Nimekutana na article hii nzuri by Vitali Maembe

kazi ipo kaka angalia waheshimiwa wetu wacje wakaiona hii hotuba yako maana hawapendi wa2 wenye mtazamo na uelewa kama huu. Wacje wakakuinterijensia.
 
Nakumbuka nilipokuwa shule ya vidudu si chekechea, tulipofundishwa, mwalimu akiingia darasani monita anasema Heshma! Wote tunasimama na kusema,
“Ili tuendelee twahitaji vitu vinne, watu ardhi siasa safi na uongozi bora sisi vijana wa ccm tupo tayari kujenga taifa… shkaaaa mooo mwaalimu!”

Nimeipenda hii, ile ni shule ya vidudu si chekechea, Ndo maana siku hizi hata mabaa wanaita changamoto, eti ukimwita zeruzeru unapelekwa kwa pilato, hawajuwi hata albino ni Kiingereza tu Kiswahili chake ni kilekile!!!!!!!
 
Bwana Maembe yuko vizuri lakini bahati mbaya Sana kazi za watu kama hawa huwa hazipati airtime kwenye media simply middlemen hawazitaki.Halafu dizain kaua Sana kwa Mzee wa nikipata nauli.It's a nice article.
 
Kaka Maembe nimekusoma. Tumelala ili tutachemsha ili tupate maji moto tuwanyweshe wamezoe vya baridi. Moto tutawasha bila kumwambia Mjomba.
 
Nafikiri ndani yake kuna dongo la Mrisho Mpoto ambaye amejigaragaza kwa kushiriki uozo wa katiba ya CCM
 
Hotuba ya mfungwa Mswahili|Na Vitali Maembe, Berlin


Ndugu waheshimiwa na wote msioheshimiwa!


Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kuniweka hai na kunitia nguvu. Hii ni hotuba ya kwanza kabisa ya mfungwa Mswahili kwa watu wote, naiandika huku nikiomba Mungu iwafikie ikiwa hivi nilivyoiandika, lakini sijui kama itawafikia wakati bado mwili wangu umeambatana na roho yangu.


Ndugu zangu, jela inatuumiza! Mimi ni mfungwa, kuwa mfungwa haimaanishi kuwa ni mtu mwovu bali ni mtu aliyeonwa na sheria. Hapa nilipo ni mahala muhimu sana, ni mahala pa kujenga. Ingawa wengi hutoka wakiwa wamebomoka na kuharibika kabisa, wamepoteza afya ya roho, akili na mwili.


Jela inawaumiza wanetu, jela inawaumiza wazazi na wapenzi wetu ingawa hawapo kifungoni. Jela inaiumiza nchi yetu. Ndugu zangu kuna umri wa kufundishana adabu lakini kwa nafasi hii niliyoipata wacha niitumie kwa kazi hii ingawa umri wenu umeenda! Nafanya hivi makusudi kwa kujua kabisa kwani hata waswahili wamenionya kuwa samaki mkunje angali mbichi, akishakauka utamvunja bure upate lawama.


Ndugu waheshimiwa, jiheshimuni, waheshimuni na wengine ili muheshimike kihalali! Nanyi msioheshimiwa muwaheshimu wenzenu na mamlaka zilizowekwa, jiheshimuni pia ndipo mdai heshima. Naomba nieleweke nimesema kuwa nimesema kuheshimu, si kuogopa au kuabudu. Nitaongea kwa mipaka ingawa leo nimepewa uhuru wa kuongea. Waswahili wamenionya kuwa Uhuru usio na mipaka ni utumwa. Haki ya nani Sijaona lugha tajiri kama hii.

Ndugu zangu! Nilikuwa nasubiri kutolewa huku kwa msamaha wa rais nije kuongea nanyi ana kwa ana lakini bahati haijawa yangu labda mwakani. Jamaa zangu chonde nawaomba mseme na roho zenu, Mungu ajaalie tuonane nyumbani tukiwa hai wote, tujenge taifa lililo jema.


