Ndege Unayetafutwa

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,809
Ndege Unayetafutwa


1. Ewe ulobahatika, ndege uliye hewani
Unopita ukiruka, na kuranda mitaani
Mwenzio ahangaika, aparamia mitini

Fanya urudi haraka, zikuone zake mboni

2. Fani yako memponza, memuathiri moyoni
Dunia kaimaliza, kwa wengine hulingani
Na sasa wamuumiza,'akutaka,hakuoni

Jaribu utavyoweza, ungie mwake tunduni

3. Fuadi kitanda chako, yeye kakutandikiya
Kifua ndicho tandiko, chake kakuzawadiya
Mwengine kwake hayuko, wewe mekusabiliya

Wafanya nini uliko?, hwendi ukamridhiya

4. Lau moja mevunjika, ya pili mbawa rukiya
Ano'itwa huitika, labeka huitikiya
Huwa hafanyi dhihaka, huenenda kisikiya

Nawe jihimu shituka, ushike wangu wasiya

5. Bahati mekugongeya, iko pako mlangoni
Sioni cha kungojeya, na kuchelewa njiani
Naona waichezeya, shilingi yako ******

Ikangia mepoteya, ndio basi huioni






Maher Fundi
 
Natamani ningekupa thanx mbili..At last kuna shairi..nimeyamiss haya!!!!
a few minutes tumjibu huyu ndege..!!!
 


Ndege unayetafutwa, sikiya weye sikia
Akusaka kucha kutwa, mwenziyo anyong'onyea
Ahisi kama asutwa, wakati akulilia!
Sikia ndege sikia, ujuwe unatafutwa!


Kile leo yu njiani, ki guu chake na njia
Achungulia mitini , na juu aangalia
Asema siyo utani, na tena kakuzimia
Sikia ndege sikia, usiingie mitini!


Ateta kwake ni soo, mwenyewe katuambia
Eshajulisha ukoo, na yote kaelezea
Asema waruka huyoo!, kwa macho akuonea
Sikia ndege sikia, umemkaba kwa koo!
 
Ewe ndege usikiye, kilio changu na miye
Upae na ufikiye, kuno aliko na yeye,
Uende umsikiye, alonalo akupeye,
Mbinde usimfanyiye, uyeye na upaiye!

Wende veve na uruke, na hima ufanye wewe,
Ulo nayo uyaleke, upae kama ndi mwewe,
Ya mtima upilike, yatoke kwake mwenyewe,
Mbinde usimfanyie, uyeye na upaiye!

Hofu isikuingiye, ya mtego kushikie,
Mikononi uingiye, chozi ukamfutie,
Moyo umtuliziye, furaha umpatie,
Mbinde usimfanyie, uyeye na upaiye.

Natama chini na miye, mwingine asisikiye,
Siyo ngoma ya ukae, ombi na likufikie,
Fanya mwendo ufikiye, na kwake ukatuliye,
Mbinde usimfanyie, uyeye na upaiye!

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
 
Ndege huwa ni wako, pale umfugapo
Katu ndege si wa kwako, pindi umuachapo,
Katu hakai kwako, utamchukua upepo
Kama ndege ni wa kwako, usimruhusu kuruka.

Bandani wamfungia, ale mashudu na pumba
Maji wamuwekea, mitaroni asijeyumba
Na dawa wampatia, pasi wadudu kumkumba,
Kama ndege ni wa kwako, usimruhusu kuruka

Na pindi akitoroka, watu watamuona
Na vile anavyowaka, mioyo itawabana
Na akili kuwaruka, ili wapate mbana
Kama ndege ni wa kwako, usimruhusu kuruka

Manati watatumia, mitego ulimbo pia
Mtama watamtupia, iwe njia kupatia
Pindi akifakamia, mikononi ataingia
kama ndege ni wa kwako, usimruhusu kuruka

Na pole nakupa pasta, ndegeyo kumpoteza
Si ajabu utampata, milango wakilegeza
Utamfugia kwenye kuta, kutoka hatapenyeza
Kama ndege ni wako kwako, usimruhusu kuruka
 
