Nini maana ya hivi vifungu vya sheria?

isasuna

Member
Jan 21, 2012
51
19
Salaaamu,

Kuna vifungu vya sheria vinavyohusu Wajibu wa kila raia katika suala la Ulinzi na Usalama wa Taifa ambavyo huwa vinatutatiza wengi tu na mimi nikiwemo. Labda kwa leo niviweke hapa ili wanasheria na wasomi wengine watusaidie.


Katiba ya sasa yaani hii ya mwaka 1977 sura ya kwanza sehemu ya tatu(Haki na wajibu muhimu) ibara ya 27(1) inasema “Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine”.

Pia ibara ya 28(1) na (2) zinasema “Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa taifa. (2) Bunge laweza kutunga sheria zinazofaa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kutumikia katika majeshi na katika ulinzi wa taifa”

Lakini ukienda mbele kwenye sura ya tisa ibara ya 147 (1) na (2) inaelezea MAJESHI YA ULINZI inasema .-(1) “Ni marufuku kwa mtu yoyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa Serikali kuunda au kuweka Tanzania jeshi la aina yoyote” (2) Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza, kwa mujibu wa sheria, kuunda na kuweka Tanzania majeshi ya aina mbalimbali kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wa Tanzania”. Ikafafanua katika kifungu cha (4) kwa kusema "mwanajeshi" maana yake ni “ASKARI aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa” Mpaka hapo kwa mimi naona vitu viwili, cha kwanza ni kwamba raia ana wajibu katika ulinzi wa taifa na cha pili raia ambaye sio “mwanajeshi” hawezi kushiriki moja kwa moja kwenye ulinzi wa taifa.


Hapa ndio utata unaanza hasa pale watu binafsi walipofikiria kuanzisha kampuni za ulinzi, watu kuwa na “body guards”, makampuni kuwa na vitengo vya ulinzi, uchunguzi na hata hapa kati vyama vya siasa navyo vina vikosi vyao vya ulinzi ambazo hizi ni kazi za Majeshi ya Ulinzi.


Nikaangalia Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inajadiliwa sasa hivi na bunge maalumu. Sura ya 4 sehemu ya pili inayohusu wajibu wa raia kwa taifa ibara ya 49(1) (e) inasema kila raia ana wajibu wa “kuilinda Tanzania na kushiriki katika ulinzi wa Taifa”


Ibara ya 51(1) inasema “Kila raia anao wajibu wa kulinda maliasili ya Taifa, Mali ya mamlaka ya nchi, na mali yoyote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine”


Mbele zaidi rasimu hii katika sura ya 15 inayohusu ULINZI NA USALAMA WA JAMHURI YA MUUNGANO ibara ya 235(1) inasema “Jukumu la Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano ni la kila raia”


Ibara ya 235(1) (a)-(c) inazungumzia vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Taifa kuwa ni (a) Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (b) Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano (c) Idara ya Usalama wa Taifa.


Kwa mtu wa kawaida kama mimi ambaye sijui sheria lazima nichanganyikiwe na ndio maana kila mara utasikia ooh! wananchi hawatoi ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, mara kosa linafanyika hadharani au mtu ana habari ya uhalifu lakini unasikia “hiyo kazi ya Polisi”, “hiyo kazi ya PCCB”, “hiyo kazi ya Usalama wa Taifa”, hiyo kazi ya JWTZ, kazi ya fulani n;k.


Nikaendelea mbele kidogo nikakutana na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai(CPA, 1985 R.E.2002) katika kifungu cha 16(1) na (2) ambacho kinaeleza kuwa mtu yeyote anaweza kumkamata/kumzuia mtu anayefanya kosa la jinai mbele yake. Kosa hilo laweza kuwa dhidi ya binadamu au mali.


Sehemu yenyewe inasema hivi(“16.-(1) Any private person may arrest any person who in his presence commits any of the offences referred to in section 14.(2) A person found committing an offence involving injury to property may be arrested without a warrant by the owner of the property or his servants or a person authorised by the owner of the property” Pia kwenye sheria inayohusu mambo ya Police na Wasaidizi wa Police (THE POLICE FORCE AND AUXILIARY SERVICES ACT) inaelezea kazi za wasaidizi wa police yaani “AUXILIARY POLICE” ambao ni wale police ambao hawana mamlaka sawa na police mwenyewe ila wanasaidia katika shughuli za ulinzi wa kawaida na shughuli nyingine za kipolisi.


Hii sheria katika kifungu cha 127 inaelezea kazi za hawa watu ambao naweza kuwaita ni Polisi Jamii, kwamba “The Auxiliary Police Force shall assist the Force in Maintaining order and protecting property in special areas”


mwisho nakutana na mpango wa polisi hapa Tanzania wa Ulinzi shirikishi au Polisi Jamii(Community Policing). Hapa polisi wanataka kuwashirikisha wananchi katika ulinzi wao na mali zao na wameona mafanikio kwa sababu wananchi ndio wanawafahamu zaidi wahalifu kwa hiyo kwa kufanya hiyo Partnership zoezi linakuwa rahisi kuwabaini.

Mpaka hapo wataalamu mnaweza kufafanua ni vipi sheria inaruhu au kuzuia hii haki ya raia kushiriki katika ulinzi wa taifa lao. Pia ni namna gani pengine hii haki inaweza kutolewa bila kuathiri utendaji wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Taifa.


Nawasilisha……….
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom