Neno moja latosha kuvunja ndoa.

Mtambuzi

Platinum Member
Oct 29, 2008
8,810
15,393
Wote sisi, kama binadamu huwa tunashikwa na hasira kutoka muda fulani hadi mwingine, lakini kushikwa na hasira na kuziacha hasira hizo ziwaumize wale tunaodai kuwa tunawapenda ni jambo tofauti sana.

Tunapojikuta tunashindwa kuzuia kulipukwa na hasira dhidi ya wale tunaowapenda mara kwa mara, inapasa tujue pia kwamba tunaujeruhi uhusiano wetu na baadae tutauuwa kabisa.

Kuna wakati kwa sababu mbalimbali, baadhi yetu huwa tunajikuta tukitaka tu kuwakera wapenzi wetu kwa kuwapandishia kila wakati kwa milipuko ya hasira. Ni kama vile, bila kulipukwa na hasira hizo, maisha yetu yanakuwa yamepoteza maana.

Ni vigumu sana wakati mwingine kwa watu hawa kuacha tabia yao hiyo, lakini juhudi ya kujitoa ni muhimu sana. Ni muhimu sana kwa sababu, uhusiano mwingi umevunjika kutokana na hasira hizi za kila wakati, ambazo wala hazina msingi, bali zinatokana na mtu kujichukia mwenyewe.

Kutokana na hasira hizi, mara nyingi wapenzi hujikuta wakilazimika kubishana badala ya kujadili. Hawa watu wenye hasira hizi za hapa na pale, huwa siyo wasikilizaji, bali ni watu wa kulaumu, kujitetea, na kutaka kusikilizwa wao tu, kwa maana ya kushinda.

Katika uhusiano wa aina hii, hakuna uwezekano wa ustawi, bali uwezekano ni uhusiano kufa. Kwani ni mara chache ambapo huyu mpenzi mwenye hasira za mlipuko atakuwa tayari kusikiliza na kuelewa.

Jambo ambalo wapenzi wanapaswa kulifanya,. Bila kujali kama wana hasira sana au hasira nyingi, ni kujitahidi kuweka nguvu kwenye jambo wanalojadili. Watu wenye hasira za ziada, huwa hawana uwezo wa kuzingatia kile kinachojadiliwa.

Huwa na ugumu huo kwa sababu hasira za ziada huwasukuma kusema chochote ambacho kitawafanya washinde, ikiwemo kusingizia na kusema uongo. Lakini huwa wanabebwa na wimbi la hasira kiasi kwamba hawana muda wa kupima athari ya kile wanachosema.

Kuna haja ya kujua kwamba, neno moja tu la hasira, linatosha kuvunja uhusiano au ndoa. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa mtu mwenye hasira za mlipuko kujifunza kuzingatia jambo ambalo, yeye na mpenzi wake wanalijadili. Anapotoka nje ya mada, ni lazima ataropoka.

Kuna wanandoa wanabishana kuhusu shule ya mtoto kwa mfano, mwanandoa mwingine hana haja ya kusema, ‘unabisha kwa sababu hukusoma, ndilo tatizo la kuoa wanawake wasiosoma.’ Hapa ni kutoka nje ya mada kwa hasira za mlipuko.

Kuna wakati kwa sababu ya hasira za mlipuko, mpenzi anaweza kutafuta kwa makusudi jambo ambalo litamuudhi mpenzi wake. Anaweza kumwambia, ‘sibishani na mwanamke mnene kama nguruwe.’ Au mwanamke akamwambia mpenzi au mumewe, ‘mbele ya wanaume nawe unajiita mwanaume.’

Kila mmoja wetu anajua ni maneno gani akisema yatamkera mwenzake. Nasema kila mpenzi anajua eneo nyeti la mpenzi wake, ambalo akiligusa anakuwa amemuuwa kisaikolojia. Kujua huku eneo hilo hakupaswi kutumiwa vibaya na wapenzi.

Kwenye uhusiano kuna kanuni ya, ‘usimtendee mwenzio yale ambayo hupendi kutendewa.’Wapenzi wanapoweza kila mmoja kufuata kanuni hii, uhusiano huwa mzuri sana.
 
Sometime mtu anaweza kuleta topic nzuri (kama hii) ila anajikuta anavunjika moyo kwa maneno ya wazi wazi yanayoonesha kuwa wengi wataipotezea eti kwasababu tu ni refu. Kama mtu ni msomaji kweli hii haina urefu (wengine wameonyesha kwa kuahidi wataipitia kwa muda wao), nimependa.
Im back to the topic. "Kwenye uhusiano kuna kanuni ya, 'usimtendee mwenzio yale ambayo hupendi kutendewa' ".
Pia yapo ambayo wewe kama wewe unaona ni sawa kutendewa, ila unapobaini mwenzako halipendi, pia usimtendee.
 
Back
Top Bottom