Ndoa zisizo na taratibu chanzo cha kukosa haki

sir.JAPHET

JF-Expert Member
May 18, 2012
699
133
Thursday, 23 August 2012 21:04

Na Mwandishi wetu, Mbeya
SABABU kadhaa zimetajwa za wanawake wengi kudhulumiwa haki zao wanapofiwa na waume.Mojawapo ya sababu hizi zimedaiwa kusababishwa na wanawake wenyewe ambao wengi huingia kwenye ndoa bila kufuata taratibu husika za ndoa.

Miongoni mwa haki wanazodhulumiwa wajane katika jamii nyingi hapa nchini, ni pamoja na kunyang’nywa mali walizochuma na waume zao, ardhi na watoto ambapo ndugu za marehemu hujiona wao kuwa na haki zaidi ya mjane.

Hayo yalibainishwa na Mratibu wa Shirika Lisilokuwa la Kiserikali linalojishughulisha na Kitengo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake na Watoto mkoani Mbeya (MBEPAU), Jane Lawa, wakati akihojiana gazeti hili ofisini kwake mjini hapa.

Lawa, alisema kuwa kitendo cha watu kuoa ama kuolewa bila kufuata taratibu zinazostahili kama vile kufunga ndoa halali inayotambulika na jamii na kupewa cheti cha ndoa, ni moja ya sababu zinazochangia kwa wanawake wengi kudhulumika mali walizochuma na marehemu waume zao.

“Kumekuwa na kasumba moja kwa watu kuoana bila ya kufuata taratibu na kuishi maisha ya ndoa kienyeji kwa vile tu wanapendana bila kutambua athari zake pindi mgogoro utakapoibuka baina yao na kutaka kuachana,” alisema Lawa na kuongeza:

“Hata ikifika mahala pindi mmoja wapo anafariki hujikuta mali zote zikichukuliwa na upande mmoja na mwingine kudhulumika, na wanawake ndiyo waathirika wakubwa katika hili na kwa vile waliooana kienyeji bila kupata cheti cha ndoa kitakachomsadia kupata haki yake mahali popote, hupoteza haki hizo,” alisema mratibu huyo.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, ili kuwa katika nafasi salama ni vyema wapendanao wanapotaka kuishi maisha ya ndoa wakafuata taratibu zinazotambulika rasmi na jamii na kupata cheti cha ndoa ambacho kitaweza kuwalinda pindi inapotokea tatizo litalowatenganisha.

Mbali na hilo mratibu huyo aliwataka wanawake kuondokana na woga au kuogopa vitisho vinavyotolewa wakati wa kudai haki zao, ambavyo huwa na lengo la kuwanyang’anya mali walizochuma na waume zao.
Inaelezwa kuwa wanawake wengi hutishwa na ndugu wa kiume kwamba endapo ataendelea ama hatatoa mali walizochuma kwa pamoja wakati wa uhai wa marehemu huyo basi watamloga, na wanapopatiwa vitisho kama hivyo huogopa na kuachia mali walizochuma na waume zao.

Hata hivyo mratibu huyo ameendelea kufafanua kuwakatika kufanikisha azma yao ya kupora mali za marehemu , jamaa hao hutumia ubabe kupora mali hizo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kutokana na hali hiyo wanawake wanashauriwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya kisheria kwa msaada zaidi.
 
Back
Top Bottom