Ni aibu kampuni za simu kunyonya wasanii wetu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Hakuna ubishi kwamba katika mataifa yaliyoendelea wasanii wanaishi maisha ya kifahari kwa sababu ya mapato halali yanayotokana na kazi zao. Kila kazi ya msanii katika mataifa yaliyopiga hatua ina hati miliki, kwa maana hiyo matumizi yake yanaendana na malipo.

Kwetu hali ni tofauti. Pamoja na ukweli kwamba usanii ni kipaji pamoja na juhudi ya kujituma katika kutengeneza kazi bora za unanii na zinazokubalika kwa walaji, ulinzi wa kisheria wa kazi hizo ni jambo lenye umuhimu wa kipekee.

Uwapo wa sheria hizi hujenga mazingira ya kisheria ya kulinda kazi za wasanii na kuwahakikishia mapato halali kutokana na jasho lao; huu ndiyo umekuwa msingi wa wasanii katika mataifa yaliyopiga hatua kunufaika na vipaji pamoja na jasho lao katika kazi hiyo ya burudani.

Kwetu Tanzania kazi ya usanii imekuwa ni ya kubaingaiza mno, siyo kwa sababu kazi zinazotengezwa na wasanii ni mbaya, ila kutokana na makundi mbalimbali yaliyojipanga kujinufaisha na kazi hizo kwa hila, hawa ni kuanzia wale wanaojipachika majina ya mapromota, wasambazaji wa kazi za wasanii na hata vituo vya redio na televisheni ambavyo hunufaika na kazi hizo bila kuwapa chochote waliovuja jasho kutengeneza kazi hizo.

Juzi wakati wa mjadala wa makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia suala la wizi wa kazi za wasanii liliibuka kwa nguvu kubwa.

Kwa bahati mbaya sana waliotuhumiwa kufanya dhambi hiyo ni kampuni kubwa za simu za mkononi. Ni jambo la kusikitisha kwamba hata kampuni makubwa kiasi hicho nazo zinaingia katika mkumbo wa kujinufaisha kimapato na kazi za watu wengine bila kujali kuwarejeshea chochote cha maana.

Bunge lilielezwa kuwa ipo kampuni moja ya nje ambayo imeingia mkataba na kampuni za simu za mkononi wa kuuza nyimbo za wasanii kama miito ya simu (ringing tone).

Katika mapato yanayotokana na miito hiyo, kampuni hizo hutoza Sh. 400 kwa kila mwiito kwa siku na Sh. 37 kila mtumiaji wa simu anapoutumia wimbo husika.

Cha kustaajabisha katika mapato hayo ni kwamba asilimia 80 ya mapato hayo huchukuliwa na kampuni za simu huku kampuni iliyongia mkataba na kampuni hizo ikiondoka na asilimia 13 wakati msanii mwenye wimbo wake akiambulia asilimia saba tu!

Kwa vyovyote itakavyoangaliwa, mpangilio wa mgawo wa mapato haya unaakisi kitu kimoja, siyo wa haki. Kama taifa siyo tu tumeshindwa kulinda rasilimali zetu kama ilivyo katika mikataba ya madini, gesi na kwingineko, bali pia hata kazi za mikono na jasho la watu wetu hatuwezi kuilinda.

Kuna habari kuwa kampuni iliyoingia mkataba na kampuni hizi za simu za mkononi mbali ya kujinufaisha isivyo halali, hata haijasajiliwa nchini.

Tunapata shida sana kujua inakuwaje kama taifa tunakuwa watu wanyonge kiasi cha kushindwa kutetea maslahi yetu kama taifa na hata ya watu wake, kama ilivyo kwa kazi za wasanii huku tukiachia wachache wajanja kujinufaisha kwa jasho la wengine tena katika mazingira yaliyojaa hisia kwamba hata serikali haipati mapato yake halali katika biashara ya kuuza kazi za wasanii kwa njia ya miito ya simu.

Serikali inatambua kwamba usanii ni kazi, inajua fika kwamba kwa miaka na miaka kumekuwa na kilio juu ya madhila wanayofanyiwa wasanii, kisa, kazi zao kutokulindwa na hata serikali haitaki kutumia vyombo vyake kuhakikisha kuwa haki inatamalaki kwenye tasnia nzima ya muziki na usanii kwa ujumla.

Maelfu ya vijana kwa sasa wamekimbilia kujiajiri katika kazi za usanii, wanajituma kwa nguvu zao zote ili walau wajikomboe dhidi ya umasikini kwa kutumia vipaji walivyojaliwa na muumba, lakini kwa bahati mbaya kampuni kubwa kwa kutumia tu udhaifu wa usimamizi duni wa serikali wanajipanga kunyonya vijana hawa bila huruma.

Ni vema serikali ikatambua kuwa mkakati wa kukuza ajira kwa watu wake ni pamoja na kuweka mazingira ya watu kujiajiri, na pale wanapojiajiri wahakikishiwe kuwa jasho lao haliporwi tu hivi hivi kwa faida ya kikundi fulani katika jamii bila kuwako kwa makubaliano ya haki miongoni mwa wahusika.

Tunatambua kwamba kuanzia mwaka huu wa fedha (2012/13) serikali imetangaza kuanza kutumika kwa stika maalum kwa kazi za wasanii (muziki na filamu), lakini tunasema hayo peke yake bila kubana kampuni kubwa kama hizi za simu zinapotumia kazi za wasanii kulipa malipo halali na ya haki, bado ukombozi wa wasanii utakuwa haujatimia. Tunataka hatua zaidi kulinda kazi za wasanii wetu.



CHANZO: NIPASHE


 
Back
Top Bottom