Mwanajamii
JF-Expert Member
- Mar 5, 2008
- 7,063
- 68
Balozi ziko hoi kifedha. Ni taarifa iliyowekwa wazi na vyombo vya habari leo. Hii taarifa imekaaje?
Tusaidiane kutafuta ufumbuzi, matusi tuweke pembeni. Tujenge hoja namna ya kujinasua na hali hii.
CHANZO: NIPASHE 14 FEBRUARI, 2012
MABALOZI WA TANZANIA HOI
Tusaidiane kutafuta ufumbuzi, matusi tuweke pembeni. Tujenge hoja namna ya kujinasua na hali hii.
CHANZO: NIPASHE 14 FEBRUARI, 2012
MABALOZI WA TANZANIA HOI
Ni ukata mkali hadi mishahara hakuna
Katibu Mkuu asema hali ni tete mno
Wakati Serikali ikikabwa koo na madaktari juu ya madai ya nyongeza ya posho na mishahara yao, hali kadhalika walimu wakiwa wamekwisha kutoa ilani juu ya nyongeza ya mishahara yao, imethibitika kwamba Ofisi za Tanzania nje ziko hoi kutokana na kukosa fedha za matumizi ya kawaida.
Kama haitoshi, baadhi ya balozi zinadaiwa kuendeshwa bila mishahara kwa kipindi kirefu sasa, hali inayovunja heshima na hadhi za ofisi hizo ughaibuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, alibainisha hali hiyo jana jijini Dar es Salaam mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Haule alisema kwa mwaka 2011/2012, serikali ilitenga Sh. bilioni 150 kwa ajili ya matumizi ya kawaida, lakini Hazina iliwapa Sh. bilioni 80 na kwamba hatua hiyo imeifanya wizara yake kuwa na wakati mgumu katika kulipa mishahara pamoja na kugharamia uendeshaji wa ofisi za balozi.
Alithibitisha kuwa, kushuka kwa sarafu ya Tanzania kunachangia hali hiyo na kwamba serikali inashindwa kumudu kulipa mishahara kwa kuwa watumishi wa balozi za Tanzania wanaolipwa kwa Dola ya Marekani kutokana na bajeti kutengwa kwa kutumia shilingi.
"Nikiri kwamba hali katika balozi zetu ni mbaya kutokana na ukata unaoikabili wizara yangu ambayo inaziangalia balozi hizi," Haule aliwambia wajumbe wa kamati hiyo ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo.
Haule aliongeza kuwa, bajeti ya kuzihudumia balozi za Tanzania inazidi kupungua mwaka hadi mwaka. Ingawa hakutoa takwimu, lakini alisema hali hiyo imekuwepo kwa kipindi cha miaka saba hadi sasa.
Katika kudhibiti matumizi ya fedha kidogo ambazo wizara yake inatengewa na serikali, Haule aliambia kamati hiyo kuwa serikali imezuia mafao ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania, Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, Mustafa Nyang'anyi, baada ya kubainika kwamba alitumia fedha za huko Dirham 31,000 (Sh. milioni 13, 402,081.20) bila kuzitolea maelezo.
Haule alisema kuwa, zaidi ya shilingi milioni tano alizostahili kulipwa kama mafao zimezuiliwa na kwamba serikali itaendelea kumdai fedha zingine kwani hizo hazitoshi kulipia kiasi anachodaiwa.
Kuhusu mahusiano ya kimataifa, Haule, alisema Tanzania imefunga ubalozi wake nchini Uholanzi kutokana na matatizo mbalimbali yakiwemo ya kupishana mtazamo wa masuala mbalimbali.
Kwa upande wake, Cheyo, alisema anasikitishwa na kitendo cha serikali kushindwa kuwalipa mishahara watumishi wake katika balozi zake.
Cheyo alisema mtumishi akiwa hapa nchini akikosa mshahara angalau anaweza kwenda kukopa kwa ndugu yake, lakini anapokuwa nje ya nchi anapata shida na kuishia kukopa benki.
Alisema ni aibu kwa Tanzania kuendesha ofisi zake za nje kwa kuhaingaika na kwamba lazima serikali ihakikishe inachukua hatua na kumaliza tatizo hilo.
"Kwa miaka 50 ya uhuru wa Tanzania sikutegemea kama balozi za Tanzania zitaendeshwa nama hii kwa kukosa fedha na watumishi wake kuendelea kuhangaika," alisema Cheyo, ambaye aliongozana na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zainabu Vulu na wajumbe wengine.
Kamati hiyo ilipitia hesabu za Wizara hiyo na kubaini kwamba katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda matumizi yake yalizidi na kumuagiza Haule kufuatilia suala hilo na kuwapatia taarifa.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, Haule, alifuatana na maofisa kadhaa wa wizara na taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo.
Hivi karibuni madaktari waligoma nchini wakidai nyongeza ya posho na mishara yao, mgomo ambao ulisababisha kukosekana kwa huduma za kitabibu katika hospitali kuu nchini kwa takribani mwezi mmoja.
Mgomo huo ulisitishwa baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kukutana nao na kutangaza nyongeza ya posho hizo, huku ikiundwa kamati ya kupitia madai ya nyongeza ya mishahara ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi, na kuwachunguza Katibu Mkuu wa Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu, Dei Mutasiwa, kwa tuhuma mbalimbali za ufisadi.
Walimu nao wametaka nyongeza ya mishahara kwa zaidi ya asilimia 100 kuanzia Julai mwaka huu, vinginevyo wataanza mgomo.