Ni maneno, maneno na maneno zaidi

saitama_kein

JF-Expert Member
Oct 29, 2009
981
99
KATIKA pekuapekua yangu, mwishoni mwa wiki, nilikutana na hotuba ya Rais mstaafu, Ben Mkapa aliyoitoa kwenye kikao cha Bunge la kwanza la vyama vingi, Novemba 30, 1995 kwenye ukumbi wa Karimjee, mjini Dar es Salaam.
Nilijikuta nikiacha kutafuta nilichokuwa nikitafuta na kuisoma hotuba hiyo ya Mkapa yenye kurasa 32. Ni hotuba iliyojaa maneno mazito yenye kuleta matumaini ya kumalizwa kwa matatizo mengi yaliyoikwaza Tanzania yetu kimaendeleo kwa muda mrefu.
Nilipomaliza kuisoma hotuba hiyo ya Mkapa nikashawishika kuitafuta hotuba ya Rais wa sasa, Jakaya Kikwete wakati naye alipohutubia Bunge kwa mara ya kwanza, Desemba 30, 2005, mjini Dodoma, ikiwa ni siku chache tu baada ya kushinda urais.
Hotuba yake, sawa na ilivyokuwa ya Mkapa, nayo ilijaa maneno mazito yenye kuleta matumaini ya kujengwa kwa Tanzania mpya – Tanzania yenye neema na maisha bora kwa kila mwananchi.
Lakini sikuishia hapo. Hotuba hizo mbili za Mkapa na Kikwete za 1995 na 2005 zikanichochea kutafuta nakala za ilani za uchaguzi za CCM za mwaka 1995 na 2005.
Ilani hizo nazo pia kimsingi zilifanana kwa kuwa na maneno mazito yenye kuleta matumaini mapya ya kujengwa kwa Tanzania mpya.
Nilichogundua, mpenzi msomaji, ni kwamba alichokuwa akikizungumza Mkapa katika hotuba yake hiyo ya kwanza bungeni (1995) na alichokizungumza Kikwete katika hotuba yake hiyo ya kwanza bungeni (2005), kimsingi ni hicho hicho.
Aidha, ahadi na vipaumbele vilivyomo kwenye ilani hizo mbili tofauti za uchaguzi za CCM, kimsingi ni zilezile. Unaweza kabisa kusema kwamba kilichofanyika katika vyote viwili; yaani hotuba na ilani, ni re-cycling ya mambo yale yale ya kale!
Hitimisho langu baada ya kuwa nimezisoma hotuba hizo na ilani hizo, ni kwamba yetu ni nchi ya kubwabwaja maneno. Maneno, maneno na maneno zaidi; lakini maneno yasiyotoka moyoni, na hivyo yasiyoendana na matendo ya dhati.
Nasema hivyo, mpenzi msomaji, kwa sababu kama watawala wetu hao wawili wangekuwa wanaamini katika maneno yale waliyoyatamka katika hotuba zao au kama chama chao CCM kingekuwa kinaamini katika ilani zake za nyuma, hakika tungekuwa tumeianza safari yetu ya kutoka “C” kuelekea “B” ili nasi hatimaye tufike “A”.
Lakini kwa sababu yalikuwa ni maneno tu yasiyoendana na vitendo, takriban miaka 15 bado Taifa limesimama pale pale “C”, na wala hatujui safari yenyewe tutaianza lini; maana yaelekea kila rais wa tiketi ya CCM atakayeingia Ikulu ata-recycle tu ahadi na mambo yale yale ya rais mwenzake aliyemtangulia.
Nirudie tena kusisitiza kwamba yetu nini nchi ya maneno, maneno na maneno zaidi! Tunapoteza muda mwingi katika kubwabwaja maneno kuliko katika kutenda. Yetu ni nchi ambayo maneno hayaendani na matendo.
Ni nchi ambayo tumekuwa mazezeta kiasi kwamba tunasisimshwa na maneno matamu yanayoporomoka kutoka vinywa vya watawala wetu, na si matendo yanayopaswa yaendane na maneno hayo!
Labda nitoe mfano mmoja. Katika hotuba hiyo ya kwanza bungeni ya Mkapa ya Novemba 30, 1995 alizungumza sana; tena kwa ukali kuhusu uadilifu, na akatangaza vita dhidi ya wezi na wabadhirifu wa fedha za umma.
Katika moja ya aya za hotuba hiyo, Rais mstaafu Mkapa aliwaonya watendaji serikalini kwamba watakaoshindwa kuheshimu taratibu za fedha watasimamishwa kazi, na hata kufungwa na kufilisiwa mali.
Hebu natujiulize; kama kweli Mkapa alikuwa anamaanisha katika hicho alichokisema, ni watumishi wangapi wezi na wabadhirifu wa fedha za umma walifungwa (achilia mbali kufilisiwa mali zao) katika kipindi cha miaka 10 ambacho yeye alikaa Ikulu?
Je, si kweli kwamba katika kila mwaka aliokaa Ikulu katika kipindi hicho cha miaka 10, ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ilikuwa inaonyesha wizi wa kupindukia wa fedha za umma karibu katika kila sekta na kila idara?
Lakini ukiisoma hotuba ya kwanza ya Kikwete bungeni ya Desemba 30, 2005 utaona kwamba naye alitoa ahadi hiyo hiyo ya kupambana na wezi wa fedha za umma. Lakini naye, kama ilivyo kwa Mkapa, ripoti ya CAG katika kila mwaka mmoja wa miaka minne aliyokwishakaa madarakani inaonyesha kitu kile kile – wizi, wizi na wizi zaidi!
Kwa maneno mengine, hapa tunazungumzia miaka 14 (ya Mkapa 10 na Kikwete 4) ya kushughulikia tatizo hilo hilo moja bila mafanikio yoyote – tatizo la wizi wa fedha za walipakodi wa nchi hii.
Hakika, mtu unasukumwa kujiuliza: Kama katika miaka 14 tumeshindwa kumaliza tatizo moja tu linalopigiwa kelele kila mwaka kwenye ripoti za CAG, tupewe miaka mingapi kulimaliza?
Labda tujiulize: kwa nini inakuwa hivyo? Kwa mtazamo wangu, inakuwa hivyo kwa sababu maneno ya ahadi ya kupambana na tatizo hilo yanayotoka vinywani mwa watawala wetu, hayaanzii moyoni.
Kwa maneno mengine, wenyewe hawayaamini maneno hayo, na ndiyo sababu hayaambatani na matendo. Kwa mfano, kama Mkapa angekuwa akiyaamini maneno hayo aliyoyatamka Novemba 30, 1995 kuhusu vita dhidi ya wezi wa fedha za umma, utawala wake kihistoria za wizi wa fedha za umma za aina ya EPA, Meremeta, Twin Towers, Rada nk.
Lakini baya zaidi ni kwamba, kwa kuwa na sisi wananchi ni watu wa maneno maneno yasiyoendana na matendo, tumeshindwa kuwawajibisha kina Mkapa; maana hatuoni ubaya wa watawala wetu kutuonyesha usanii wa maneno usioendana na vitendo. Wachache wanaododosa wanajibiwa kwa Kiingereza; ‘what is the big deal?; yaani cha ajabu kipi?
Kwa hakika, kubwabwaja maneno tusiyoyaamini wenyewe na ambayo hatuwezi kuyasimamia utendaji wake kwa sababu wenyewe hatuyaamini, umekuwa ndiyo utamaduni wetu mpya wa Watanzania!
Nimetoa tu mfano wa Mkapa na Kikwete kwa kuwa wao ni viongozi wanaopaswa kutuonyesha njia kwa vitendo, lakini ukweli ni kwamba hili ni tatizo linaloanzia mbali – kwenye nyumba zetu, shuleni, mitaani, ofisini, kanisani, msikitini, magazetini, redioni (hasa za FM), na hata bungeni. Huko kote ni maneno tu yanayobwabwajwa yasiyoendana na matendo.
Ndiyo, na hata bungeni! Jaribu kuangalia kwenye televisheni nyuso za baadhi ya mawaziri wanapojibu maswali ya wabunge, utagundua kwamba wao wenyewe hawayaamini majibu wanayoyatoa.
Wengi majibu yao yanakuwa ni ya kisanii, yenye kutoa matumaini ya kutatuliwa matatizo yanayoulizwa; hata pale ambapo uwezekano wa kuyatatua kwa wakati ule haupo! Na kwa kuwa mbunge naye ni uzao wa jamii hiyo hiyo iliyoathirika na utamaduni huo wa kubwabwaja maneno yasiyoendana na vitendo, anayakubali kirahisi maneno yaliyomo katika jibu la waziri!
Angalau katika hilo bado heshima zangu zipo kwa Waziri Mkuu wa zamani, marehemu Edward Sokoine. Waziri Mkuu huyo wa zamani, ambaye mpaka sasa hana mfanowe, hakuwa mbwabwaja maneno asiyoyaamini. Kila alichokisema alikiamini na alikisimamia utekelezaji wake kwa nguvu zake zote.
Wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka kwamba Sokoine alikuwa na kawaida ya kusimama bungeni kuwasahihisha mawaziri wake pale wanapobwabwaja maneno wasiyoyaamini wenyewe au pale wanapotoa ahadi kwa wabunge ambazo hazitekelezeki.
Nakumbuka siku moja waziri mmoja aliulizwa na mbunge ni lini serikali ingeiwekea lami barabara ya jimboni kwake, na yeye waziri akajibu kwamba Serikali italiangalia suala hilo haraka iwezekanavyo.
Sokoine alikasirishwa mno na jibu hilo kiasi kwamba alisimama na kumwambia mbunge yule kwamba serikali haikuwa na fedha za kuijenga barabara ile, na kwamba asimpe mbunge jibu la uongo; maana hapakuwa na fungu lililotengwa kwa ajili ya ujenzi huo kwenye bajeti ya serikali!
Ni dhahiri, Sokoine hakupendezwa na jibu la udanganyifu la waziri wake yule ambaye alilitoa huku mwenyewe akiwa haliamini moyoni; kwani, kama waziri, alijua kabisa kwamba hakuna fungu la fedha lililotengwa kwa ajili ya barabara ile.
Usanii wa waziri huyo wa kubwabwaja maneno asiyoyaamini mwenyewe moyoni ulizimwa na Sokoine pale pale ndani ya Bunge, na wala hakungoja kikao cha kebineti kumtahadharisha waziri yule juu ya majibu yake ya kisanii. Na kuanzia muda ule, mawaziri wakawa makini katika majibu yao kwa wabunge!
Ndugu zangu, laiti tungekuwanaye Sokoine kwa muda mrefu serikalini kama PM, watawala wetu wasingejenga utamaduni huu wa kubwabwaja maneno yenye ahadi tamtam wasizoziamini wao wenyewe mioyoni mwao.
Leo hii, watawala watasimama jukwaani na kutoa hotuba kali kali dhidi ya ufisadi, lakini inapokuja kwenye kutenda ni hao hao wanaocheza usanii kuwaepusha maswahiba wao mafisadi wasifukuzwe CCM au kunaswa na mkono wa sheria. Kwa hiyo, wanachofanya ni yapping tu!
Mfano mzuri ni kikao cha NEC kilichomalizika juzi huko Dodoma kilichojaribu kumaliza uhasama wa kimakundi ndani ya CCM ambao chanzo kikuu ni ufisadi, wajumbe walizungumza na kujadili hadi saa 7 usiku, lakini mwisho wa yote hawakuibuka na maamuzi yoyote ya maana!
Laiti angekuwepo Sokoine, nchi yetu isingekuwa a yapping nation ambako watawala na watawaliwa wote wako katika kiwewe (frenzy) cha kubwabwaja maneno matamu ambayo mioyo yao yenyewe haiyaamini – maneno yasiyoendana na matendo.
Kama Sokoine angelikuwa hai na Mwalimu Nyerere akamkabidhi nchi kuiongoza wakati alipostaafu mwaka 1985, watawala wetu, leo hii, wasingethubutu kutujia tena mwaka huu wa uchaguzi wakiwa na maneno yale yale matamu wasiyoyaamini ya ahadi walizotupa miaka 15 iliyopita!
Wasingethubutu; kwa sababu Sokoine angekuwa ameshatukomboa kwa kutupa werevu na ujasiri wa kukataa kudanganywa kirahisi na usanii wa wanasiasa wetu, na hasa wa chama tawala CCM!

Source:
Raia Mwema
Johnson Mbwambo
Februari 17, 2010
 
Back
Top Bottom