Nikutonye... wapinzani wanajua fedha haramu zaidi kuliko serikali soma hotuba yao

Yericko Nyerere

JF-Expert Member
Dec 22, 2010
16,987
20,271
HOTUBA YA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA UDHIBITI WA FEDHA HARAMU WA MWAKA 2012,(THE ANTI-MONEY LAUNDERING (AMENDMENT) ACT, 2012 IKIWASILISHWA NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KATIKA WIZARA YA FEDHA, MHE.KABWE ZUBERI ZITTO (MB).

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni; Mhe. Kabwe Zuberi Zitto (Mb), na kwa mujibu wa kanuni za Bunge kanuni ya 86(6), toleo la mwaka 2007, naomba kuwasilisha maoni ya kambi ya Upinzani kuhusu Muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya udhibiti wa fedha haramu wa mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, fedha haramu ni biashara ambayo hufanyika bila kuwepo kwa mteja wa kuinunua biashara hii kwani mteja na mpokea mapato huwa ni mtu mmoja, kwa mujibu wa wataalamu wa kushughulikia uhalifu huu wanasema kuwa , huwa inapitia katika hatua tano muhimu kabla ya kukamilika katika mzunguko wake, hatua hizo ni;

1. Tendo la kihalifu , hii ni kujipatia fedha kwa njia ambazo sio halali kama vile kufanya biashara haramu kama za madawa ya kulevya,ufisadi, rushwa n.k

2. Fedha haramu kuingizwa kwenye mzunguko kupitia taasisi mbalimbali za fedha, hii ni mbinu ambayo hutumika katika kuhalalisha fedha hizo , kwa mfano mtu kufungua kampuni ambayo inajihusisha na biasahara mbalimbali tofauti hivyo kuweza kufungua akaunti benki kulingana na majina ya biashara husika na kwenye mabenki mbalimbali na hivyo hutumia akaunti hizo kuingiza fedha haramu kwa lengo la kuzisafisha.

3. Fedha haramu husafishwa ili kuficha hatua ya kupatikana kwa fedha hizo kihalifu,hii ni mbinu ambayo hutumiwa na wahalifu katika kuhakikisha kuwa hawawezi kufahamika na vyanzo vya fedha husika , kwa mfano mtu huamua kununua vitu mbalimbali kama magari, kusafirisha fedha nje kwa kutumia mifumo ya kibenki , kuanza kujipatia mikopo, tenda n.k

4. Fedha halali kuzaliwa, hapa ni hatua ya mtuhumiwa kuanza kupokea faida kutokana na vitega uchumi mbalimbali alivyojiwekea kutokana na fedha haramu na hivyo kuwa na uwezo wa kuonyesha vyanzo halali vya fedha zake .

5. Fedha hutumika kihalali kwa mujibu wa sheria, mzunguko huishia kwenye hatua ya matumizi kuwa halali na hakuna uwezo wa kuendelea kumfuatilia tena .

Mheshimiwa Spika , kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Maendeleo la Umoja wa mataifa (UNDP) ya mwaka 2011 mwezi mei , ilinaonyesha kuwa mataifa yanayooendelea yameathiriwa zaidi kiuchumi na biashara hii ya fedha haramu kwani iliongezeka kutoka dola za kimarekani 9.7 bilioni mwaka 1990 na kufikia kiashi cha dola 26.3 bilioni mwaka 2008 kwenye nchi zinazoendelea (LDCs), na madhara yake ni makubwa kwani ilichangia kushusha kiwango cha thamani ya fedha za nchi hizo kwa kiwango cha asilimia 6.2 kwa mwaka katika kipindi husika , hii inaonyesha kuwa Tanzania hatuko kisiwani kwani nasi tuliathiriwa kwa kiasi hicho hicho.

Mheshimiwa Spika, taifa letu limekuwa na sheria nyingi ambazo ziliwahi kutungwa kwa ajili ya kukabiliana/ kuondoa tatizo la fedha haramu,rushwa na uhalifu uliopangwa hapa nchini mwetu tangu tupate uhuru na hii inathibitishwa na uwepo wa sheria zaidi ya 15 kuwahi kutungwa tangu uhuru kama ifuatavyo;

the establishment of the Permanent Commission of Inquiry, or Ombudsman, 1966;

the Foreign Exchange Control Act 1966;

the Anti-Corruption Act 1971;

the establishment of an anti-corruption squad in 1975;

the Economic Sabotage Act 1983;

the Economic and Organised Crime Act 1984;

the Proceeds of Crime Act 1991;

the Leadership Code (Declaration of Assets) Act 1995;

the appointment of the Presidential Commission of Inquiry into Corruption, 1996;

the BOT Circular to Banking and Non-banking Financial Institutions, No. 8 of 2000, on Money Laundering.

the Drugs and Illicit Traffic of Drugs Act 1995;

the Arms and Ammunition Act 1991;

the Mutual Assistance in Criminal Matters Act 1991; and

the Tanzania Intelligence and Security Act 1998.

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kuwa pamoja na uwepo wa sheria zote hizi lakini bado kulikuwa na mianya ya biashara haramu ambazo zimekuwa zikifanyika kupitia maeneo mbalimbali .Kwa mfano mnamo mwaka 2001 jarida maarufu la Marekani la Wall street Journey liliandika kuwa mtandao wa Al-qaeda ulikuwa unanunua Tanzanite kutoka Tanzania na kuitumia kibiashara katika kusafishia fedha zao haramu zilizokuwa zinapatikana kutokana na ugaidi.

Hoja hii ilitiwa chumvi zaidi na takwimu za mwaka 1999-2000 kuwa mauzo ya Tanzanite ya Tanzania nchini Marekani yalikuwa yamefikia kiasi cha dola 328 milioni, wakati takwimu ambazo zilikuwa Tanzania zikionyesha kuwa tuliuza tanzanite nchini marekani zenye thamani ya dola 31 milioni tuu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kukosekana kwa mamlaka ya uthibiti wa majengo yaani Estate Regulatory Authority (ERA) kama ambavyo tuliwahi kusema kwenye hatuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni na kurejewa na ile wa waziri kivuli wa nyumba na Maendeleo ya makazi kwa mwaka wa fedha 2011/2012 wakati wa bunge la bajeti ni dhahiri kuwa ongezeko la majengo mengi na kupanda kwa thamani ya ardhi kwa kiwangop cha kutisha katikati ya majiji yetu kwa kipindi cha miaka ya karibuni kinapaswa kufuatiliwa kikamilifu .

Mheshimiwa Spika, Hii ni kutokana na uzoefu wa nchi mbalimbali kuwa katika ujenzi wa majengo mbalimbali huwa fedha hizi haramu huingizwa na kusafishwa ili kuwa kwenye mzunguko halali na wa kisheria na haswa ujenzi huo unapofanywa na watu ambao hawafahamiki wanafanya biashara gani ambayo inawawezesha wengine kujenga majengo marefu kwa kipindi kifupi lakini ya gharama kubwa sana .Hivi fedha wanazopata maharamia wa kisomali wanapoteka meli huwa wanawekeza wapi, kwani tunajua sote hali halisi ilivyo huko Somalia ya usalama mdogo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa sheria zote hizi lakini mnamo mwaka 2004/2005 taifa lilikumbwa na kashfa kubwa ya wizi wa fedha za umma ,yaani ndani ya kipindi cha miaka 2 ziliibiwa fedha kutoka kwenye Benki kuu zaidi ya shilingi bilioni 288 , ambazo ni kutoka akaunti ya EPA 133 Bilioni na Meremeta 155 Bilioni. Wizi huu ulifanikishwa kupitia taasisi zetu za fedha pamoja na uwepo wa sheria zote hizi.

Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2006 serikali ikaleta mswada Bungeni wa sheria ya kuzuia fedha haramu ili kuweza kutafuta ufumbuzi wa wizi huu na ili kuweza kuzuia usitokee tena ,sheria hiyo ilipitishwa na Bunge na tangu wakati huo haijawahi kutungiwa kanuni za utekelezaji na hii ni kusema kuwa haijatekelezwa kwa ukamilifu wake .

Kwa mfano sheria iliyopo kifungu cha 23 (1)kiliweka utaratibu wa fedha ambazo zinaingia na zinatoka nje ya nchi lakini la kustaajabisha tangu wakati huo kwa kipindi cha miaka 6 sasa mipaka ya nchi imekua ikiachiwa holela na fedha nyingi zinatoka bila hata kujulikana , kutokana na kukosekana kwa utekelezwaji wa kifungu hiki cha sheria. Kifungu hiki kilimpa waziri mwenye dhamana ya fedha mamlaka ya kuamua ni kiasi gani cha fedha kinaweza kusafirishwa nje ya nchi kikiwa kiasi tasilimu ambacho mtu anapaswa kuwa nazo .

Mheshimiwa Spika, maelezo yote hapo juu yanaonyesha wazi kuwa tatizo sio sheria bali ni utekelezwaji wa sheria husika na mamlaka zinazopaswa kusimamia utekelezwaji huo kuwa ndio chanzo cha kupotea kwa fedha hizo, kama ambavyo Bot waliweza kushiriki kwa kushirikiana na mabenki mbalimbali katika kuhakikisha kuwa fedha haramu zinapitia kwenye mzunguko wote ili kuwa halali na hatimaye kuingia kwenye mzunguko wa fedha .

Mheshimiwa Spika, kama kweli tumedhamiria kuzuia biashara ya fedha haramu ni muda mwafaka sheria zetu kuonekana hivyo, kwani sasa hivi hakuna katazo lolote kwa mtu kuondoka hapa nchini na fedha za kigeni kwa kadri anavyoona yeye inafaa. Utoroshaji wa fedha nyingi sana za kigeni umekuwa ndio jambo kubwa linalosababisha thamani ya shilingi yetu kushuka kila mara.

Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba mtu mmoja asiruhusiwe kuondoka na fedha taslim zenye thamani ya zaidi ya USD 10,000.

Hoja ni kwamba Je, ni kwanini marekebisho haya ya sheria hayajaweka kiwango Maalumu cha fedha mtu anatakiwa kuingiza au kutokanacho ndani ya nchi? Sambamba na hilo tunaitaka Serikali ilieleze Bunge ni utaratibu gani umewekwa wa kudhibiti mipaka yetu kwa wale wanaotorosha fedha nyingi za kigeni kwenda nje ya nchi.

Muswada wa kuthibiti matumizi ya fedha haramu .

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla maudhui ya muswada huu yako wazi, na hivyo Kambi ya Upinzani haina pingamizi na hilo. Jambo la kulizingatia ni kwamba uhalifu wa fedha haramu ni mtandao mkubwa sana ambao unahusisha watu wa kada mbalimbali kutoka katika taasisi mbalimbali. Hivyo tukumbuke kuwa kada hizo katika taasisi mbalimbali na wengine ndio hao hao wanaotakiwa wasimamie utekelezaji wa sheria hii lakini inakuwa ndio wahusika katika uharamia huo.

Mheshimiwa Spika, kuna tukio lililotolewa taarifa mkoani Mbeya la msamaria mwema kutoa taarifa kuhusiana na mashine ya kutengeneza fedha bandia na polisi waliukamata mtambo huo na mhusika kukamatwa lakini baada ya muda mtuhumiwa akaachiwa na hivyo kupelekea maisha ya mtoa taarifa kuwa hatarini. Kesi hiyo hadi Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi wana taarifa nayo. Hivyo basi, sheria inaweza kuwa ni nzuri lakini dhamira ya dhati ya wanaotekeleza hiyo sheria likawa ni tatizo kubwa sana; kwani imani kwa wananchi katika utekelezaji wa sheria ni jambo la muhimu sana wakishaamini kuwa wakubwa au vigogo sheria haiwahusu na inawahusu watu wa chini ni tatizo pia.

