Neno La Leo: Unapokandamiza Mpira Uliojaa

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu Zangu,


KUNA mawili yanayoweza kutokea binadamu unapoukandamiza mpira uliojaa na hata ukabonyea. Mosi, kama umebonyea, basi, yaweza kuwa upepo umetoka kidogo. Pili, kama umebonyea, basi, yaweza kuwa mpira huo umefutuka upande wa pili.


Na kibaya zaidi, kama mpira huo ukakandamizwa kwa nguvu nyingi, basi, utapasuka. Ndio tunayoyashuhudia kule Egypt. Tumeyashuhudia Tunisia na kwingineko.


Vijana wale wa Tunis, Cairo na Suez hawana tofauti na vijana wa Kigali, Nairobi, Dar es Salaam na Kampala. Tofauti ni kwenye viwango vya uvumilivu. Ni kama kabati la nguo. Kabati likijaa nguo, na mwenye nalo akazidi kuweka nguo, basi, sio tu mwenye nalo atashindwa kulifunga, bali nguo zitaanza kuanguka.



Makabati ya vijana wa Tunisia na Egypt yameshajaa. Ndio maana tunawaona wakilala mbele ya vifaru vya jeshi . Wako tayari kwa lolote, liwalo na liwe. Makabati ya vijana wetu bado yana nafasi ya kuweka nguo. Busara kwa watala wetu ni kutosubiri yajae.


Ndio, binadamu anayekandamizwa sana hufikia kikomo cha uvumilivu. Miaka kumi iliyopita hakuna aliyefikiri vijana wale wa Tunisia na Egypt wangefanya waliyoyafanya. Wamefikia ukomo wa uvumilivu. Hata mjusi ukimwandama sana anaweza kugeuka nyoka kwako. Na paka naye unaweza kumfuga na ukamlisha vyote akanenepa. Lakini, siku ile utakapojifungia kwenye chumba kidogo, wewe na paka wako. Kisha ukachukua rungu uanze kumpiga , hakika, ukali wake utazidi wa chui. Atakurarua, paka wako mwenyewe!


Yanayotokea Egypt ni darasa kubwa kwa watawala wetu barani Afrika, kuwa unapoukandamiza mpira uliojaa na ukabonyea, basi kuna matokeo ya upepo kupungua, mpira kufutuka upande mwingine au kupasuka. Mawili ya mwisho ni lazima yatokee, ni suala la wakati tu.
Na hilo ni Neno La Leo.


Maggid,
Iringa,
Ijumaa, Februari 11, 2011
mjengwa
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom