Nimwite nani?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,460
39,927
Nimeivuta manati, kumlenga ndege huyu,
Nikasikia sauti, siyo yake mbayuwayu,
Kutoka tawi la mti, si mbuyu ni mkuyu
Ndege anataka jina, bila jina hatunguki
Nimwite nani?

Kwanza nipe hilo jina, ndege huyo katamka
Bila jina mimi huna, msituni nitaruka,
Niwe mlo wa mchana, jina langu ninataka
Ndege anataka jina bila jina hatunguki!
Nimwite nani?

Karuka karukaruka, mtini akiringia,
Huku anacheka cheka, mbawa akinipungia,
Manyoya yakitimka, manati nimeshikia
Ndege anataka jina bila jina hatunguki,
Nimwite nani?

Katunisha na kifua, na wimbo kaniimbia,
Hamu ikanichukua, jiwe nikaachilia,
Ndege akajichepua, mbali likapitilia,
Ndege anataka jina, bila jina hatunguki!
Nimwite nani?

Huamini wa kijiji, bila jina mimi siji,
Hata ukinipa mji, Wa Dar au Ujiji,
Na univishe na taji, unipe togwa na maji,
Ndege anataka jina, bila jina hatunguki!
Nimwite nani?

Njaa imenizidia, ndege namtamania,
Jina naliulizia, wawindaji saidia,
Mwingine atajilia, huyo akiniwahia,
Ndege anataka jina, bila jina hatunguki!
Nimwite nani?

Nawauliza malenga, mabingwa wa kutungia
Mnaotoka Karenga, Wa Pwani nawaitia,
Ndege bado namlenga, jibu nalisubiria,
Ndege anataka jina, bila jina hatunguki!
Nimwite nani?


Na: M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
 
Wa kijiji una mambo
Si leo toka kitambo
Kuzinyaka zako chambo
Ita jeshi si mgambo
...
 
Wakijiji salaam,malenga nakupatia
Nashika yangu kalamu,nipate kusimulia
Najivuta kwa nidhamu,majibu kukupatia
Majina kweli ni mengi,Tabia ni tofauti

Cherero shingo ya njano, La kwanza napendekeza
Kupenda kuso mfano,Ni jambo analoweza
Sauti yake miguno,Mawimbi yanoteleza
Majina kweli ni mengi, Tabia ni tofauti.

Teleka mkia sindano, wa pili nakupatia
Na kama ni mashindano, hakuna wakufikia
Tatizo ni majivuno, na kutopenda sikia
Majina kweli ni mengi, Tabia ni tofauti.

Kuchamsitu hakika,ye nyuma hakubakia
Kijivu ilopauka, mwenye rangi ya kuvutia
Mayai yasohesabika, Kodata yake failia
Majina kweli ni mengi, Tabia ni tofauti

Na huyu Kirukanjia, jinale la jieleza
Kamwe hawezi tulia, kaponyoka kateleza
Kuruka na kukimbia, ni sifa alizojaza
Majina kweli ni mengi, Tabia ni tofauti

Firigogo doa doa, wa mwisho nakupatia
Ni bingwa wa kusogoa, hana asichokijua
Ukimficha Kondoa, ya Arusha takwambia
Majina kweli ni mengi, Tabia ni tofauti
 
mpwa wakijiji, heshima natanguliza
mpwao nipo poa, japo kwa kubangaiza
vipi leo kulikoni, mbona unagugumiza?
mlenga bila malengo, huwezaje kutimiza?

manati umeshalenga, kigugumizi cha nini?
yaachie asiliani, maswali mengi ya nini?
kitoweo kibindoni, mengineyo magilini
mlenga bila malengo, huwezaje kutimiza?

Sijapata kusikia, ndege asiyelika
wanamtaja kunguru, japo sina uhakika
mtungue kwanza chini, ili upate hakika
mlenga bila malengo, huwezaje kutimiza?

hizo zangu nasaha, waweza zipuuzia
ninapotaka timiza, maswali napuuzia
shida niitimizapo, ndipo ninaulizia
mlenga bila malengo, huwezaje kutimiza?
 
Hili sasa ndilo dongo
Laja tena kwa usongo
Mwisho kunitoa chongo

Ndege nimuite nani?

Mpe jina la kikwere,ringo lake kuumbua
Usijaribu tetere,hilo weshalitambua
Usikuze lake were,aje akakusumbua
Mwite kwa haiba yake,kidomo,kidari,kinda

Usitumie manati,wala mawe ya mtoni
Na kujaribu ukuti,hilo litakuwa tani
Simpandishie goti,akaingia kunani
Mwite kwa mluzi tuli,na tabasamu la pwani
 
Mpe jina la kikwere,ringo lake kuumbua
Usijaribu tetere,hilo weshalitambua
Usikuze lake were,aje akakusumbua
Mwite kwa haiba yake,kidomo,kidari,kinda

Usitumie manati,wala mawe ya mtoni
Na kujaribu ukuti,hilo litakuwa tani
Simpandishie goti,akaingia kunani
Mwite kwa mluzi tuli,na tabasamu la pwani

Ndege ameninunia,
La Kikwere kachukia,
Kadai namtania
Kwa haiba kuitia!

Nipe jina linifae
Usinipe nikatae
Kama nguo nilivae
La mwingine nisivae!

Nipe langu peke yangu
Sifanani na wenzangu
Hata liwe la Kizungu
Lisiwe kanakasungu!
 
Malenga leo na jana, salamu zipokeeni
Ukumbini tangu jana, majina tuleteeni
Hatunguki pasi jina, wakijiji tumteteeni
Using'ang'ane na jina, tatizo huenda kifaa

Kama tatizo jina, Shorwe mpatieni
Shabaha yataka kina, manati mvutieni
Majina mengine sina, labda ya ‘umenyeni’
Using'ang'ane na jina, tatizo huenda kifaa
 
Mzee nasalimia, wa Kijijini hujambo?
La mgambo likilia, ninajua lina jambo!
Mbiu nimeisikia, sio leo ni kitambo
Unataka kumjua, huyu ndege mwenye mambo
Ndege huyu ni KASUKU!

Ndege huyu ni Kasuku, jina nimelibaini
Si Bata wala si Kuku, hawa ndege wa shambani
Wala si yule Chiriku, wa sauti ya kughani
Itafika ile siku, atanaswa mtegoni
Ndege huyu ni KASUKU!

Nashangaa wa Kijiji, humjui ndege huyu!
Kama unamhitaji, 'usizunguke mbuyu'
Kwenye mti huo haji, amedandia mkuyu
Nawe sipande Bajaji, panda mti wa mkuyu
Ndege huyu ni KASUKU!

Wa Kijiji msifika, sasa unayo safari
Nenda msitu na nyika, jina ukilikariri
Wewe unajua fika, Msafiri ni kafiri!
Ndege huyu ni KASUKU!

Nenda siku na mapema, Kasuku 'kiita jina
Atakuja akihema, unataka nini Bwana
Huyu ni ndege wa zama, alifugwa kiungwana
Pema usijapo pema, kipema si pema tena!
Ndege huyu ni KASUKU!

Katu sibebe manati, ndege atakupuuza
Mithili ya Goliati, Daudi alimbeza
Wala sipige magoti, ndege kumbembeleza
Taja jina kwa sauti, KASUKU twende kucheza
Ndege huyu ni KASUKU!

Beba la mchuma Tenga, ndege kumhifadhia
Asije akakuchenga, msituni kurejea
Tembea 'kiringaringa, nyumbani 'naporejea
Ukishukuru wahenga, kwa dua kukuombea
Ndege huyu ni KASUKU!

Nyumbani ukiwasili, Tenga ulitue pindi
Katengeneze kufuli, kwa wale stadi mafundi
Tenga ulifunge kweli, na ndege mpe mahindi
Funguo katupe mbali, mle bahari ya Hindi
Ndege huyu ni KASUKU!

Acha na kucheka cheka, na huyu ndege Kasuku
Kuiga yake silika, atacheka kila siku
Ndege anahangaika, huenda huko na huku
Umesha 'piga mweleka, Karata umempiku
Ndege huyu ni KASUKU!

Fumbo fumbia mjinga, mwerevu huling'amua
Waliyasema wahenga, wa zama za Mwinyimvua
Ndiyo mana najiunga, la mgambo kupigia
Mwakaribishwa malenga, ulingoni kuingia
Ndege huyu ni KASUKU!

Namuita Andanenga, 'Sauti ya Kiza' Rufiji
Tumepuliza kipenga, mimi na Mwanakijiji
Mpira kupiga chenga, baadaye tunywe uji
Katu hatutawatenga, wa vijiji na wa miji
Ndege huyu ni KASUKU!

Na malenga wa Mvita, Juma Bhalo wa zamani
Nakuita kwenye vita, uje hapa Barazani
Najua utajikita, mashairi kuyaghani
Kati ya Popo na Bata, utambue ndege nani
Ndege huyu ni KASUKU!

Beti nazikamilisha, beti hizi za kudumu
Jibu nimewasilisha, Mmeipata elimu
Anayetaka kubisha, anitumie salamu
Hakuna kisichoisha, iliyobaki karamu
Ndege huyu ni KASUKU!

Hapa sasa ninakoma, sitaki kuitwa Kenge!
Nataka kwenda kusoma, mimi si Kalumekenge
Salamu zao Musoma, na wenyeji wa Rulenge
Wa Dar na wa Kigoma, na wa Kusini Mahenge
Ndege huyu ni KASUKU!


Na: Mrimu wa Herakuli (Jitu la miraba minne)
 
Nimeamua kurudi,ndege wenu kanichosha
Ndege ana makusudi,anataka kujikosha
Kuuliza sina budi,ni kwa nini anabisha
Ndege huyu ndege gani, asietaka sikia

Majina mengi twatoa, ndege hataki sikia
Mengine tumetohoa, ili apate chukua
Sasa kama twamboa,aseme tupate jua
Ndege huyu ndege gani,asietaka sikia

Kwanza keshaniudhi, kwa pozize na maringo
Ameitwa tangu juzi,abaki tikisa shingo
Jikoni tui la nazi,na viazi vya viringo
Ndege huyu ndege gani, asietaka sikia

Ndege nimemgundua, Atakua hajakua
Kwa nini akuchekea, mbawaze akipungia?
Kuliwa hajafikia, minofu hajapatia
Ndege huyu ndege gani, asietaka sikia

Kwanza jina la nini, wakati enda kuliwa?
Jina la kazi gani,mezani kushambuliwa
Jina halafu nini, nyama kutumbuliwa
Ndege huyu ndege gani, asietaka sikia

Ndege wako kanchosha, hana analojua
Njoo kwetu Arusha, upate walotulia
Makazi utahamisha,ukionja nakwambia
Ndege huyu ndege gani, asietaka sikia
 
nimeivuta manati, kumlenga ndege huyu,
nikasikia sauti, siyo yake mbayuwayu,
kutoka tawi la mti, si mbuyu ni mkuyu
ndege anataka jina, bila jina hatunguki
nimwite nani?

Kwanza nipe hilo jina, ndege huyo katamka
bila jina mimi huna, msituni nitaruka,
niwe mlo wa mchana, jina langu ninataka
ndege anataka jina bila jina hatunguki!
Nimwite nani?

Karuka karukaruka, mtini akiringia,
huku anacheka cheka, mbawa akinipungia,
manyoya yakitimka, manati nimeshikia
ndege anataka jina bila jina hatunguki,
nimwite nani?

Katunisha na kifua, na wimbo kaniimbia,
hamu ikanichukua, jiwe nikaachilia,
ndege akajichepua, mbali likapitilia,
ndege anataka jina, bila jina hatunguki!
Nimwite nani?

Huamini wa kijiji, bila jina mimi siji,
hata ukinipa mji, wa dar au ujiji,
na univishe na taji, unipe togwa na maji,
ndege anataka jina, bila jina hatunguki!
Nimwite nani?

Njaa imenizidia, ndege namtamania,
jina naliulizia, wawindaji saidia,
mwingine atajilia, huyo akiniwahia,
ndege anataka jina, bila jina hatunguki!
Nimwite nani?

Nawauliza malenga, mabingwa wa kutungia
mnaotoka karenga, wa pwani nawaitia,
ndege bado namlenga, jibu nalisubiria,
ndege anataka jina, bila jina hatunguki!
Nimwite nani?


Na: M. M. Mwanakijiji (sauti ya kijiji)

njiwa jike!
 
Mzee nasalimia, wa Kijijini hujambo?
La mgambo likilia, ninajua lina jambo!
Mbiu nimeisikia, sio leo ni kitambo
Unataka kumjua, huyu ndege mwenye mambo
Ndege huyu ni KASUKU!

Ndege huyu ni Kasuku, jina nimelibaini
Si Bata wala si Kuku, hawa ndege wa shambani
Wala si yule Chiriku, wa sauti ya kughani
Itafika ile siku, atanaswa mtegoni
Ndege huyu ni KASUKU!

Nashangaa wa Kijiji, humjui ndege huyu!
Kama unamhitaji, 'usizunguke mbuyu'
Kwenye mti huo haji, amedandia mkuyu
Nawe sipande Bajaji, panda mti wa mkuyu
Ndege huyu ni KASUKU!

Wa Kijiji msifika, sasa unayo safari
Nenda msitu na nyika, jina ukilikariri
Wewe unajua fika, Msafiri ni kafiri!
Ndege huyu ni KASUKU!