Nafahamu ndege wengi,Chokoriko , mbalarungi
Ndege hua hajitengi,Wataruka kwa makundi
Ni lazima yapo mengi,ya kumkimbiza bundi
Ndege haruki mwenye, pasi kuna sababu

Ukiona ameruka,Kwenda sehemu mbali
Na ujue mesituka,Hapo alipo si mali
Puresha itamshuka,Akibaki hana hali
Ndege haruki mwenye, pasi kuna sababu

We wenda zako kazini,Wamuacha kwenye tundu
Hujaaga kwa amani,Unamuona kirundu
Chakula cha uchoyoni, ndo wamrushia kwa tundu
Ndege haruki mwenye,pasi kuna sababu

Na ukirudi nyumbani, badala ucheze naye
Unakaa sebuleni, anabaki hohe haye
Chakula akitakani, wamhaidi keshoye
Ndege haruki mwenye, pasi kuna sababu
 
Ndege wewe tokea,
Toka ulikotokomea,
Yeye alokusotea,
Akwita, tokea.

Umeruka hata wapi,
Umekaa mti upi,
Nikutafute hata wapi,
Ama ni upande upi.

Wako uhuru kichakani,
Hata pia tunduni,
Wasubiriwa asilani,
Urudi mwako tunduni.

Ndege wewe ndege wewe,
Uso jamii ya mwewe,
Usipatwe na kiwewe,
Ukajilaumu wewe.

Nakuita kwa sauti,
Hadi kwenye makuti,
Hata katika miti,
Nitaipaza sauti.
 
Nia yangu ni kujua, kama ndege amerudi,
Moyo unanisumbua, mwili wapata baridi,
Na Pasta anaugua, moyo wake haudundi,
Kisa ni ndege wake, abaye ametoroka.

Jua lilipochomoza, mtandaoni kuingia,
Ili kupata mwangaza, ka ndege kamrudia,
Ili tupate chombeza, furaha ikimfikia,
Kisa ni ndege wake, ambaye ametoroka

Nikafungua jamvini, thredi nikatafuta
Toka juu mpaka chini, jibule sikulipata,
Nikajishika kichwani, na majonzi nikapata
Kisa ni ndege wake, ambaye ametoroka.

Sasa tufanye nini, Kumnusuru rafiki
Asiporudi tunduni, wazo halifikiriki
Pasta wetu maskini,asiipate mikiki,
Kisa ni ndege wake, ambaye ametoroka
 
well done washairi niko class najifunza haya mambo nikirudi hamnikamati ..kila siku nawatamania nyie mlobarikiwa ktk hii fani
 
well done washairi niko class najifunza haya mambo nikirudi hamnikamati ..kila siku nawatamania nyie mlobarikiwa ktk hii fani

mwana dada usijari,
zaidi ongeza ujasiri,
hutokuwa bahiri,
wa mawazo ya siri.

utaongeza umakini,
hutokuwa masikini,
wa lugha ya maskani,
kujipatia shukrani.

uwezo kujivunia,
wa lugha ya kitanzania,
na iwe yako nia,
tena bila kudhania.

utamu utajionea,
mzinga kujichongea,
ufanisi kujiongezea,
asante kujizolea.
 
well done washairi niko class najifunza haya mambo nikirudi hamnikamati ..kila siku nawatamania nyie mlobarikiwa ktk hii fani

Festi ledi nimeona, posti yako jamvini
Na umevipenda vina, na ujumbe utenzini,
Na sasa una nia, utenzi kuweka ndani,
Ushairi si mgumu, msamiati ni muhimu

Kazi yake ni rahisi, siri vina na mizani,
Mistari wainakisi, na kalamu mkononi
Kitu utakachohisi, utakiweka utenzini,
Ushairi si mgumu, msamiati ni muhimu

Likija wazo kichwani, chukua yako kalamu
Nane namba ya mizani, mistari ni muhimu,
Kupungua uhaini, kuighani ni vigumu
Ushairi si mgumu, msamiati muhimu,

Uviangalie na vina, kufanana ni lazima
Kama ya kwanza ni na, vifuatavyo kuzizima
Ni lazima kujibana, vina vipate fanana
Ushairi si mgumu, msamiati muhimu

Jaribu na beti moja, lenye vina vyake nane
Kukosea sio hoja, misitari iwe ninne
Tutausoma pamoja, na kuongeza mengine
Ushairi si mgumu, msamiati muhimu.
 
Haya ninaruka naja, uneleze ya moyoni
kisababishacho hoja, kuniita jukwaani
na uache kubwabwaja, ati naranda mitani
Ndege nimeshajileta, jieleze kiundani!

Nakubali mi mzuri, kamwe hupati popote
kuanzia adhuhuri, hadi mvi zikupate
taishia kusafiri, paka ukauke mate
Ndege nimeshajileta, jieleze kiundani!

Shidayo kubwa ni moja, leo nakutamkia
uko na mimi saa moja, saa tatu ni kwa Leah
nilichoka na vioja, mbali nikatimkia
Ndege nimeshajileta, jieleze kiundani!

Wala mbawa javunjika, ndo mana nimekufata
wito nimeitika, nenolo naona tata
muda wako wakatika, hujasema wachotaka
Ndege nimeshajileta, jieleze kiundani!

Bahati ni mimi kwako, ila umeichezea
nilikupenda kuliko, moyo ukanivunjia
mesikia yako heko, nikaja kukusikia
Ndege nimeshajileta, jieleze kiundani!

Onyo ninakupatia, uache wako uhuni
lasivyo watakimbia, unaowaita hani
uwanja wa fisi kimbia, utafute wa undani
Wosia nakuachia, la sivyo tabaki peke.
 
Vilio vyenu nimesikia, mie ndege nimetua
X-Paster mesikia, nenolo sikioni limetua
toka mbali mesikia, moyoni likanitua
ukungu najauondoa, nimerudi wako ndege

Choveki na Mwanakijiji, wito nimeuitika
Narudi kwangu kijiji, X-Paster kumwitika
Nimechoka na hili jiji, wito ninauitika
Kifuani kwako narejea, X-paster unipokee

Ngambo Ngali nimerudi, kwake X-Paster kifuani
Kurejea sina budi, nimpe raha siyo kifani
Anyisile obheli hodi, X-Paster wangu mwandani
Ndege mie narejea, kumwangukia mwandani

Compaq nawe Amani, niachieni wangu mwandani
mbona hamumpi amani, kumwandama wangu hani
hebu tulieni kwa amani, niko kwake kifuani
X-Paster wangu mpenzi, twende tukapumzike ndani.
 
Vilio vyenu nimesikia, mie ndege nimetua
X-Paster mesikia, nenolo sikioni limetua
toka mbali mesikia, moyoni likanitua
ukungu najauondoa, nimerudi wako ndege

Choveki na Mwanakijiji, wito nimeuitika
Narudi kwangu kijiji, X-Paster kumwitika
Nimechoka na hili jiji, wito ninauitika
Kifuani kwako narejea, X-paster unipokee

Ngambo Ngali nimerudi, kwake X-Paster kifuani
Kurejea sina budi, nimpe raha siyo kifani
Anyisile obheli hodi, X-Paster wangu mwandani
Ndege mie narejea, kumwangukia mwandani

Compaq nawe Amani, niachieni wangu mwandani
mbona hamumpi amani, kumwandama wangu hani
hebu tulieni kwa amani, niko kwake kifuani
X-Paster wangu mpenzi, twende tukapumzike ndani.

X-paster leo halali, kazi ni kuota tu
atashindwa kula wali, kwa mtoto wa kihutu
Mwanajami tafadhali, usinipige mtutu
mtunze kwa kila hali, pasta nimekuachia.
 
Furaha ya leo kesha, Umma nautangazia
Mazuri yangu Maisha, Ndege wangu karejea
Namfanyia Tamasha, Kucha Kutwa twaongea

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini

Tutapeana mapenzi, Dunia ipate jua
Kwa haki tamuenzi, Mwingine apati tua
Huyu Wangu la azizi, Moyo umepata poa

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini

Amerudi ametubu, Kama si yule wa jana
Penzi letu limesibu, Wapenzi tumekutana
Watu wanastaajabu, Jinsi tunavyo pendana

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini

Twakumbushana zamani, Penzi tulivyo peana
Mengi tulio tamani, Leo tunakumbushana
Mimi na wangu mwandani, Twakesha kibusiana

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini

Namaliza tano beti, Mbele sito endelea
Mpenzi avuta shati, Ndani nipate rejea
Nikampe sharubati, roho ipate kutua

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini
 
Furaha ya leo kesha, Umma nautangazia
Mazuri yangu Maisha, Ndege wangu karejea
Namfanyia Tamasha, Kucha Kutwa twaongea

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini

Tutapeana mapenzi, Dunia ipate jua
Kwa haki tamuenzi, Mwingine apati tua
Huyu Wangu la azizi, Moyo umepata poa

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini

Amerudi ametubu, Kama si yule wa jana
Penzi letu limesibu, Wapenzi tumekutana
Watu wanastaajabu, Jinsi tunavyo pendana

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini

Twakumbushana zamani, Penzi tulivyo peana
Mengi tulio tamani, Leo tunakumbushana
Mimi na wangu mwandani, Twakesha kibusiana

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini

Namaliza tano beti, Mbele sito endelea
Mpenzi avuta shati, Ndani nipate rejea
Nikampe sharubati, roho ipate kutua

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini

Kwanza pokea hongera, ndegeyo kwa kurudi,
Tutalichora duara, kutotoka hana budi,
Tutaomba mkandara, amlinde kwa juhudi,
Jamani tuhakikishe, ndege huyo katulia.

Mwanakijiji yako kazi, ushauri kuutoa,
Lazima uweke wazi, pasta kuzingatia,
Lasije kupita wezi, mpenziye kumkwapua,
Jamani tuhakikishe, ndege huyo katulia.

Compaq na obheli, jamani twawashukuru,
Amani choveka kweli, muda mliunusuru,
Kucheki kila mahali, mathias na msururu,
Hakika twawashukuru, kumliwaza Pasta.
Sasa ndege amerudi, nyumbani kuna amani.
 
X-Paster ni yako raha,
na ukae kwa madaha,
ujiongezee furaha,
kuiondoa karaha.

kifuani katulia,
tena hatoweza lia,
mazuri kusimulia,
ye akikupumulia,

utasahau machungu,
lipoita kwa uchungu,
na umshukuru Mungu,
kanusuru na mizungu.
 
Pasta nakupa hongera, kurudiwa wako ndege
siipati yako sura, ulivyokumbata kidege
ntoto wa tabora, huku mnameza mbege
Hongera tena nakupa, simwache aruke tena.

Kweli mshukuru Mungu, kwa ndege kurudisha
ama kweli si mzungu, wafaa andika insha
situmie tena rungu, kipande cha khanga tosha
Hongera tena nakupa, simwache aruke tena.
 
Tutapeana mapenzi, Dunia ipate jua
Kwa haki tamuenzi, Mwingine apati tua
Huyu Wangu la azizi, Moyo umepata poa

Mapenzi kweli matamu, Leo nimeyabaini


Uma mumetangaziwa, naye bwana Pasteri
Mwenyewe amerudiwa, na sasa ajivinjari
Ahisi mmeshajuwa, kishasema Pasteri
Ameaonya Pasteri, chumbani kajifungia!


Kajifungia chumbani, ajilia kuku wake
Msije enda nyumbani, esha onya huko kwake
Mtaishia langoni, akila kakuku kake
Eshaonya Pasteri, chumbani kajifungia!


Msimtake ubaya, na kwenda msalimia
Hatawaonea haya, mlango kutofungua
Mubaki mwagwaya gwaya, ka ndege akijilia!
Eshaonya Pasteri, chumbani kajifungia!

Choveki
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom