Ngonjera za CCM na upepo wa mabadiliko

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
Na Abdallah Vuai, Zanzibar| May 23, 2012 | Zanzibar Yetu

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Tanzania Bara, Pius Msekwa akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Ujerumani wiki iliyopita aliweka bayana msimamo wa Chama chake kubakia na sera ya Serikali mbili katika Muungano. Katika mahojiano na DW Msekwa alisisitiza na kuwakumbusha wanachama wa CCM wakati watakapotoa maoni mbele ya Tume ya Katiba kukumbuka sera ya Chama hicho katika Muungano ni kubakia na Serikali mbili.

Ama kweli Msekwa ameachwa nyuma katika wakati mpya, anaonekana wazi kuwa anashindwa kubaini hisia za Wazanzibari na hata zile za wanachama wake ndani ya CCM kwamba wamechoka na sera zisizowaletea manufaa.

Muundo wa Serikali mbili umeelezwa na watu wengi kwamba ndio kiini cha matatizo mengi ya Muungano,lakini mtu kama Msekwa ambaye ameshiriki kuandika katiba ya mwaka 1977 angeweza kutoa ushauri ambao unaendana na mazingira ya sasa.

Wazanzibari wengi hawautaki Muungano wa kikatiba, wanapendelea kuwepo na muundo mpya wa Muungano usio wa Serikali mbili wenye manufaa kwao.

Sera ya Serikali mbili ni sawa na nyumba kongwe na nguo iliyochakaa, lakini kwenye macho ya CCM bado inaonekana mpya, fikra za watu wengi walitegemea kikao cha NEC kingekuja na mkakati wa ujenzi wa nyumba mpya iwe na haiba mpya na yenye mvuto hata kwa wapiti njia wakatamani nao kuwa na nyumba ya aina hiyo au ramani yake.

Nyumba hiyo iliyojengwa kwa mawe na chokaa Wazanzibari hawaipendi, hata ukiifanyia matengenezo ni yake yale,mbwa kumwita jibwa , ukiacha mawe,chokaa,udongo wake hauwezi tena kushika chokaa na pia haiwezi kuhimili vishindo,ni lazima ijengwe upya katika mtindo mpya na wa kisasa.

Ikiwa CCM itaendelea kupuuza ujenzi wa nyumba mpya ya matofali,saruji,basi
ijiandae kukataliwa na wapigakura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwani kwa hali ilivyo Zanzibar Chama chochote cha siasa ambacho kitakumbatia sera ya Serikali mbali au tatu hakitaweza kupata uungwaji mkono na wapigakura.

Ingawa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais mstaafu Amani Abeid Karume kabla ya kustaafu aliweka misingi imara ya kukihakikishia Chama chake kubakia ndani ya Serikali hata kikishindwa uchaguzi chini ya maridhiano ya kisiasa yaliyosababisha katiba kurekebishwa na kuwepo kwa Serikali ya umoja wa kitaifa.

Karume amemaliza kazi ya Urais na mwishoni mwa mwaka huu atamaliza kazi ya Umakamu Mwenyekiti wa CCM kwa kujijengea mazingira ambayo hata kikishika nafasi ya pili katika uchaguzi kitakuwepo,lakini hilo halikuwa lengo la Karume,lakini kwa hali ya leo mwendo wa CCM Zanzibar ni mbaya hauridhishi na zaidi tangu kumalizika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Wana CCM wanamtaja pia Naibu Katibu Mkuu mstaafu,Saleh Ramadhan Ferouz kuwa aliweza kukiongoza Chama hicho katika ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2005 na ule uliopita,lakini wanamashaka kama rekodi hiyo inaweza kuendelezwa au la.

Ile Maskani kaka ya muembe kisonge imekuwa daraja na jiko la kutafuta chejio kwa wengine, magari makubwa kwa kunufaika na siasa za kushupaliana, iwapo CCM itashindwa kukabili wimbi la mabadiko kitajikuta kikimbiwa na wanachama kama wenzao Bara wanavyohamia CHADEMA.

CCM Zanzibar inapita katika kipindi kigumu na ikiwa Naibu Katibu Mkuu Vuai Ali Vuai mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za CCM anayefanyia kazi zake Zanzibar asipokuwa makini na kukubali kusoma wakati anaweza kuingia kwenye historia ya Chama chake kuwa mshindi wa pili katika uchaguzi mkuu.

Mabadiliko ni lazima hakuna atakayeweza kuyazuia kwani wakati umebadilika,ni matarajio kwamba CCM ndio chama kilichoshinda kwa maana ya Chama tawala kiwaongoze Wazanzibari kufikia katika muundo wa Muungano wanaoutaka ambao ni ule wa mkataba sio tena wa kikatiba.

Na iwe itakavyokuwa, hali halisi ya muundo wa Muungano unahitaji mabadiliko ambayo yatakubaliwa na Wazanzibari,lakini hatua yoyote ambayo inawanyima haki hawatakubali kwani nguvu ya umma ambayo imeoneshwa katika mikutano tofauti ya kudai kuwepo kwa mfumo mzuri wa muungano haiwezi kuzuilika kwa ngonjera za CCM.

CCM inapaswa kutumia fursa ya kuandika kwa Katiba mpya kutoa ushawishi wa kubadili mfumo wa muundo wa muungano ambao kilio cha Wazanzibari kwa sasa kama walivyoamua kuvuana magamba basi nawaamuwe kuvua muundo mkongwe wa Serikali mbili, kwani "ukiamua kula Mbwa ule Mbwa wa Kizungu, usile Popi anayeshinda kwenye majaa. "

Mfano wa Popi isije kutafsiriwa kuwa ndio kitoweo sahihi cha Watanzania ni kujaribu kutoa tofauti ya Mbwa wa Kizungu na Popi wa Tandale kwa tumbo au Chwaka.

Waafrika wengi wana imani kuwa kitu kizuri na chenye thamani hakiwezi kuwa cha Kiswahili, bali lazima kiwe cha Kizungu. Kuna Kuku wa Kizungu,mayai ya kizungu, embe ya kizungu, na Kuku wa Kienyeji!

Katika Muungano ni hivyo hivyo, Miungano ya kizungu imekuwa haina malalamiko, tazama Muungano wa Ulaya, Uingereza, Ubelgiji na hata Marekani,lakini Afrika wapi leo uko wapi Muungano wa Senegal na Gambia,uko wapi Muungano wa Ginneu, Misri na Morocco,Sudan, Ethiopia?

Yawezekana kabisa kusambaratika kwa Muungano wa Mataifa hayo kumetokana na kuwepo kwa mfumo dhaifu wa muundo,hivyo kwa kuwa Tanzania itaandikwa Katiba mpya wakati ndio huu kuweka sawa nyumba yetu.

Kwa wale wote wanaopenda kuiona Zanzibar ikirudia zama zake za kuwa kituo cha kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki hawana budi kuunga mkono kubadili muundo wa muungano kwani ikiwa tutakuwa na muungano wa mkataba Zanzibar inaweza kuwa kituo kikubwa cha biashara kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bandari huru itafanya kazi kama ilivyo katika nchi za Dubai, Emirate, Singapore, Malasyia, Hong Kong, ambapo itachangia kukuza uchumi wa eneo la maziwa makuuu.
 
Back
Top Bottom