Nenda siku na mapema, Kasuku 'kiita jina
Atakuja akihema, unataka nini Bwana
Huyu ni ndege wa zama, alifugwa kiungwana
Pema usijapo pema, kipema si pema tena!
Ndege huyu ni KASUKU!

Katu sibebe manati, ndege atakupuuza
Mithili ya Goliati, Daudi alimbeza
Wala sipige magoti, ndege kumbembeleza
Taja jina kwa sauti, KASUKU twende kucheza
Ndege huyu ni KASUKU!

Beba la mchuma Tenga, ndege kumhifadhia
Asije akakuchenga, msituni kurejea
Tembea 'kiringaringa, nyumbani 'naporejea
Ukishukuru wahenga, kwa dua kukuombea
Ndege huyu ni KASUKU!

Nyumbani ukiwasili, Tenga ulitue pindi
Katengeneze kufuli, kwa wale stadi mafundi
Tenga ulifunge kweli, na ndege mpe mahindi
Funguo katupe mbali, mle bahari ya Hindi
Ndege huyu ni KASUKU!

Acha na kucheka cheka, na huyu ndege Kasuku
Kuiga yake silika, atacheka kila siku
Ndege anahangaika, huenda huko na huku
Umesha 'piga mweleka, Karata umempiku
Ndege huyu ni KASUKU!

Fumbo fumbia mjinga, mwerevu huling'amua
Waliyasema wahenga, wa zama za Mwinyimvua
Ndiyo mana najiunga, la mgambo kupigia
Mwakaribishwa malenga, ulingoni kuingia
Ndege huyu ni KASUKU!

Namuita Andanenga, 'Sauti ya Kiza' Rufiji
Tumepuliza kipenga, mimi na Mwanakijiji
Mpira kupiga chenga, baadaye tunywe uji
Katu hatutawatenga, wa vijiji na wa miji
Ndege huyu ni KASUKU!

Na malenga wa Mvita, Juma Bhalo wa zamani
Nakuita kwenye vita, uje hapa Barazani
Najua utajikita, mashairi kuyaghani
Kati ya Popo na Bata, utambue ndege nani
Ndege huyu ni KASUKU!

Beti nazikamilisha, beti hizi za kudumu
Jibu nimewasilisha, Mmeipata elimu
Anayetaka kubisha, anitumie salamu
Hakuna kisichoisha, iliyobaki karamu
Ndege huyu ni KASUKU!

Hapa sasa ninakoma, sitaki kuitwa Kenge!
Nataka kwenda kusoma, mimi si Kalumekenge
Salamu zao Musoma, na wenyeji wa Rulenge
Wa Dar na wa Kigoma, na wa Kusini Mahenge
Ndege huyu ni KASUKU!


Na: Mrimu wa Herakuli (Jitu la miraba minne)


Swadakta..........!
 
MKJJ MKJJi
Kwakweli sitambui
Kufulia nimefulia kweli
Kwahili nawaachieni ninyi

Lekha nizeeeeeee
 
Ewe Kasuku sikia
Jina ninakupatia
Manati naachilia
Ombi ninakupatia
Uwe wangu!

Mtini umetulia
Wimbo ukiniiambia
Mtima nashikilia
Goti ninakupigia
Uwe wangu!

Na chozi nakulilia
Shauku yanishikia
Mikononi kukutia
Kasuku wangu sikia
Uwe wangu!

Kila nikifikiria
Na ninapokuwazia
Nashindwa kujizuia
Ewe tunu nakuambia
Uwe wangu!

Jina umeulizia
Nikikupa wanijia
Mtegoni naingia
Mbele zako naumia!
Uwe wangu!

Mbingu ningekupatia
Na dunia yote pia
Nisivyonavyo ubia
Navyo kukutafutia,
Uwe wangu!

Ahadi nakupatia
Malaika wasikia
Mahoka nawalilia
Jibulo nasubiria
Uwe wangu!

Mikono nafungulia
Tayari kukumbatia
Malenga nashukuria
Na wote mlochangia,
Uwe wangu!

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)

NB: Asante sana washairi, wasomaji, na wachangiaji wengine. Inshallah, Jumatatu tutakuja na kipande kingine cha kimtego mtego!
 
Splendid! you all guys are simply amazing!
MKJJ big up

Mashairi siyawezi, hilo nami nalijua
sio mengine siwezi, yako ya kujivunia
mmeniacha kichizi,hata kama ninania
hongereni watunzi, kwa kazi hii yakujivunia
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom