Nasikitika hadumu...

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,810


1
Ujana kitu kitamu, tena ni azizi sana
Maungoni mwangu humu, nilikuwa nao jana
Kwa wingi katika damu, tahamaki leo sina!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

2
Kichwa kimejaa mvi, kinywani meno hamna
Nikenda kama mlevi, miguu nguvu haina
Kumbe ujana ni hivi, ukenda hauji tena!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

3
Jua langu limekuchwa, na nyota nilizoona
Ukinitizama kichwa, nywele nyeusi hakina
Kama zilizofikichwa, zikang'olewa mashina
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

4
Natatizika kauli, midomo najitafuna
Nimekusanya adili, walakini hali sina
Dunia kitu bahili, hiki una kile huna!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

5
Nilikuwa ni waridi, furaha ya wasichana
Neno hawakunirudi, wakati wa kukutana
Sasa nanuka baridi, wanionapo waguna
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

6
Walio wakinibusu, walikuwa wengi sana
Wanawake wenye busu, uzuri na usichana
Sasa sina hata nusu, ya wanitajao jina
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

7
Wazuri wenye uturi, na mikono yenye hina
Kila mtu mashuhuri, alipenda kuniona
Nilifaa kwa shauri, na sasa sauti sina
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

8
Dunia bibi arusi, kwa watu kila namna
Inapendeza nafsi, wakati wa kuiona
Na leo sina nafasi, kwa uzee kunibana
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

9
Kilichokuwa gizani, niliweza kukiona
Nikakijua thamani, sura yake hata jina
Sasa sijui ni nini, hata ikiwa mchana
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

10
Kilichotaka fikira, niliweza kukinena
Kwa mfano na kwa sura, mpaka kikafanana
Leo tazama hasara, nguvu hiyo sina tena
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

11
Kilichotaka mapimo, sikifahamu mapana
Marefu yake na kimo, siifahamu bayana
Nusu nimo nusu simo, duniani najiona
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

12
Hadumu nasikitika, rafiki yangu ujana
Machozi yamiminika, na la kutenda hapana
Ni wakati umefika, uzee dawa hauna
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

13
Hauna dawa uzee, mabega yamepetana
Anionaye ni"wee!, ondoka hapa laana"
Wanaposema na miye, niliyekuwa na jina!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

14
Wakatabahu shairi, uchungu wanitafuna
Walakini nafikiri, twafuata Subuhana
Katika ile amri, ya"kuwa"na "kutengana"
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana




By Shaaban Robert
 
Du...Mkuu umeweka ukweli mno...Inatisha!

Waja kwa utaratibu, waja kwa kukunyatia
Huwezi kuuratibu, hilo neno zingatia
Hata uwe muhasibu, mapesa kuukatia
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana
 
1.
usililie ujana, uzee pia fahari,
ujana una hiyana, uzee hautakabari,
japo upakwe hina, bila sahau uturi,
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo

2'
uzee marhamu ya moyo, wengi wanigunia,
kama ningesifia choyo, wangekuja wa kununia,
sasa nimegusa mioyo, waamka kunikimbia
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo.

3.
nilogusa ni uzee, sambamba nayo hekima,
hiyo walonayo wazee, kijana kwake kisima,
akiruhusu hiyo imee, daima ataichuma
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo

4.
kama kuna asojua, mzee atamjuza,
asipojifanya kujua, aende kwake ajuza
huyo ataikunjua, akiliye na kuijuza,
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo.

5.
mi natamani uzee, ujana niukimbie,
hakima niizoee, upofu niuambae,
tena nisiyachezee, maisha kama kigae,
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo

6.
hakika haya yatosha, kwako upende uzee,
ujana usipokutosha, ni vyema usikemee,
bali uende jiosha, shomo lisikuenee,
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo
 
paster na mgombea, yote mmesema kweli,
nashindwa na kuongea, kati ya yenu mawili,
ujana mi naujua, uzee sifagilii,
kati ya yenu mawili, utoto ndo mambo yote!

Ujana maji ya moto, ingawa sharti kuoga,
mambo yake ya mpito, ila huwa yananoga,
utapitia kokoto, unapotafuta mboga,
kati ya yenu mawili, utoto ndo mambo yote!

Mgombea wewe tena, uzee wang'ang'ania,
hujashindwa kujikuna, na fimbo kutembelea,
mbele kashindwa ona, mke kuhudumia,
kati ya yenu mawili, utoto ndo mambo yote!

acheni yangu nitoe, maoni ya utotoni,
mgongoni nisitembee, maziwa mimi nipeni,
utotoni kweupe pee, mkiweza nirudisheni,
kati ya yenu mawili, utoto ndo mambo yote!

nitakacho mimi napewa, nikilia wanaogopa,
siwezi kuula muwa, v'tamu zaidi wanipa,
kijana sitaki kuwa, uzee nataka hepa,
kati ya yenu mawili, utoto ndo mambo yote!

Nawakilisha..
 
1.
Ebi wataka utoto, kama si lana ni nini,
Sasa waukana moto, japo wapenda hereni,
Navyo vile vyenye joto, daima vi maanani,
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo

2.
hekima uiheshimu, mzee wako sawia,
utoto uondoe hamu, ujana kutokawia,
uzee usione pumu, bali uanze lilia
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo

3.
utoto kama ujana, ndivyo vya kuanzishia,
uzee kama hazina, ndio wa kumalizia,
ukongwe ndio huvuna, yote yote ya dunia,
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo

4.
ujana utagombana, utoto utadekea,
wapenzi mkishibana, wazee mtaendea,
mikono mkishikana, wazazi taangulia,
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo

5.
kwa baba tasema ndiyo, kwa mama mtazizima
babu mtakuna nyayo, bibi mtapata sima
ndoa iwe ya moyo, tena ile ya daima
ujana maji ya moto, uzee marhamu ya moyo
 
na huku umejileta, porojo kutupatia,
sijakunyima kuteta, uzee kuusifia,
ni kama umeshapita, machungu kujionea,
uzee ama ujana, bora utoto jamani!

ndo kwanza umeingia, uzee wausifia,
utaposhindwa jongea, hekima takukimbia,
sije tulalamikia, wahenga hakukwambia,
uzee ama ujana, bora utoto jamani!

shidaze metafakari, ama umekurupuka,
uzee na zake shari, utoto heri hakika,
ujana bila ya gari, utoto umetukuka,
uzee ama ujana, bora utoto jamani!
 
1.
Abi umeaibisha, utoto kuutetea,
Heri ufunge dirisha, macho yasijeng’amua
Hasira wazipaisha, uzee kuukamua,
Utoto ujana pisha, uzee ndio hudumu

2.
Nasema njoo uzee, hima usikawie,
Hekima itujongee, werevu sasa umee,
weledi tutembelee, hata kwayo harambee,
Utoto ujana pisha, uzee ndio hudumu.

3.
Utoto jaa la deko, ujana jaa la pepo,
Yote yana vituko, warevu wala haupo,
hata pasipo na meko, wataka lishwa upepo,
Utoto ujana pisha, uzee ndio hudumu.

4.
Utoto nao ujana, yote yote yatapita,
Uzee siyo hiyana, hivyo sio wa kupita,
Hata kama utabana, peke waweza kufuta
Utoto ujana pisha, uzee ndio hudumu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom