (RAS) Doroth Mwanyika hakuweza kupatikana kuzungumzia jambo hilo, lakini afisa mmoja wa ofisi ya Ras alithibitisha kuwepo kwa malalamiko ya Wenje na kudai kuwa yalikuwa yakishughulikiwa. Kwa upande wa vyama, Mwanasheria wa Chadema, Tindu Lisu, alilieleza gazeti hili kuwa bado hawajapata taarifa rasmi kutoka kwa wabunge wao na kuwa watakapozipata wataihoji serikali sababu ya wabunge wao kufanyiwa kitendo hivyo. “Nafikiri ni vizuri kwanza nikapa taarifa rasmi, mpaka sasa bado hatujapokea taarifa rasmi juu ya haya lakini tukipata, itabidi tuiulize serikali kwani wabunge wetu wanafanyiwa hivyo,” alisema Lisu.
Katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya vitendo hivyo vinavyofanywa na waliokuwa wabunge wa chama tawala, alimtaka mwandishi kumuuliza waziri mkuu ili atoe ufafanuzi huo. Makamba alisema, ingawa wabunge wanaofanya vitendo hivyo ni wa CCM, yeye hawezi kuzungumzia chochote juu ya vitendo vyao hivyo kwakuwa ofisi za wabunge siyo za chama hicho. “Muulize Waziri Mkuu, ofisi ya mbunge siyo ya CCM, nizaserikali na ndio wanaopaswa kuweka samani, siyo chama ingawa kweli wabunge wanaofanya hivyo niwa-CCM,” alisema Makamba kabla ya kukata simu. Sakata ya wabunge walioangushwa katika uchaguzi, kuondoka na vifaa vya ofisi za wabunge, lilianzishwa na aliyekuwa Waziri wa mambo ya ndani Lawrence Masha, aliyehamisha vifaa mbalimbali vya ofisi ya bunge katika jimbo la Nyamagana, kwa madai kuwa alivinunua mwenyewe katika kipindi chake cha ubunge.

Mbunge wa sasa wa jimbo, Ezekieli Wenje alisema baada ya kutoka bungeni alikwenda kuingia katika ofisi hiyo lakini baada ya kukabidhiwa hakukuta vitu hivyo. Kwa mujibu wa Mbunge huyo baada ya kufuatilia aliambiwa kuwa vifaa hivyo viliondolewa na Masha kwa madai kwamba alivinunua kwa fedha zake mwenyewe. Siku chache baadaye, Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi, naye alikabidhiwa ofisi ambayo haikuwa na samani ndani yake. Ofisi hiyo ilibainika kukosa samani zinazotakiwa baada ya mbunge huyo kwenda kwa Mkurugenzi wa Jiji, Juma Rashid Idd, kwa lengo la kukabidhiwa rasmi ili aanze kazi. Kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku (siyo Mwananchi) Makabidhiano hayo ya ofisi kati ya Mkurugenzi wa Jiji Idd na mbunge huyo, yalikwama kutokana na ofisi hiyo kutokuwa na samani na uchafu uliokuwa umezaa katika ofisi hiyo.
Pia Iringa Mjini mbunge wa Chadema, Peter Msigwa alidai kuikuta ofisi ikiwa imeondolewa kila kitu, ikiwa ni pamoja na mapazia. Msigwa alidai kuwa vitu hivyo vimeondolewa na mbunge aliyemaliza muda wake, Monica Mbega ambaye alianguka kwenye uchaguzi mkuu uliopita baada ya kuliongoza jimbo hilo kwa miaka kumi. Msigwa alidai aliikuta ofisi hiyo ikiwa katika hali ya uchafu huku ikiwa haina mapazia, kompyuta, simu, nyaraka wala faili za kuhifadhia taarifa muhimu ingawa ilikuwa ikitumika katika kipindi kilichopita.
 
Back
Top Bottom