Nani anasema ukweli kuhusu mgomo wa madaktari: serikali au wahusika wenyewe?

Magobe T

JF-Expert Member
Mar 19, 2008
4,620
2,567
Ndugu wanaJF, leo wakati wa Kipindi cha Patapata kinachorushwa na Wapo Radio kuanzia saa 1:15 asubuhi nimemsikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick akiwataarifu wananchi kuwa huduma za afya kwenye hospitali za umma zilizokuwa zimesimama zimerudia hali yake ya kawaida baada ya mgomo kuwa umesitishwa na madaktari wanafanya kazi kama kawaida.

"Madaktari wamerejea kazini na huduma zinaendelea kama kawaida," alisema. Alipoulizwa kuhusu tetesi kuwa madaktari wanasema hawajasitisha mgomo alisema wao (serikali) ndio wanaopata habari kutoka vyanzo vya uhakika na mengine yanayosemwa ni upotoshaji huku akiendelea kusisitiza wagonjwa waendee kwenda hospitali kutibiwa kama kawaida. Alisema huduma zimerudia kwenye hali yake ya kawaida kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili na zile za manispaa – Temeke, Amana na Mwananyamala.

Alipoulizwa kama mgomo umeleta athari zozote - mfano vifo, alisema hakuna na kama kumetokea vifo ni hali ambayo haiwezi kuepeukika maana hata kama hakuna mgomo wagonjwa na hata wasio wagonjwa wanakufa. Kuhusu upatikanaji wa dawa na vitendea kazi alisema vyote viko sawa ila yaliyobaki ni matatizo madogomadogo ambayo hayakosikani mahali popote.
Wapo Radio waliongea pia na Katibu wa Chama cha Madaktari Dr Edwin Chitage ili kujua kama wamesitisha mgomo lakini yeye alidai mgomo wao bado uko palepale ingawa kuna baadhi ya madaktari ambao wako kwenye mafunzo chini ya uangalizi wa daktari (interns) baada ya serikali kuwatishia kuwafukuza kazi wameamua kurudi kazini kwa utashi wa mtu binafsi lakini si wote wamerudi.

Alisema kuwepo kwa mgomo kulifanyika baada ya madaktari kufanya kikao na kuazimia kugoma na ili kurudi kazini lazima pia warudi baada ya kikao maana huo ndio utaratibu. Alidai yeye hawezi kusema kitu tofauti na uamuzi wa kikao cha madaktari maana hana mamlaka ya kusema tofauti na uamuzi wa kikao chao.
Alisema kumlazimisha daktari kufanya kazi wakati serikali bado ina mgogoro naye si sahihi maana hakuna daktari yoyote anayeweza kufanya kazi kwa vile amelezimishwa au kujituma kufanya kazi kwa kulazimishwa wakati anajua kuwa haki zake zinaendelea kuvunjwa.Baada ya kusikia kauli mbili zinazopingana, nikachanganyikiwa na kujiuliza: nani anayesema ukweli kuhusu kurejea kwa huduma za afya (kusitisha mgomo)?

Utaratibu huu wa serikali kucheza na maisha ya Watanzania kutaendelea hadi lini? Inasikitisha na kwa upande mwingine ngoja matatizo kama haya yaendelee kututafuna maana ni sisi wenyewe tunaochagua viongozi wabovu si kwa kuangalia sifa zao za uongozi bali uwezo wao kifedha (mazingira ya rushwa) labda baadaye tutapata akili na kuanza kuchagua viongozi kwa kutumia akili.
 
Back
Top Bottom