NDIYO, CCM NA IKULU WANATUMIKIA MAFISADI - Hii imakaaje?

Mukuru

Member
Apr 14, 2009
40
0
Source: Gazeti la Mwananchi


NILIWAHI kuelezea ukigeugeu wa CCM wanapokuwa jukwani na wanapokuwa kwenye vikao vyao kwenye safu hii. Wanapokuwa jukwaani hujifanya watu wa watu na wanapokuwa kwenye vikao vyao hugeuka kuwa adui wa watu.


Jamaa hawa wanapokuwa jukwaani huzungumza kama wameshushwa na Mungu kujali maslahi ya wananchi, lakini wanapokuwa kwenye vikao ndani, huongozwa kwa nguvu za fedha za matajiri ndani ya chama. Ukinyonga huu wa viongozi na wajumbe wa NEC ndio unazisuta roho zao.


Awali kila mtu aliamini kuwa aliyekabidhiwa usukani wa chama na serikali angeweza kuishi kwa maneno yake. Aliwajengea imani hiyo katika hotuba yake ya kwanza na akaimwagilia maji aliposema hana ubia katika urais.

Miaka minne sasa matendo ya dereva huyo wa CCM na serikali yameonyesha kuwa hayuko hivyo. Ingawa katika hotuba yake ya kwanza kwenye mkutano wa kwanza wa Bunge, Desemba 30, 2005, dereva huyo alijipambanua kuwa mtu wa watu akizungumza kwa hisia juu ya mipango yake ya kuleta neema nchini, maisha bora kwa wananchi, kuwanyoa mafisadi na kuwaunganisha jamaa wa Pemba na Unguja kijamii, kisiasa na kiuchumi, iko wazi sasa amepwelea.


Leo ukiwa umesalia mwaka mmoja kuelekea uchaguzi mkuu mwingine, siyo tu ameyumba kwenye reli bali ametekwa na mafisadi wenye nguvu ndani ya chama. Unaweza kuona anavyoongozwa na mafisadi kama madereva wa daladala wanavyoamrishwa na makondakta wao.


Vita dhidi ya ufisadi aliyotamba kushinda, imemshinda; amebaki anahamisha kutoka shubaka moja hadi jingine ndani ya Ikulu majina ya majambazi, wauza dawa za kuleva, walarushwa wakubwa TRA—kwa kifupi majina ya mafisadi.


Kwa kawaida NEC ikikutana, hujadili masuala kadhaa kuhusu uendeshaji wa nchi; hali ya siasa na uchumi. Mbali na kupokea ripoti ya utendaji, huiagiza serikali itekeleza masuala fulani fulani kama vile ujenzi wa shule, kilimo, ufumbuzi wa umeme nk.


Mwaka 2006, NEC ilipoiagiza serikali itafute ufumbuzi wa umeme, serikali ikawaita mafisadi wachangamkie tenda hiyo. Hapo Mzee wa Monduli akaanza safari za Thailand kusaka mvua za kutengeneza. Baada ya watu kutoa maoni kupinga mradi huo, Ikulu ikabuni mazingira ya kukubalika kampuni ya kufua umeme ya Richmond.


Tulio nje hatujui kampuni hiyo ni ya nani lakini wenyewe wanaijua ndiyo maana wanahaha kuwasafisha watu wote wanaodaiwa kuipa kampuni hiyo mkataba wa kuvuna Sh 152milioni kutwa kwa miaka miwili.


Kwa kuwa NEC ndiyo iliiagiza serikali itafute kampuni na serikali ikafanya hivyo kwa kuwapa ulaji maswahiba wao ndani ya chama, mradi huo ulipokuja kubainika kuwa ni wa kifisadi, chama na Ikulu wanakuwa mbogo dhidi ya watu wote wanaoisakama kampuni hiyo.


Hivyo, kuendelea kudodosa wamiliki wa kampuni hiyo ina maana kukaribia kabisa kuwataja wamiliki wake waliomo ndani ya CC, NEC na Ikulu. Mwenyekiti wa chama ndiye pia kiongozi CC, NEC na serikali, kwa hiyo kile wanachokitetea anapokuwa kwenye chama ni dhahiri atakitetea akiwa Ikulu. Bila yeye hakijadiliwi kitu.


Kwa hiyo, kama mafisadi wako ndani ya chama, rais anawajua. Na inapotokea kuwa mafisadi hao ndani ya NEC ndio wenye ushawishi mkubwa juu ya nani hasa achaguliwe, katika fungamano hilo au utatu huo wa kifisadi hakuna mwenye uwezo wa kumnyoshea kidole mwingine.

Zaidi mafisadi ndio wanaonekana kukitumia chama na Ikulu kuwalinda. Nguvu hizi za mafisadi zimewafunga mdomo, macho na masikio kiasi kwamba wajumbe watiifu kwa mafisadi hawasikii cha mnadi swala wala mwadhini. Wamepoteza mwelekeo, sasa wabaya wao ni wanaowasakama mafisadi.


Mafisadi kwao ni msamiati mpya ukimaanisha watu wema na wazalendo kwa chama. Kwa CCM, fisadi si mtu mbaya; mtongozaji, mharibifu, mpotevu, mwasherati au mfitini na mgomvi, mtu huyo amepewa sifa za ujasiri na uzalendo.


Kwa hiyo, mtu yeyote atakayejitokeza kupambana na fisadi-mzalendo atakuwa anakifedhehesha chama. Kama huo ni mtazamo wa mwenyekiti wa chama, basi huo ni mtazamo wa Ikulu, hivyo sioni uwezekano wa kujitenga na mkakati ulioandaliwa kumsulubu Spika, Samuel Sitta.


Miaka ya nyuma hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alitufundisha kuwa ubeberu ni unyonyaji uliokomaa hadi kuvuka mipaka, lakini CCM inasema ubeberu haupo ila utandawazi; na unyonyaji haupo ila uwekezaji. Serikali inafuata kile bepari-mwekezaji anachotaka.


Watoto wetu Bunda wamefungwa miaka mitatu jela kwa madai ya kulisha ng’ombe kwenye pori la wanyama ambalo amepewa bepari. Japokuwa sheria zinazokataza kufungwa watoto kwenye jela za watu wazima zipo, inafanyika hivyo kwa vile CCM na serikali yake wanatumikia mabepari kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.


Kutokana na mwelekeo huo, adui namba wani wa CCM na Ikulu kwa sasa ni Spika anayeonekana kuruhusu mijadala mizito ya kupinga mafisadi wa Richmond, EPA pamoja na rais mstaafu kujimilikisha mgodi wa Kiwira na wengineo.


Mafisadi hawa wa sasa hawana tofauti na tuliowasikia miaka ya 1990. Tuliwasikia kina Chavda, mwarabu wa Loliondo na Kampuni ya Mohamed Enterprises kuingia mchele mbovu nchini. CCM na serikali walikingia kifua ufisadi ule.


Ufisadi wa Chavda ni sawa na wa EPA leo. Jamaa huyo alikopeshwa mamilioni ya pesa ya Mfuko wa Kununulia Madeni ya Nje (DCP) kwa ajili ya kufufua mashamba ya mkonge Tanga, lakini hakufanya hivyo. Suala la Loliondo ni sawa na suala la umilikishwaji wenye utata wa mgodi wa Kiwira leo ila tofauti ni rangi. Kashfa ya mchele mbovu ni sawa na Richmond.


Watu walioshupalia masuala hayo kama aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Lyatonga Mrema waligeuziwa kibao. Mrema alijengewa mazingira magumu ndani ya chama na serikali akaachia ngazi.


Kwa hiyo, mshikamano wa kifisadi ndani ya chama na serikali ndiyo kikwazo kikuu kwa wapambanaji dhidi ya ufisadi kwa miaka mingi. Mafisadi ndio wajumbe wa CC na NEC na ndio watoa maamuzi.

Mafisadi ndio wafadhili wakuu wa chama na ndio wenye ushawishi mkubwa kwa viongozi wa chama na serikali. Mafisadi wameushika pia umoja wa vijana.


Wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa viongozi wa UVCCM, ziliibuliwa tuhuma za ufisadi katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya la umoja huo, aliyeibua tuhuma hizo alitoswa kuwania uongozi na aliyeshupalia ni Katibu mkuu Yusuf Makamba. Ikaundwa kamati ya kuchunguza madai hayo huku ikijumuisha pia watuhumiwa ili kuua hoja.


Kwa hiyo, haishangazi leo kuona Makamba anatumika vilivyo kuua hoja ya ufisadi kama alivyoua hoja ya Nape Nnauye juu ya ufisadi katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya la umoja wa vijana. Kama CC na NEC imejaa mafisadi, ni dhahiri mabosi wao ni Katibu mkuu na rais/ mwenyekiti.


Kwa kutumia nadharia ya Pythagoras kama chama kimejaa mafisadi na wasemaji wakuu wa chama ni katibu mkuu na mwenyekiti ambaye pia ni rais, basi ni sahihi kusema CCM, na Ikulu wanatumikia mafisadi.


Vilevile, kwa kutumia nadharia hiyo ya Pythagoras, hatua ya kumshirikisha Rais mstaafu, Mzee Ruksa kwenye kamati ya kuchunguza uhusiano kati ya chama, serikali na Bunge ni sawa na kumwamini mtu aliyebariki ufisadi wa Loliondo, Chavda, mchele mbovu nk. Mzee Ruksa ni majeruhi wa Bunge. Aliyumbishwa katika suala la Tanganyika na OIC. Atasema nini? Kwenye kiti bungeni alikuwa Pius Msekwa aliyeruhusu mijadala ya kuikoroga serikali ya Mzee Ruksa. Sasa anakuwa hakimu wa Sitta? Majeruhi hawa watakuwa huru katika suala hili?

Hivi kuna hadidu za rejea ambazo CCM walimpatia Spika azifuate katika uendeshaji wa Bunge? Kama zipo, labda Mzee Ruksa atazifuata hadidu hizo ili kudhibiti viwango vya mijadala dhidi ya chama bungeni. Mbona yeye hakuingilia utendaji wa Msekwa? Hata tutashuhudia fungamano la kifisadi.
 
Back
Top Bottom