OCS mbaroni kwa ujangili

Ochu

JF-Expert Member
May 13, 2008
975
47
OCS mbaroni kwa ujangili


na Charles Ndagulla, Arusha




MKUU wa Kituo cha Polisi (OCS) cha Loksale kilichopo Wilaya ya Monduli, mkoani hapa, Koplo Amani, amefikishwa katika mahakama ya kijeshi akikabiliwa na tuhuma za kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwa kujihusisha na matukio ya ujangili.

Koplo Amani alikamatwa mwanzoni mwa mwezi huu na askari wa kikosi cha kuzuia ujangili kilichopo chini ya Idara la Wanyamapoli ya Wizara ya Maliasili na Utalii akiwa na nyara za serikali.

Habari za uchunguzi zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha, zinaeleza kuwa, Koplo Amani amekuwa akijihusisha na ujangili kwa muda mrefu kwa kuua wanyama na kuuza nyama yake kwa wafanyabiashara wa mjini Arusha.

Mwingine aliyekamatwa na askari huyo, ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Loksale aliyetajwa kwa jina moja la Amiru ambaye siku ya tukio gari lake aina ya Land Rover linadaiwa kubeba nyara hizo.

Nyara za serikali wanazodaiwa kukamatwa nazo watuhumiwa hao ni twiga watatu ambao tayari walikuwa wameshachunwa ngozi huku bunduki mbili aina ya Sub Machine Gun (SMG) mali ya Jeshi la Polisi zikidaiwa kutumika kuwaua twiga hao.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Basilio Matei, alithibitisha kukamatwa kwa ofisa huyo wa Jeshi la Polisi, lakini alikataa kulizungumzia kwa undani tukio hilo na kumtaka mwandishi wa habari hizi awalisiane na askari wa Idara ya Wanyamapori.

Akizumgumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki kwa njia ya simu, Kamanda Matei alithibitisha ni kweli mkuu huyo wa Kituo cha Polisi anashitakiwa kwenye mahakama ya kijeshi na akibainika kuhusika na tukio hilo atafukuzwa kazi.

“Ni kweli amekamatwa akiwa na nyama ya twiga, lakini wanaomshitaki ni askari wa wanyamapori, hao ndio waliomkamata, sisi tunamshitaki kwenye mahakama ya kijeshi na mashitaka yake yameshaanza na akibainika ametenda kosa, tutamfukuza kazi,” alisema.

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Loksale aliyezungumza kwa sharti la kutotaka jina lake kutajwa gazetini, alidai kukamatwa kwa OCS huyo kunatokana na taarifa za siri zilizopelekwa kwa askari wa wanyamapori na raia wema.

Alidai baada ya taarifa hizo kuwafikia askari hao, mtego uliandaliwa na siku hiyo watuhumiwa hao walinaswa wakiwa wamewaua twiga hao.

Katika tukio lisilokuwa la kawaida, baada ya mkuu huyo wa kituo cha polisi kufikishwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa, askari wa kawaida wanadaiwa kumpa kipigo.
 
Back
Top Bottom