Nikajifanya kutaka ujiko, demu akaniletea noma……….!

Katika watu ambao wamepambana na misukosuko hapa jijini, naweza kusema mimi ni mmoja wao. Na labda niseme tu kwamba tabia yangu ya kiherehere na kupenda ujiko, iliniletea kasheshe nyingi sana kiasi kwamba mpaka leo hii nikikumbuka mapito niliyopitia, wakati mwingine huwa nacheka mwenyewe. Nisiwapotezee muda, ngojeni niwasimulie hili kasheshe nililolipata miaka ya tisini.

Nakumbuka kipindi hicho nilikuwa nakaa kwa dada yangu maeneo ya Mwananyamala, ambaye alinichukua kwa mjomba wangu niliyekuwa nikiishi naye maeneo ya Tandale. Lengo lilikuwa ni kunitafutia kozi yoyote ili niweze kujimudu, kwani matokeo yangu ya kidato cha nne niliangukia pua.

Siku nilipokutana na dhahama hiyo ilikuwa ni kipindi cha sikukuu ya Pasaka. Siku hiyo nilitoka nyumbani kwa dada yangu Mwananyamala kwenda kwa rafiki yangu aishiye maeneo ya Kinondoni. Huyu jamaa alikuwa ni rafiki yangu ambaye nilikutana naye maeneo ya club moja maarufu maeneo ya Mwanayamala iliyokuwa ikijulikana kama Mwanayamala Club Villa. Nilikutana naye hapo wakati wa mashindano ya disco, kipindi hicho ule mtindo wa break dance ndio ulikuwa umeshika kasi, na mimi na yeye tulikuwa ni miongoni mwa vijana tulioingia fainali, wakati huo nilikuwa naweza kujinyonga hasa kwa mtindo huo wa break dance na ndio chanzo cha kujuana na huyo kijana.

Na yeye kama mimi alikuwa ameangukia pua kidato cha nne, lakini mwenzangu alikuwa ametafutiwa shule ya kulipia huko Moshi ili aendelee na kidato cha tano. Huyu mwenzangu wazazi wake walikuwa wanajimudu kidogo, kwa hiyo mara nyingi tukienda kujirusha jamaa ndiye alikuwa mfadhili wangu.

Siku hiyo, tuliamua kwenda beach ambapo jamaa yangu alikuwa ametafuta wasichana wawili wa kujirusha nao. Ile jioni tulipokutana jamaa yangu alinambia kwamba itabidi nichukue msichana mmoja lakini akaninong’oneza , ‘inabidi ujifanye mtoto wa mtu mkubwa, maana demu mwenyewe ni mtoto wa kigogo.’

Mimi bila kumuuliza ni mtoto wa nani nilichangamkia ‘tenda.’ Jamaa hakuniangusha, alinipatia shilingi 6,000 na mimi nilikuwa na kama 1,200. Kwa kipindi kile hizo zilikuwa ni hela nyingi za kutangazia ujiko.

Basi jamaa akamchukua demu wake na mimi nikamchukua demu wangu, tukaenda kila mtu njia yake. Tulifika kwenye kona moja tukakaa na kuagiza vinywaji, kisha tukaanza kupiga stori. Yule msichana akaniuliza jina langu na ninaishi wapi, yaani akitaka kunijua vema.

Na mimi kwa kiherehere changu na kupenda ujiko, nikatafuta jibu la haraka haraka, Nilimtaja kigogo mmoja ambaye wakati ule alikuwa ni waziri kwamba ndiye baba yangu. Yule msichana aliniambia, ‘nakuuliza kweli, siyo mzaha.’ Lakini mimi kwa akili yangu ya kifisi maji niliendelea kusisitiza kwamba yule kigogo ndiye baba yangu. ‘ Am very serious na wala sitanii yule ndiye baba yangu kabisaa’ niliweka msisitizo wa madai yangu kwa kukoleza na kiingereza changu cha kuombea maji.

Yule msichana alionekana kukereka na alisema, ‘sasa mbona sikufahamu, wakati huyo mzee ni baba yangu mdogo na ninaishi kwake.’ Kwanza nilidhani ni mzaha, lakini aliponikazia macho na kuzidi kuniuliza, nilibabaika kidogo na kujikuta nikianza kuchanganyikiwa. Lakini akili yangu ikafanya kazi harakaharaka na kupata jibu la kuua soo……………… Si mnajua wanaume hawakubali kushindwa kirahisi, hasa na mwanamke!

Nikamwambia kwamba, huyo mzee ni mlezi wangu, ndiye anayenilea, ingawa ninaishi na mama yangu. Yule binti ambaye alionekana kunitazama usoni kwa makini kama anasoma mawazo yangu, alinitupia swali la kushtukiza. ‘je unawajua watoto wake?’

Nilijikuta naropoka, ‘ndiyo nawafahamu watoto wote wa yule mzee.’ Yule binti ambaye nadhani amesomea saikolojia ya kuwabaini watu waongo, aliniuliza kuhusu mtoto wa yule mzee aliyefariki miezi miwili iliyopita. Kwa kweli sikuwa najua chochote, nikabaki nimeduwaa nisijue nijibu nini.

Yule msichana alianza kunituhumu kwa kujikweza. ‘kama umetoka familia masikini si useme tu, kwani mapenzi unadhani ni lazima mtu awe na fedha au umaarufu!’ Alianza kunisomea, na kwa sababu alikuwa ameshapata moja moto moja baridi, aliongea kwa kelele kubwa bila staha kama mwanamke. Ilibidi jamaa yangu ambaye hakuwa mbali na tulipo waje na mpenzi wake ili kujua kulikoni.

Yule binti alimwambia jamaa yangu. ‘Nini bwana unanipa mshamba huyu, sijui katokea Mbwinde huko, anajifanya kujikweeza na kunibania pua. Anataka ukubwa wa kulazimisha, mwambie aache hizo.’

Jamaa yangu alinivuta kando na kuniuliza kulikoni. Nilipomsimulia, alihamaki na kushika mdomo. ‘Ah umeharibu, huyu binti, huyo ni baba yake mdogo na amemlea tangu akiwa mdogo.’

Kama mjuavyo watu wa Dar hawataki kupitwa na jambo, walijisogeza karibu ili kujua sababu ya ile tafrani, na yule binti ambaye alikuwa anaongea kama cherehani, aliendelea kunipaka kishenzi, na kila kitu kikawa hadharani…………….

Watu walikuwa wakiniangalia kwa huruma na wengine wakinicheka kwa ushamba wangu. Uso wangu ulisawajika kwa tahayari nikawa kama vile nimeachwa uchi……………

Najua mnataka kujua kilichojiri baada ya pale. Kwa bahati mbaya nimepoteza kumbukumbu. Kwani nyie mnadhani ni kitu gani kiliendelea………………tafuteni jibu………………………LOL

Mtambuziiiiiiiiiiiiiiiiii!!!!!!!!!!!!!!! Story zako zinaniachaga mie hoiiiiiiiiiiiiiiiiiii!!! Aksante kwa kuniongezea siku za kuishi. Hadithi hii inatufundisha ule msemo wa acha Mungu akukweze, husijikweze mwenyewe. Siku hizi sioni kile kidude cha thank u. Nimekugongea kwa huku huku, nadhani utakuwa umeona cha kwamba nimegonga like.
 
unamuacha alipe mwenye,unajiondokea kimyakimya na kupitia mwananyamala pale kuna dada poa unamchukua mmoja unabonyeza kinanda hadi asubuhi.
 
Kwa taarifa yako tu ni kwamba, mimi nilikuwa ni mmoja wa waandishi wa visa hivi katika hilo gazeti.............................

Kwa maana hiyo hapo juu, unakiri kwamba una - copy na ku paste kutoka gazeti tajwa au? Bana sitaki kusikia hivyo, maana mi nikisoma naamini kabisaaaaaaaaaa kwamba ni wewe. Nitakasirika nikisikia ni vya ku-copy na ku-paste halafu nitajipunguzia siku zangu za kuishi wakati kila mara nikusoma humu ndani huwa naongeza siku zangu za kuishi.
 
Back
Top Bottom