NCCR - Wake wa marais wasianzishe taasisi Ikulu

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,009
Naam maana zinatumika kufanyia ufisadi.

NCCR - Wake wa marais wasianzishe taasisi Ikulu

na Salehe Mohamed
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimewataka wake wa marais waache kufanya biashara wakiwa Ikulu kwa kisingizio cha kuanzisha taasisi za kuwasaidia wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, Kampeni na Uchaguzi, Faustine Sungura, alisema taasisi hizo zinawanufaisha zaidi wanawake wa marais badala ya walengwa.

Alisema hiyo ni mbinu ya kuitumia Ikulu kufanya biashara, kwani kama kweli taasisi hizo zingeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wanawake, kusingekuwa na taasisi mpya kila anapoingia mke wa rais mpya.

Alisema Mfuko wa Fursa Sawa kwa wote (EOTF), ulio chini ya Mama Anna Mkapa, mke wa rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa hivi sasa umegeuka kuwa mali ya mtu binafsi, jambo ambalo kimsingi halikupaswa kuwa hivyo.

Alisema hata mke wa Rais Jakaya Kikwete naye kaanzisha mfuko wake ujulikanao kama WAMA, nao atalazimika kuondoka nao pindi Rais Kikwete atakapomaliza muda wake wa kuongoza.

“Sisi haturidhiki na matumizi ya mifuko au taasisi inayoanzishwa na marais wetu kwani inaonekana ni ujanja wa kufanya biashara kwa kutumia mwamvuli wa Ikulu,” alisema Sungura.

Alisema uanzishwaji wa mifuko hiyo ni dalili za marais kukwepa kulaumiwa kufanya biashara wakiwa Ikulu hivyo kuwatumia wake zao kufanya biashara.

Aidha, alisema kufanya biashara huko kunasababisha migongano mbalimbali kwenye uongozi, jambo linalochangia kuzorota kwa maendeleo yaliyokusudiwa.

Alisema ni vema kuanzia sasa mifuko hiyo ikawa ya kudumu na ikaendelezwa na kila mke wa rais anayekuja badala ya utaratibu wa hivi sasa ambapo kila mke wa rais huanzisha taasisi yake na kuondoka nayo, mume wake anapomaliza muda wa kuongoza nchi.

Kauli hiyo ya NCCR-Mageuzi imekuja siku chache baada ya Mbunge wa Mbozi (CCM), Godfrey Zambi, kutamka bungeni kuwa EOTF ni miongoni mwa mifuko inayowatapeli walimu katika Wilaya ya Mbozi kupitia Kampuni ya Bayport ambayo EOTF ina hisa.
 
Date::7/21/2008
NCCR- Mageuzi wawaandama wake za marais
Na Tausi Mbowe
Mwananchi

CHAMA Cha NCCR- Mageuzi, kimepinga hatua ya wake wa marais (first lady), kujihusisha na biashara au shughuli zozote zinazoweza kuwaingizia kipato wakiwa Ikulu wakati waume zao wakiwa katika madaraka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Kampeni na Uchaguzi ya chama hicho, Faustine Sungura, alisema wake wa marais wabaki kuwa hudumia waume zao na wasipewe mifuko yoyote ya maendeleo kuiendeleza kwa kuwa wamekuwa wakitumia mifuko hiyo kwa maslahi yao binafsi.

Sungura alisema wake hao wamekuwa wakaitumia fursa hiyo kufanya mambo yao kwa maslahi yao binafsi kwa kisingizio cha maslahi ya taifa na kutoa mfano wa mke wa Rais Mkapa aliyekuwa Mwenyekiti wa IOTF ambaye anakabiliwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi ikiwemo ya kuwaibia walimu, lakini baada ya kuondoka tu akaja mama Salma Kikwete na mfuko wake wa Wanawake na Maendeleo (WAMA).

Hii ni mifuko hewa inachangia pesa kuliwa, hawa wake za Marais wamekuwa wakianzisha mifuko hiyo kwa kisingizio cha kutetea maslahi ya wanawake, kumbe wamekuwa wakijihalalishia kula pesa kwa maslahi yao binafsi,?alisema Sungura.

Katika hatua nyingine chama hicho kimepinga hatua ya serikali kutumia vibaya rasilimali za nchi kwa kufanya ziara kila kukicha huku wananchi wakizidi kuwa na hali ngumu.

Sungura alisema kwa sasa Rais Kikwete yupo ziarani mkoani Tanga, na kwamba katika ziara hiyo amekuwa akitumia gharama kubwa wakati wananchi wanahitaji kutatuliwa matatizo yao akitoa mfano wa wazee wa iliokuwa wakifanya kazi katika Jumuhiya ya Afrika Mashariki ambao hivi karibuni waliandamana hadi Ikulu na Rais aliwaacha na kuanza ziara yake hiyo mkoani Tanga.

Wakati huo huo Sungura alielezea hatua ya Mamalaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), kupandisha nauli ya mabasi nchini kuwa ni matokeo ya uongozi mbovu wa serikali na kushindwa kuboresha maisha kwa wananchi wake.

Sungura alisema hiyo ni dalili kuwa serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuongoza dola kwa kuwa imeonyesha dhahiri kuwa imeshindwa kutetea maslahi ya wananchi wake licha ya kuendeleza falsafa zake za kuboresha maisha kwa kila Mtanzania lakini ukweli ni kwamba maisha ya wananchi yamezidi kudidimia siku hadi siku.

Mapema wiki iliyopita Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Israel Sekilasa, alitangaza ongezeko la nauli kwa wastani wa asilimia 20 kunzia Agosti mosi mwaka huu.
 
Back
Top Bottom