Neno La Leo: Afrika Kuku Hachimbiwi Kaburi!

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu Zangu,



AFRIKA viongozi ni wengi wanaopatwa na vigugumizi wanapoombwa watoe maoni yao kwa kile anachofanya mwenzao Ghadaffi kwa watu wake. Vigugumizi hivyo vina tafsiri nyingi; moja kuu ni ukweli, kuwa kuna viongozi Afrika wanaofanana fanana naye.


Kwamba nao wasingesita kufanya kama alivyofanya Ghadaffi pale inapotokea watu wao wanapoamua kuingia mitaani kuonyesha hisia zao kwa amani kabisa. Watatafuta visingizio vya kuwatwanga risasi watu wao ili kuwatishia wengine.


Ndio, kinachotokea Afrika ni hiki; kwanza, mtawala atawaita waandamanaji ‘kuku’ na majina mengineyo. Kisha ataamrisha vikosi vyake vitumie risasi za moto kuwadhibiti ‘kuku’ waandamanaji. Si tunajua, kuwa Afrika kuku hachimbiwi kaburi?
Viongozi Afrika watambue sasa, kuwa Afrika kuna kimbunga kimelipuka. Ni kimbunga kinachosambaa. Kimeanzia Tunisia, kikaenda Misri na kimetua Libya. Kinasambaa. Ni kimbunga cha mabadiliko.


Waafrika wengi wanaokandamizwa na watawala au vyama tawala katika nchi zao, leo wana kiu kubwa ya kuwa na ‘ Tahrir’ zao ili nao wajikomboe. Kiongozi makini, mwenye busara na mapenzi ya dhati kwa nchi yake, hatosubiri watu wake wafikie ukomo wa uvumilivu ili afanye mabadiliko hitajika na yenye kukidhi matakwa ya wakati husika.


Nimepata kuandika kuwa katika nchi, mabadiliko ya amani yanawezekana; lakini kwa anayejaribu kuyazuia atambue kuwa mabadiliko yenye vurugu hayaepukiki.


Maana tumeona Wamisri na Walibya wamefikia ukomo wa uvumilivu wa kukandamizwa. Na watu wa Afrika wameshaibaini siri ya kuwatoa madarakani wakandamizaji wao; ni kutoka mitaani kwa wingi na kuandamana kudai haki zao.


Ndio, Waafrika wameamka usingizini. Wameshatambua kuwa hakuna risasi au kombora la mtawala litakaloweza kushinda nguvu ya umma uliodhamiria kutaka mabadiliko. Yametokea Tunisia, Misri, Libya. Yanaweza kutokea popote pale Afrika. Busara ni kuenenda na wakati uliobadilika. Na hilo ni Neno La Leo.



Maggid,
WAMO- Kibwe
Morogoro
Machi 3, 2011
mjengwa
 
Mbona hii imeshatokea Tanzania? Kwani yale mauaji ya Arusha yalikuwa yanaashiria kitu gani?
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom