Nguzo: Serikali imetudhulumu fedha zetu toka Uingereza

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
0000000001mkoooo.jpg

*Ana miaka 119
* Alipigana Vita ya Pili ya Dunia
Na Florence Majani
NI saa tano za asubuhi, basi litokalo Mabibo kuelekea Posta linashika breki katika kituo cha Usalama, eneo la Magomeni.
Katika kituo hiki, anaingia abiria mmoja pekee … ambaye mkononi ameshika mkwaju.

Abiria huyu amevaa koti, ambalo lina kitambulisho kikubwa, chenye picha yake ndogo na maandishi yanayosomeka:

“Abdallah Salimu Nguzo. Askari aliyepigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia, 1939-1945”
Kitambulisho chake kinaeleza hata namba yake ya uaskari kuwa ni 186421.

Sura yake iliyojawa na makunyanzi inaonyesha dhahiri kuwa amekula chumvi nyingi. Halikadhalika mwendo na kibiongo kilichojitokeza katika mgongo wake vinathibitisha hilo. Aidha, anapopewa shikamoo, anajibu, lakini mdomoni hana jino hata moja.

Udadisi wa kubaini mengi kumhusu mzee huyu,unakatisha safari yangu na kushuka katika kituo cha Fire, anachoshuka.
Mzee Nguzo anasema hakumbuki mwezi aliozaliwa, lakini anachokumbuka ni kuwa alizaliwa mwaka 1893.

Anasema, mwaka huu ukimalizika, basi atakuwa amefikisha miaka 120, kwani kwa sasa anayo 119!
Anaeleza sababu ya kujiunga na jeshi la Mwingereza wakati huo na kusema, chuki dhidi ya Mjerumani ndiyo iliyomfanya ajiunge na jeshi.

“Sikutaka kabisa Mjerumani arudi kutawala Tanganyika, alikuwa ni katili ajabu,” anasema.

Anasema, watawala wa Kijerumani, walikuwa wakiwatesa sana, kwa mfano, walikuwa wakitaka wabebwe na Watanganyika katika viti vyao kwa umbali mrefu.

Ilikuwa ni lazima kwa raia wengine kuisalimia kofia ya Mjerumani. Atakayekwenda kinyume na agizo hilo, basi alichapwa bakora 25.

Anaikumbuka siku aliyojiunga na jeshi, ingawa hakumbuki tarehe, lakini anakumbuka baadhi ya mambo.

“Ilikuwa mwishoni mwa mwaka 1937, mvua inanyesha, nilikuwa nakunywa chai na baba yangu,” anasema.

Anasema alisikia tetesi kwa watu kuwa Wajerumani wanakamata vijana watakaokwenda kupigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

“Sikutaka kukamatwa kwa nguvu, nilitembea kwa miguu mpaka Korogwe, nikafika katika kituo cha jeshi nikawaambia nataka kupigana vita,” anasema nguzo, akicheka na kuonyesha mapengo yake.
Anasema, Wajerumani walimpima uzito, kisha wakamsajili na akapelekwa kwa gari hadi Arusha.

“Nilipopimwa nilikutwa na paundi 120 yaani kilo 60, nikasajiliwa tukaenda Arusha, kisha Nairobi, mpaka Kisumu, eneo la Kitale ambapo ndiyo kambi ya Jeshi,” anasema

Pale walipewa mafunzo ya awali kwa mwaka, lakini kabla ya kwenda vitani walijaribiwa.
“Wakati wa majaribio nililenga shabaha kwa umahiri. Katika tundu kumi za shabaha, nilipata tisa,” anasimulia.

Anasema, baada ya kufanikiwa kulenga shabaha, alipewa cheo cha sajenti, yaani V3 na mwanajeshi Mwingereza anayemkumbuka kwa jina moja tu la utani, Afande Magongo.

Kuelekea vitani
Mwaka 1939, ndiyo wakati ambao Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilianza rasmi.

Hata hivyo, kabla hawajaenda vitani, walipata habari kuwa, Japan ililipua na kuzamisha meli iliyokuwa na silaha pamoja na askari wa Uingereza.

“Tukaambiwa ili tuepuke hatari yeyote, tusitumie bahari. Hivyo basi, tukatumia Mto Nile,” anasema.
Anasimulia kuwa safari ile ilikuwa ndefu mno, walipita katika nchi nyingi, lakini kituo chake cha vita kilikuwa Calcuta, India.

Anasema, wakiwa vitani, chakula chao kikuu kilikuwa ni nyama za kwenye makopo na biskuti, maji ya kunywa yaliletwa na ndege maalum.

Anasema, kwa kuwa, eneo alilokuwa anapigana vita lilikuwa ni eneo la milima na mabonde, hawakutumia silaha nyingine zaidi ya mabomu ya mkono na bunduki aina ya ‘machine gun’
“Tulikaa pale kwa miaka sita, hatimaye tulimshinda Mjerumani,” anasema

Baada ya hapo, Mzee Nguzo na watu wa mataifa mengine, kama Kenya na Uganda walirudi nchini mwao, wakiwa mashujaa.

Fedha zetu ziko wapi?
Mzee Nguzo anasema anashukuru kupata nafasi hii ya kutoa dukuduku lake la miaka mingi.
Nalo ni madai ya kudhulumiwa fedha ambazo Uingereza ilitoa kwa askari hao kama mafao yao.

“Nasema ukweli daima na ninataka kila mtu ausikie, Mwalimu Julius Nyerere alizipokea fedha zile toka Uingereza, lakini hakutupa,” anasema.

Anasema, inawezekana Nyerere hakuzitumia zile fedha peke yake, lakini pengine watendaji wake.
“Kwani Nyerere alikuwa na shida gani? zile fedha zitamsaidia nini? Lakini, nasikitika amefariki mapema, wakati hajatatua tatizo hili,” anasema kwa masikitiko.

Anasema, ingawa wapo askari waliofariki tayari, lakini familia zao yawezekana zipo na wanahitaji wapate haki hiyo.

Li wapi jengo lao la askari wastaafu?
Anasema, wakati huo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Edward Twining, alitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la askari wastaafu, Tanzania Legion, ambalo hivi sasa limeuzwa.

“Wakati ule Sir Twining alitoa ‘fedha tano’, ili lijengwe jengo kubwa kwa ajili ya sisi askari. Lengo ni kuwakutanisha askari ili waweze kubadilishana mawazo. Lakini nasikitika kuwa jengo hilo limeuzwa kwa raia wa Asia,” anasema.

Anamtaja mtu aliyeuza jengo hilo na kusema: “Mimi ni mzee sana, na siku zangu za kuishi zimebaki chache, sina haja ya kuficha chochote, mtu mmoja aliyeuza jengo hilo.

Anasema, eneo lile lilikuwa muhimu mno kwao kama sehemu ya makutano na kumbukumbu, lakini limeuzwa bila hata wao kuombwa ushauri.

Masikitiko yake hayakuishia hapo, lakini anakumbuka kuwa, hata ifikapo sikukuu ya mashujaa, anachopewa ni mkono tu, wa rais.
“Nasema ukweli kabisa, nashangaa sikukuu yetu ikifika ninapewa mkono tu, kisha narudi nyumbani, hakuna hata kiinua mgongo chochote kwa sisi wazee,” anasema.

Hata hivyo, anashukuru kuwa, anapokwenda kutembelea kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), hupewa chochote kinachomsukuma kimaisha.

Mzee Nguzo ambaye ana watoto wanne, wajukuu na vitukuu lukuki anasema, anaishi kwa kutegemea misaada ya watu na kiasi toka kwa watoto wake.
Anasema, katika miaka yote 119 aliyoishi, siku asiyoisahau maishani ni mwaka 1983, wakati ambapo alimpoteza mke wake kipenzi, Zaina Mwinjuma.

Kanali Paulo Gailanga, wa makao makuu ya JKT ambaye anatajwa na Nguzo kumsaidia kifedha anasema, yeye humsaidia Mzee Nguzo kama baba au babu na si kama jeshi.

“Kwa taratibu za kijeshi ukishaastafu ni Serikali inayokubeba si jeshi tena,” anasema Kanali Gailanga.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Kanali Kapambala Mgawe anakanusha madai ya mzee huyo kuhusu fedha toka Uingereza.

“Askari waliopigana vita za dunia kutoka Uingereza, walituma ujumbe tuwatafute wazee wa Kitanzania waliopigana vita hizo, kisha tuwapelekee majina, ndipo watume fedha kama zawadi kwao,” anasema Kanali Mgawe.

Anasema, Kanali Gailanga alizunguka Tanzania nzima kuwatafuta wazee hao. Walipopatikana, majina yao yalitumwa. Kinachosubiriwa ni kuwasili kwa wanajeshi hao toka Uingereza.

Nguzo: Serikali imetudhulumu fedha zetu toka Uingereza

“Askari hao wakifika hapa, watawatambua wenzao kwa maneno au namba za siri maalum, ambazo walizitumia enzi hizo wakati wa vita, ndipo watawakabidhi fedha hizo wao wenyewe” anasema
Kuhusu kuuzwa kwa jengo la Tanzania Legion, anasema kuwa, hatua zimeshachukuliwa na pengine jengo hilo likarudishwa kwa askari hao.
“Mtu aliyefanya mauzo hayo kinyume cha sheria anashughulikiwa kisheria,” anasema.
 
Back
Top Bottom