Maisha ya jela ni magumu na ya hatari, lakini kuna wakati tunapata nafuu, hasa pale wanapoletwa wakubwa huku ndani, mlo unabadilika na dawa za mbu zinapulizwa, uji sukari kibao na maji safi kama kawaida, lakini tatizo hawakai sana… hata hivyo msemo wa Kiswahili huwa hauachi kutimia “mgeni njoo mwenyeji apone”.

Nduguzangu! kama nitajaaliwa kutoka tutaonana nyumbani, ila sina matumaini sana maana wenye nguvu wameshaanza kunipiga kwa siri, kama roho yangu ikiachanishwa na mwili basi msisahau kuwaambia watoto wa leo kuwa Tanzania mpya ipo, Tanzania mpya bora ipo, ila wajikaze na waishike vizuri adabu yao.


Mheshimiwa mwongozaji!
Sikia sauti ya kilio cha Mswahili tangu kwenye sakafu ya moyo wake. Sikiliza bwana mkubwa, tutazame, nyuso zetu watanzania hazijui kudanganya, zinazungumza hali waziwazi tena kwa lugha nyepesi kabisa!


kuna kitu tumefanyiwa hapa! Sijui ni kwa ubaya au kwa wema lakini ukweli ni huu. Mmekamata vyombo vya habari, mmetukamata makoo, mnavipa ruhusa baadhi ya vyombo vya habari kuua maadili na utamaduni wetu! Mmeharibu mfumo wa elimu, halafu
Mnatutishia dini mnafikiri hatujui Mungu anataka nini?


Mnatutishia madaraka mnatufanya hatuijui siasa safi ikoje? Nakumbuka nilipokuwa shule ya vidudu si chekechea, tulipofundishwa, mwalimu akiingia darasani monita anasema Heshma! Wote tunasimama na kusema, “Ili tuendelee twahitaji vitu vinne, watu ardhi siasa safi na uongozi bora sisi vijana wa ccm tupo tayari kujenga taifa… shkaaaa mooo mwaalimu!” wakati huo ukisema nasema kweli tupu na chama kinilinde chama kinakulinda kweli. Kipindi hicho vtuo vya polisi haba mtuhumiwa akipatikana kwanza anafungiwa kwenye ofisi ya chama unasikia watu wanasema ‘kapelekwa zoni’


Ulaaniwe kujua, kujua si kwema, maana ningekuwa mjinga nisingepata shida akilini na moyoni kama hivi. Nimeishia darasa la nne tu nateseka hivi, je ninge…. Tofauti ipo! Tofauti kati ya utawala bora na uongozi bora… tofauti ipo. Tunatarajia elimu ndiyo ituokoe lakini elimu yenyewe mitaala hailingani na maisha ya kweli! Kila kitu mnakitia siasa, mnakifanya biashara.


Utajiri wa nchi yetu ndicho chanzo cha mateso kwetu. Hatufurahii maisha ndani ya nchi nzuri tuliyoachiwa na baba zetu. Hivi, ni lini mtatupa fursa ya kuishi maisha yetu? Ni lini tutafurahia uhuru wa nchi yetu? Tangu nchi inapata uhuru mpaka leo nchi inafikia nusu kalne, inahitaji uhuru mpya bado pua zetu hazijahisi hata kwa mbali harufu nzuri ya maendeleo. Mnatuonyesha kuwa njia rahisi ya mtu kuendelea ni kuwa mhalifu, sasa mnafikiri tutapungua huku jela?


Alafu nilitaka kusahau, niliona mambo yanaharibika nikaomba kusaidia mapambano dhidi ya rushwa nikaambiwa si kazi yangu, niliumia sana. Alafu na wewe muweka kanda, nani kakupa kibari cha kazi hiyo wakati hujui unachofanya? Mnaona hii nchi ya kishkaaji sio? Hujakatazwa kupiga muziki wa waswahili redioni lakini nikikuletea ooh nisamehe kaka… maneno ya nyimbo zako hayatawafurahisha waheshimiwa… huu si wakati wa kufurahishana huku nchi inaangamia, unaleta usomi wako wa kishamba bwana! Wamekuambia hawataki kusikia sauti ya kweli ya mswahili?

Acha kujipendekeza wewe! Unajua kazi ya muziki wewe? Au unafikiri kazi ya muziki ni kujaza ukumbi wa disko na kuvutia watu kwenye kampeni? Ukome kujipendekeza, kama hujui hata wao waheshimiwa wana haki ya kuburudika, kujifunza na kusikia sauti za ukweli. Usiwanyime haki yao ya kupata taarifa, elimu na burudani.


Viongozi wangu wapendwa!
Mliniziba mdomo Watanzania wenzangu wasinisikie kwakuwa siendani na matakwa yenu. Mkaweka uadui kati yangu na wenzangu.
Mkawapa nafasi wanamuziki wanafiki ili wawafichie uovu wenu, nyimbo za matusi zinaimbwa wazi wazi nanyi mnazichukulia poa tu.
Eti maendeleo, Chuo cha Sanaa Bagamoyo kinakufa mnajifanya hamuoni, Chuo Kikuu Dar es Salaam kinazalisha matakataka mnachekacheka tu! Subirini kidogo muone matokeo ya bomu mnalolitengeneza.


Mnaandaa mitaala ya elimu ya kuwajaza ujinga watu, mtu amehitimu lakini bado yuko uchi akilini. Heri mimi sikusoma kabisa. Ila najua kuhesabu hela. Wenye makucha makubwa wanatutesa, wanajificha nyuma ya siasa, biashara na dini, watushambulia wanyonge bila huruma.


Halafu na nyinyi waumini mimi ndio nimewatoa maana kabisa kwa unafiki wenu! Na kwenye nyumba zenu za ibada mnifukuze kabisa mkitaka! Mungu atanipokea na kuwaaibisha wanafiki wakubwa nyie… mtu anasimama kashika katiba na kitabu cha Mungu wenu, anaapa kwa jina la Mungu halafu anaenda kinyume cha kiapo chake kisha nyie mnamkenulia meno tu, mnajua maana ya kiapo nyie? Sawa katiba imepitwa na wakati, biblia na msaafu je? Mnashindwa kusimama kwa ajili ya jina la Mwenyezi Mungu mtasimama kwa ajili ya nani?


Nitasahau kusema yote lakini hili ntalisema kabla sijafa, Tanzania inataka katiba ya kitanzania, katiba ambayo si ya kikoloni, katiba ya zama hizi, ambayo hata tukiongozwa na bora kiongozi itamfanya aonekane ni kiongozi bora. Katiba itakayo tuongoza kwenye maendeleo ya kweli, kumheshimu Muumba aliyeamua kuusimamisha Mlima Kilimanjaro, akaiweka Ngorongoro na kutuzawadia bahari, akatupa Ziwa Tanganyika, Nyasa, Rukwa, akajaza utajiri ardhini. Katiba itayoruhusu tume huru ya uchaguzi na pia taasisi huru ya kuzuia rushwa.


Nendeni mtoni mkaoshe akili na roho zenu ubinafsi umewachafua.. nasema mimi mfungwa Mswahili, ashindikene! Mimi si yule msaliti anayesubiri nauli wakati aendapo ameshafika! Wala sina ujamaa naye, mie sitangazi ujomba ili nibebwe. Msinichanganye kwanza nna mwiko wa kuchanganika na watu wanaoupenda sana uhai wao kuliko kuishi kwao.


Tofauti ipo! Tofauti kati ya utawala bora na uongozi bora… tofauti ipo. Siogopi maumivu mliyoniandalia, mimi ni marehemu niliyerudishwa kwaajili ya mswahili aliaye shidani? Mtu hafi mara mbili bwana. Ndimi ashindikene bwana, kaulize Bagamoyo, mimi pilipili, mimi dawa chungu.


Nimetumwa naye mwenye uwezo wa kuumba na kuumbua anasema kwamba huu ndio wakati pekee ambao sauti na na kalamu zetu zinaweza kuiokoa nchi yetu kabla halijachwa jua la amani hii. Ndugu wanafiki wafanyabiashara wa muziki, maadui wa utamaduni wetu wabinafsi na waabudu pesa wote!


Msijisumbue kunitishia umasikini, mkafikiri mtanibadilisha, mimi vita yangu si ya utajiri na mali, sikuja na mizigo wala sihitaji mizigo katika kuondoka kwangu, nilikuja uchi kutoka tumboni mwa mamaangu nitarudi uchi katika tumbo la nchi. Heshima ya nchi hii ya babaangu itarudi, kwa vyovyote na kwa gharama yoyote, kikiharibika kitu babaangu atarekebisha, na sita kufa tena niwaache wanangu na njaa. Mimi si masikini na kila mtanzania aliyezaliwa baada yangu si mtoto wa masikini.

Na njaa itamheshimu.
Tofauti ipo! Tofauti kati ya utawala bora na uongozi bora… tofauti ipo. Na wote mliotuibia imekuwa vema hatukufundishwa kushika silaha, na Muumba atunusuru na hilo, lakini ole wao watoto na wajukuu zenu, sijui wataoga wapi hata shombo na vumba la uozo wenu liishe, maana wanakuja watoto wetu hodari, wala nyuki, nyoka waumao usiku.


Mungu wangu, ulisha ibariki Tanzania Mungu ulishaibariki Afrika Mungu usituondelee Baraka hii. Sina haki sana ya kupewa kila nitakachoomba lakini kwa neema zako naamini utanijaalia kwa ajili ya Tanzania yako. Tofauti ipo! Tofauti kati ya baraka na laana… tofauti ipo. Watie aibu maadui wa mtumishi wako. Amlaaniye uliyembariki laana yake imrudie.


Vitali Maembe ni msanii wa muziki. Ni mtunzi pia wa nyimbo mbalimbali aliyenolewa katika Taasisi ya Sanaa Bagamoyo. Kwa sasa yuko ziarani katika nchi kadhaa barani Ulaya.

Ahsante sana Vitali, kwa hakika hotuba imetulia na imejaa ukweli mtupu.
 
nimeisomaa na imenipaa hisia sana....safi sana. vitali maembe
 
Last edited by a moderator:
dah vitalis jembe sana ,nimewahi kutana nae kwenye hafla fulani alitupa kipande cha hii hotuba yake
 
Mkuu kama una audio hiyo itupie humu..

Ile sauti iliyosoma hii hotuba ni Maembe mwenyewe si mpoki. Sauti zimefanana..


Mbona mm nina audio ya hotubu hii na imesomwa na Mpoki! Mpoki ndiye Vitali maembe? Au alimpa mpoki aisome? Plz naomba kujuzwa.
 
yupo smart sana msanii huyu, tofaut hawa diamond et wzee wa zamani wlinena kuchapiwa demu ni siri ya ndani. huyu kweli anamaono kweli
 
Hongera Maembe, hizi ndio sanaa tunazozihitaji ingawa naweka angalizo Mrisho Mpoto alianza hivyo na sasa kageuka maudhi kwa jamii inayojitambua. Keep it up ndugu.
 
Hii naifananisha na video ya Masoud Kipanya niliyoitambua kwa jina la vipande 24 vya keki!! Ndivyo wasanii wanavyotakiwa kuwa, kuamsha hisia za ndani za kizalendo.
 
Back
Top Bottom