Ndege asiyetulia

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,476
39,995
Swali nawaulizeni, mabingwa wa kiswahili,
Wanazuoni jibuni, kwa kina kiso bahili,
Hoja zenu zipangeni, kwa vyema ilo ayali,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Ni ndege nimpendaye, kutwa yuko mawinguni,
Ndiye nimtafutaye, namsaka msituni,
Mtego niuandae, ninmase asilani,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Ala kulli hali, ndege nitamsifia,
Alhasir kauli, kwanini namsakia,
Naelezea amali, kwa jinsi namshakia,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Sekunde akishatua, fumba fumbua karuka,
Mtini akishatua, mbawaze zapeperuka,
Mtego keshagundua, adonoa kwa dhihaka,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Mtegoni hanasiki, machale yamemcheza,
Najiona mwenye dhiki, ndege nambembeleza,
Arijojo hashikikiki, wenzangu wananibeza,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Nilidhani nimenasa, kumbe amenizugia,
Kaniacha napepesa, ndege amenikimbia,
Wajuzi wenye kuasa, majibu nasubiria,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Na. M. M. Mwanakijiji
Sauti ya Kijiji
 
Mzee mwanakijiji,
Usichoke kujihoji,
Ahidi tanipa taji,
Jibu nikikupatia.

Ndege asotuliaga,
Nirahisi kumtega,
Na kisha ukamfuga,
Kibandani kutulia.

Hutegwa kwa tundu bovu,
Wala si kwa ndizimbivu,
Fanya kama mpumbavu,
Mkononi tamtia.

Exaud J. Makyao
 
Hategeki kwa urimbo, Wala kipande cha bati
Huyu mtungie wimbo, atalala katikati
Tena usitie fumbo, la mti wa katikati
Ndege asiyetulia, hutulizwa kwa gitaa!


Ni wimbo namna gani, wauliza asilani
Si wa lugha ya kigeni, aya zake teni teni
Muimbishe kinyumbani, ataingia kimyani
Ndenge asiyetulia, hutulizwa kwa gitaa!

Matejoo wa Kwetu
 
Huyo ni ndege mjanja, hunaswa na tundu bovu,
Kama walivyo wajanja, hukwama mali pabovu,
Hutegeshwa kwa ujanja, si kwa mbinu mbovumbovu.
Ndege asiye tulia, hunaswa na tundu bovu.

Na tundu bovu hunaswa, ndege asiye tulia
Umakini haswa haswa, na akili lo tulia,
Na ujipange ki haswa, ndipo atapotulia,
Ndege asiyetulia, hunaswa na tundu bovu.

Kwa ndani ya tundu bovu, ulipakae ulimbo,
Lonekane bovu bovu, na sio lenye urembo,
Lisijulishe ni bovu, na kumbe ni limtambo,
Ndege asiyetulia, hunaswa na tundu bovu.

Wewe tulia kwa mbali, watajileta mwenyewe,
Wa aina mbalimbali, watasogea wenyewe,
Na kutokea kwa mbali, utamuona mwenyewe,
Ndege asiye tulia, hunaswa na tundu bovu.

Tamati nimefikia, hapa ninamalizia,
Mtegoni kafikia, ndege kajimalizia,
Mwanakijiji sikia, usije jimalizia,
Ndege asiye tulia, hunaswa na tundu bovu.

By Pasco
 
Swali nawaulizeni, mabingwa wa kiswahili,
Wanazuoni jibuni, kwa kina kiso bahili,
Hoja zenu zipangeni, kwa vyema ilo ayali,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Ni ndege nimpendaye, kutwa yuko mawinguni,
Ndiye nimtafutaye, namsaka msituni,
Mtego niuandae, ninmase asilani,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Ala kulli hali, ndege nitamsifia,
Alhasir kauli, kwanini namsakia,
Naelezea amali, kwa jinsi namshakia,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Sekunde akishatua, fumba fumbua karuka,
Mtini akishatua, mbawaze zapeperuka,
Mtego keshagundua, adonoa kwa dhihaka,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Mtegoni hanasiki, machale yamemcheza,
Najiona mwenye dhiki, ndege nambembeleza,
Arijojo hashikikiki, wenzangu wananibeza,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Nilidhani nimenasa, kumbe amenizugia,
Kaniacha napepesa, ndege amenikimbia,
Wajuzi wenye kuasa, majibu nasubiria,
Ndege asiyetulia, huyo anategwa vipi?

Na. M. M. Mwanakijiji
Sauti ya Kijiji

Ni haka hapa




Kandege!.gif
 
Mzee mwanakijiji,
Hoja uliianika,
Kwa moyo ukatuhoji,
Msaada ukitaka,
NDEGE AMESHATEGEKA?

Ndege ulimuhitaji,
Kutulia hakutaka,
Hukujua utegaji,
Ushauri ukataka,
NDEGE AMESHATEGEKA?

MATEJOO msomaji,
Alijibu kwa hakika,
Kisha PASCO mtungaji,
Pembeni hakujiweka,
NDEGE AMESHATEGEKA?

SURA yule mchoraji,
Picha akaibandika,
MAKIYAO msemaji,
Sikuacha kuandika,
NDEGE AMESHATEGEKA?
 
Ndege niliyemtaka
Huyo ameshanasika
Mtego nilioweka,
Mwenyewe kajitundika!

Ndege nikamtambua
Si kwale wala si hua
Ni tetere nikajua
Hamu ikanizingua!

Kisu kikalamba shingo,
Nikamweka kwenye ungo
Kanyonyolewa kwa mpango,
Huku nikiweza tungo.

Ndipo nikamuandaa,
Na macho nimeyatoaa
Mate nikidururizaa
Na tumbo likingurumaa!

Ndipo nikambanika
Limao nimemfunika
Na chumvi ya kutosheka
Ndege wangu kaungika!

Nikamla!

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
 
Furaha imenijia,
Mwanakijiji sikia,
Ndege uliyelilia,
Mkononi kumtia.

Mbona huja tukumbuka,
Meza ulipoandika,
Walau tuje kucheka,
Huku tukiserebuka?

E. J. M
 
Hima hima wa kijiji, witowo nausikia
Nakinurisha kipaji, jamvini kwa kuingia
Eti ndege aso mji, ni vipi kumnasia?
Ndege asiyetulia, hutegwa kwa kutotegwa

Kamwe usitake inda, ya ndege asotulia
Kwa vile itakushinda, takuruka kama KIA
Kimya wende kama winda, kwa hila hutonyatia
Ndege asiyetulia, hutegwa kwa kutotegwa

Hutegwa kwa kutotegwa, ndege asiyetulia
Tunduni utambeba, bila ya kutarajia
Kijifanya kwa mijeba, takosa mzungukia
Ndege asiyetulia, hutegwa kwa kutotegwa

Mtego mtege panya, ndege kaustukia
Na yote takayo fanya, kwa mtama kubugia
Ndege atautapanya, hata chumba kurukia
Ndege asiyetulia, hutegwa kwa kutotegwa

Ndege mjanja huruka, mtego akiangia
Ndiyo yakwe hi hulka, kazaliwa nayo siha
Vipi wewe waanguka, kutaka mkumbatia?
Ndege asiyetulia, hutegwa kwa kutotegwa

Hutegwa kwa kutotegwa, wala kamba kutofungwa
Hapo ndipo tambeba, tia kapu kama chungwa
Kama wataka kuremba, au kumlisha punga
Ndege asiyetulia, hutegwa kwa kutotegwa

Ukimtega mtege, lakini atang'amua
Si kama kalewa mbege, hawezi kupambanua
Kwani yeye legelege, kama mabua ya muwa?
Ndege asiyetulia, hutegwa kwa kutotegwa

Ndege mwenda wa marifa, hunaswa na tundu bovu
Ndege mwenye kila sifa, hunaswa bila mapovu
Ndege wa kwenda kwa dhifa, hushikwa bila makovu
Ndege asiyetulia, hutegwa kwa kutotegwa

Kaditama nimefika, Edita kwa beti tisa
Ushauri kwa kushika, katika cha ndege kisa
Mshikadau wa fika, mwenye majununi hisa
Ndege asiyetulia, hutegwa kwa kutotegwa
 
Hategeki kwa urimbo, Wala kipande cha bati
Huyu mtungie wimbo, atalala katikati
Tena usitie fumbo, la mti wa katikati
Ndege asiyetulia, hutulizwa kwa gitaa!

Ni wimbo namna gani, wauliza asilani
Si wa lugha ya kigeni, aya zake teni teni
Muimbishe kinyumbani, ataingia kimyani
Ndenge asiyetulia, hutulizwa kwa gitaa!

......Matejoo wa Kwetu


Matejoo wachekesha, na mbavu zanivunjika
Ukiimba utakesha, kapa kapa utatoka
Ubaki wajikondesha, na ndege hata nasika
Wabantu hatuimbi, vimwana tunawabonga!

Ukimuona wabonga, kifundi na kistadi
Ikibidia wahonga, ukiongeza juhudi
Mgee hata kilonga, na vocha usiinadi
Wabantu hatuimbi, waachie bolywood!

Waachie Bolywudi, kuimba na kurembusha
kwa maneno huna budi, kinywani kuyazungusha
Kuimba siyo kwa jadi, nasema utachemsha!
Wamatumbi hawaimbi, waachie Boliwudi!
 
Hakika nimefurahi, kusikia umenena,
kabla Ya kukusabahi,kukupa yaliyo mema,
Ndege wako kumuwahi,hongera ninazituma.
nakupa nyingi pongezi,ndege huyo umtunze.


Dr Hamza Yousuf Al-Naamani
Doha
Qatar
 
Hakika nimefurahi, kusikia umenena,
kabla Ya kukusabahi,kukupa yaliyo mema,
Ndege wako kumuwahi,hongera ninazituma.
nakupa nyingi pongezi,ndege huyo umtunze.

Dr Hamza Yousuf Al-Naamani
Doha, Qatar
........
Ndege nikamtambua
Si kwale wala si hua
Ni tetere nikajua
Hamu ikanizingua!

Kisu kikalamba shingo,
Nikamweka kwenye ungo
Kanyonyolewa kwa mpango,
Huku nikiweza tungo.
......Nikamla!
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)

Barubaru kumbukia, ndegewe eshamchinja
Kwa kisu kakimbilia, halafu akamchinja
Busara hakutumia, wengine tukajikunja
Hakutumia ujanja, choveki nafikiria!

Mzee wakijijini, usije ukarudia
Ukimfuga tunduni, tetere hupendezea
Tetere nambari wani, nyumbani tunafugia
Hukutumia ujanja, choveki nafikiria!

Nawakumbusha vijana, papara mje zihepa
Ulizeni waungwana, mawazo kitapatapa
Tetere ndiye mwanana, si kuku wala si papa
Papara za kumuonja, choveki nafikiria
 
Barubaru kumbukia, ndegewe eshamchinja
Kwa kisu kakimbilia, halafu akamchinja
Busara hakutumia, wengine tukajikunja
Hakutumia ujanja, choveki nafikiria!


La haula l'haki,mash'kuur ya Choveki,
Jicho halikuhakiki, maneno kustahaki,
japo ningelibaini,nisingefanya hatiki,
mashkuura ya akhuy, mashkuura a jamiiya.


Dr Hamza.
Doha ,safarini Dar
 
La haula l'haki,mash'kuur ya Choveki,
Jicho halikuhakiki, maneno kustahaki,
japo ningelibaini,nisingefanya hatiki,
mashkuura ya akhuy, mashkuura a jamiiya.
Dr Hamza.
Doha ,safarini Dar

Twakumbushana mtani, kumbukia Barubaru
Hatucheki asilani, hata ukiwa ngumbaru
Hatuna huo uhuni, twapatiana uhuru
Akhsante, shukuru, lafudhi zetu za pwani!
 
Wakijiji umchoyo, kwa walokutegea ndege
kutuita shereheni, ilikuwa shida gani,
amaje tuambie, kama kweli limnasa,
sijekuwa watuteka, na bado wajililia!
...au...
ndege kweli limnasa, kitoweo ukaweka,
lakini lipopata, hukufuata sharia,
kuosha yako mikono, kuhalalisha chakula,
ukamla vivyohivyo, bila kufuata mila!
..nadhani umenipata!!?
 
Back
Top Bottom