Mheshimiwa Spika, wananchi wanazo taarifa nyingi sana kuhusiana na wahusika wakubwa wa fedha haramu kwa ujumla wake, lakini wanaamini kuwa wakubwa au vigogo hawaguswi na sheria hiyo wakati wao ndio wahalifu wakubwa.Mfano mzuri ni wahusika wa madawa ya kulevya kama ambavyo Mhe. Rais alivyokiri kuwa majina yao alikuwa nayo, walarushwa n.k.

Mheshimiwa Spika, katika kuonyesha kuwa dhamira ya kweli ni jambo linaloleta imani kwa wananchi, bunge hili na Serikali vililikwishapatiwa taarifa rasmi kuhusiana na wizi wa kitaasisi unaoihusu kampuni ya Kagoda na jinsi fedha zilivyokuwa zikiingizwa kwenye benki ya CRDB lakini hadi sasa hakuna hatua yeyote iliyokwisha chukuliwa kwa wahusika wa wizi huo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa utangulizi huo, naomba sasa nipitie baadhi ya vifungu ambavyo tunaona bado kuna haja ya kuviweka vizuri au kuvitolea ufafanuzi wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, Kifungu kipya cha 4(3) kinaweka kitengo kipya cha kuzuia biashara ya fedha haramu na chenye uhuru na kutengewa bajeti yake ili kutenda kazi zake kwa uhuru zaidi. Kambi ya Upinzani inashauri kuwa kitengo hiki kiondolewe na kisiwe chini ya wizara ya fedha ili kiweze kuwa na uhuru wa kutosha kiutendaji na kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi tofauti na pendekezo la sasa kuweka kitengo hiki ambacho kinapewa mamlaka hata ya kuchunguza regulator wengine ambao wako chini ya wizara ya fedha au wanafanya kazi kwa maelekezo ya wizara. Kumuondoa mtendaji mkuu wa kitengo hiki ni mpaka rais aunde tume, sasa kwanini awekwe chini ya katibu mkuu wa wizara ?

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 5(6) pamoja na 5(7) kinachohusu jinsi ya kuondolewa kwa Mtendaji Mkuu wa Kitengo, kuwa Mhe Rais hatokuwa na madaraka ya kumwondoa ofisini Mtendaji Mkuu hadi Rais aunde kamati itakayochunguza tuhuma na kumshauri Rais. Kamati inayoundwa yote inahusisha wateule wa Rais au watu ambao wanaweza kuwa wanatarajia maslahi ya kikazi kwa kukubaliana na matakwa ya Rais kwani wote ni wajumbe ambao wanapendekezwa kuingia kwa nyadhifa zao na ni watendaji katika vitengo mbalimbali na ambao kiutendaji wanapaswa kutokuwa na masilahi ya moja kwa moja ili waweze kutenda haki bila ya kuwa mkinzano wa kimaslahi (conflict of interest).

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Kambi ya Upinzani inaona kuwa ingekuwa ni busara sheria ikatamka kuwa pale mtendaji huyo atakapokutwa na hatia ya kuondolewa kazini ni vyema hatua zaidi za kisheria zikatumika kwani ni dhahiri atakuwa amekiuka kanuni na mashrti yanayo muongoza katika utendaji kazi wake wa kila siku. Kwa njia hii tutaondokana na tabia iliyozoeleka ya watendaji wa serikali pale wanapoachishwa kazi kutokana na makosa mbalimbali hawafunguliwi mashtaka hata kama wameliingizia taifa hasara kubwa. Mifano ni mingi na ni dhahiri kwa kila mtu. Na pia wengine wakikutwa na makosa ya kiutendaji adhabu yao ni kuhamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine na tatizo hili limeota mizizi nchini mwetu .

Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani tunataka Sheria iweke utaratibu kuwa kama ikibainika ametenda makosa sheria ichukue mkondo wake kwani huyu ni mtu ambaye ni muhimu katika kusimamia uchumi wetu na kuondoa matumizi ya fedha haramu ambazo zimekuwa zikishiriki kudidimiza uchumi wetu kwa kushusha thamani ya fedha yetu.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 10 cha muswada kinachofanyia marekebisho kifungu cha 13 cha sheria kwa kuongeza kifungu kipya cha 10(2) kitakachowezesha kitengo cha FIU au Mamlaka ya Usimamizi kupeleka maombi mahakamani kwa lengo la kuiomba mahakama kuzifungia kwa muda au kuziweka chini ya uangalizi wa Mdhibiti taasisi au makampuni yaliyotiwa hatiani kwa makosa ya biashara ya fedha haramu. Kwa mujibu wa tafsiri mpya iliyotolewa katika muswada huu, “regulator” ni pamoja na Bank Kuu, hoja hapa ni kwamba kutokana na historia ya matukio ya nyuma “money laundering” imekuwa ikihusisha taasisi za fedha na taasisi hizo kwa kiasi kikubwa fedha zinazohusika zina mkono wa moja kwa moja na Bank Kuu. Sasa kama Bank kuu imekuwa inahusika ni kwa vipi itachukua jukumu la kuwa mwangalizi wa taasisi ambayo inatuhumiwa kuwa inafanya au imejihusisha na fedha haramu. Mfano Fedha za Meremeta zilitoka Bank Kuu na Akaunti ya Deep Green ikafunguliwa NBC siku ya mapumziko bila ya kufuata utaratibu. Je kwa hili Bank Kuu inapata wapi uhalali wa kuwa regulator?

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 28B kinapendekeza adhabu ya jumla kwa mtu kuwa faini ya juu ni shilingi milioni 500 na kiwango cha chini ni shilingi milioni 100 au kifungo kisichozidi miaka mitatu, wakati kwa kampuni au taasisi kiwango cha adhabu ni kuwa faini isiwe chini ya shilingi milioni 500 .

Mheshimiwa Spika, utaratibu huu wa kutoza faini ni dhahiri kuwa haukufikiwa kwa kuzingatia kigezo chochote kile kwani haijabainisha kuwa ni kiwango gani cha fedha kitapaswa kulipiwa faini hiyo na hivyo kinaweza kutumika kama kishawishi katika kuvutia wahalifu na haswa makampuni kutumia mwanya huu kupitisha fedha nyingi haramu kwani wanajua kuwa wakibainika wanauwezo wa kulipa faini hiyo na kuendelea na biashara zake kama kawaida.

Kambi ya Upinzani, inaona faini hizi haziko kiuhalisia hivyo tunaona faini ziwekwe kwa kutumia asilimia ya fedha atakazotuhumiwa nazo na kiwango hiki kiwekewe jedwali kuwa kama mtu binafsi atakuwa amehusika katika kutenda kosa basi kiasi cha fedha ambazo zimepatikana kutokana na uhalifu huo kitozwe faini ya asilimia 50 , na kwa upande wa taasisi zitozwe kiasi cha asilimia 65 ya fedha zote zinazohusishwa pamoja na kupewa adhabu ya kufungiwa kuendelea na biashara kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja .

Mheshimiwa Spika, kabla ya bunge lako kukubaliana na pendekezo hili la serikali la kupitisha mabadiliko haya , yafaa kwanza likapewa majibu kwenye mambo yafuatayo;

kwanini sheria ya mwaka 2006 ambayo leo inatakiwa kubadilishwa haikutungiwa kanuni za utekelezaji? Je? Nini kitatufanya tuamini kuwa hii itatekelezwa kikamilifu.

Je? Mabadiliko haya yanatosha katika kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za biashara ya fedha haramu?

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

.............................................

Christina L.Mughwai(Mb)

k.n.y Waziri Kivuli Wizara ya Fedha
 
so what? Ulitaka waongelee v2 wasivyovijua? Hotuba nzuri..
Binafsi nimesikitishwa kuona serikali au inajua au haijui uchafu huu, lakini chama makini kimefafanua vema bila mawaa! Naishauri serikali bila woga wala haya watumie maandiko hayo kutekeleza!
 
Back
Top Bottom