Neno La Leo: Viongozi Afrika Hawana Shukrani!

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Na Maggid Mjengwa,
HISTORIA ni mwalimu mzuri. Nimekumbushia hilo mara kwa mara. Kabla ya kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill alipata kuwa waziri wa masuala ya majini ( Marine Minister). Ilikuwa ni wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Winston Churchill ambaye pia alikuwa askari mwanamaji, aliacha ofisi yake na kuongoza vikosi vya wanamaji katika vita hivyo. Na hata baada ya vita kwisha, Churchill akafanywa kuwa ‘ Waziri wa Vita’ ( Defence Minister). Baadae, Winston Churchill akaja kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.
Pamoja na ukweli, kuwa Winston Churchill aliiongoza vema Uingereza na hata kuweza kufanikisha ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, bado, Waingereza hawakumchagua Winston Churchill katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1945. Inaweza kusemwa, kuwa wapiga kura wa Uingereza hawakuwa na shukrani. Kwamba wapiga kura wa Uingereza hawakumpima Churchill kwa historia bali kwa yatakayokuja. Kuna cha kujifunza.
Maana, nchi nyingi katika bara letu hili la Afrika mwaka huu na mwakani zitatimiza miaka hamsini tangu kupata uhuru wake kutoka kwa wakoloni. Ni nusu karne. Ni muda mrefu. Yamkini shingo zetu wanadamu ni ndefu, lakini maisha yetu ni mafupi sana. Ndio, muda wetu wa kuishi humu duniani ni mfupi sana. Na historia itabaki kuwa hakimu kwa tunayoyafanya sasa.
Maana, wengi wetu tunaishi na kuziacha nchi zetu tulizozaliwa hata kabla hatujatimiza miaka 80 humu duniani. Lakini nchi tulizozaliwa tunaziacha zikiwa na wanadamu wenzetu. Ni watoto wetu, ni wajukuu zetu. Na sisi Waafrika tumekuwa ni watu wabinafsi sana. Ni watu tunaoishi bila kufikiria sana ya kesho na kesho kutwa. Tunajiangalia sisi tu.
Sehemu kubwa ya matatizo ya nchi zetu hizi yanatokana na ubinafsi huo. Na bahati mbaya kabisa, baadhi ya viongozi tuliowapa dhamana za uongozi ndio wenye kuongoza kwa matendo yenye kutanguliza maslahi yao binafsi. Katiba za nchi zetu ni kielelezo halisi cha ubinafsi huo. Maana, wakoloni walitengeneza katiba ili ziwasaidie katika kututawala. Katiba ya mkoloni ilikuwa na maana moja kubwa; kuonyesha namna ya kuwatawala watu wa nchi iliyo mikononi mwa wakoloni. Na nchi zetu nyingi zimerithi misingi ya katiba hizo za kikoloni. Katiba nyingi za nchi za Kiafrika zinaonyesha namna ambavyo Waafrika wachache walio katika mamlaka ya Kiserikali watakavyowatawala “ Waafrika” wenzao! Katiba zetu zionyeshe namna tutakavyojitawala. Na iwe ni neno la leo.
/Maggid



mjengwa
http://www.kwanzajamii.com
 
Back
Top Bottom