Neno La Leo: Njau, Kalumekenge Na Ushahidi Wenye Utata!

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
KUNA kisa cha hakimu aliyepata tabu sana katika kuthibitisha ukweli wa urefu wa mtuhumiwa wa wizi. Mashahidi walikuwa wawili; Njau na Kalumekenge.

Wote wawili, Njau na Kalumekenge, walimwona mtuhumiwa akivunja mlango wa nyumba kabla ya kuingia ndani na kuiba. Utata wa ushahidi wao ni kuwa; shahidi Njau alitamka kwa kujiamini mahakamani kuwa mwizi alikuwa mfupi. Na shahidi Kalumekenge naye aliongea kwa kujiamini kuwa mwizi alikuwa mrefu. Huu ni ushahidi wenye utata uliopelekea Bwana Hakimu aumize kichwa kabla hajapata njia ya kutatua utata huo.

Hatimaye hakimu akapata njia ya kufahamu urefu halisi wa mtuhumiwa wa wizi. Ndio, hakimu alibaini, kuwa kwa vile shahidi Njau ni mrefu, yeye alimwona mwizi kuwa ni mfupi. Na kwa vile shahidi Kalumekenge ni mfupi, kwake mwizi huyo alikuwa ni mrefu. Basi, Bwana Hakimu alichofanya ni kutafuta wastani wa urefu wa Njau na Kalumekenge ili kupata urefu halisi wa mtuhumiwa wa wizi ambaye Njau na Kalumekenge walimwona kwa wakati mmoja.

Kuna tunachojifunza katika utata na utatuzi wa ushahidi huo. Na hakika, kisa hiki nilichopata kukisikia zamani sana, kimenisaidia katika kuyatafakari yanayotokea katika jamii yetu kwa sasa. Hata kama sifanikiwi mara zote, lakini nimejifunza kutafuta ‘ wastani’ wa mambo kabla ya kukurupuka na kuyatolea maoni. Ndio, aliye juu anaweza kuyaona mambo kwa mtazamo wake, na aliye chini vivyo hivyo.

Kwamba wanadamu tunayoyaona, tunayaona kwa mitazamo tofauti. Vivyo hivyo kwa tunayoyasikia na kuyaangalia. Kwamba wanadamu tuna hulka ya kusikia tunachotaka kusikia, na kuona tunachotaka kuona. Na mjinga asipojua kuwa yeye ni mjinga unafanyaje? Na hilo ni Neno La Leo.


 
Na mjinga asipojua kuwa yeye ni mjinga unafanyaje?

Hapa ni kazi kweli kweli kumuelimisha huyo mjinga ili aweze kujua kuwa yeye ni mjinga. Anaweza kukuona na wewe ni mjinga pindi unapo taka kumwelewesha tu akajua kuwa na wewe ni mjinga.
 
Back
Top Bottom