Nani anaelekeza taifa hili kwenye maangamizi haya?

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,082
katuni%20juni%2028.jpg

Maoni ya Katuni


Mgomo wa madaktari umeingia katika sura mpya na mbaya zaidi. Hali hii inajidhihirisha katika mkanganyiko mkubwa ambao hakika hauna maelezo ya kuweka bayana ni nini hasa kinaendelea.

Wakati leo ni siku ya saba tangu mgomo huu uanze Jumamosi iliyopita licha ya kuweko kwa amri ya mahakama ya kuusitisha, hali imezidi kuwa ya kizungumkuti mno.


Leo Serikali imesema kuwa itatoa tamko ndani ya Bunge juu ya mgomo huu. Ahadi hii ilitolewa jana na Waziri Mkuu bungeni baada ya kuibuka hoja kutoka kwa Mbunge wa Mbozi Magharibi (CCM), Geoffrey Zambi juu ya hali ya wagonjwa kuendelea kutaabika huku serikali na madakrati wakiendelea kuvutana.


Kwa hakika huduma za kitabibu katika hospitali kuu nchini, hasa zinazomilikiwa na serikali imedorora sana, hali ya huduma siyo nzuri Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), hospitali ya rufaa ya KCMC, Bugando, Hospitali ya Rufaa Mbeya na hospitali kadhaa za mikoa na za maeneo mbalimbali nchini. Kwa kifupi hali ni mbaya.


Mvutano huu wa serikali na madaktari ulilipuka mapema mwaka huu, hali iliyosababisha mgomo uliotanda kwa takribani mwezi mmoja, kati ya Januari na Februari.


Serikali iliingilia kati kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupeleka madaktari wa jeshi pale Muhimbili kuokoa jahazi, lakini baadaye hali ilikuwa mbaya zaidi mwishowe serikali na madaktari wakaamua kukaa meza moja na kupatana jinsi ya kutatua madai ya madaktari yaliyokuwa yamesababisha mvutano na hatimaye mgomo.


Kwa mujibu wa habari kutoka pande zote, yaani serikalini na kwa madaktari, mwafaka wa mazungumzo haujafikiwa kwa kipindi chote cha mazungumzo, na hivyo kuwasukuma madaktari katika mgomo mwingine ndani ya kipindi cha miezi minne tu. Ni shida, usumbufu na

masikitiko ya kila aina kwa hali hii kutokea tena nchini tena katika kipindi kifupi sana.

Wakati hali hii ikiendelea kuwa tete hivyo, jana habari za kusikitisha zimeibuka kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madakati katika kadhia yote hii tangu Januari/Februari, Dk. Stephen Ulimboka, ametekwa nyara na watu wasiojulikana, akapigwa na kwa kweli ameumizwa sana.

Habari hizi zilienea kama moto wa nyika na habari za kipolisi zinasema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, ingawa hakuna
aliyetiwa mikononi mwa dola hadi sasa kuhusiana na kadhia hiyo.


Tunasikitika kwamba mkanganyiko huu unatokea katika kipindi kigumu kama hiki cha mgomo wa madaktari, kwamba kiongozi wa mgomo husika ametekwa na kuponea tundu la sindano kuuawa kwa kipigo, na waliohusika hawajulikani. Ni masikitiko na ni jambo baya sana.


Ukitafakari kwa kina sana hali hii inaibua hisia mbaya na shuku mbaya kwamba taifa letu sasa linaelekea kubaya.

Pamoja na ukweli kwamba hatuungi mkono madaktari kugoma kwa sababu ya ukweli halisi wa nafasi yao katika kuokoa maisha ya

wanadamu wanaosumbuliwa na maradhi mbalimbali na tukiwa wakati wote tunalalamika na kuiasa serikali itafute suluhu ya madai ya madaktari, lakini pia hatuwezi pia kuunga mkono matukio ya kuteka watu na kuwapiga kwa nia yoyote ile, iwe kuwakomesha au kutaka kukatisha maisha yao au kuwatisha madaktari ili waache mgomo.


Kwa hali hii, tunasikitika kwamba tukio hili baya la kutekwa kwa Dk. Ulimboka na kujeruhiwa kiasi hiki limetokea wakati tukiwa katika mtanziko mkubwa wa mgomo wa madaktari, hali hii inafanya serikali kutazamwe kwa jicho baya na jamii hata kama mpaka sasa hakuna ushahidi wowote wa kuhusika kwake katika uhalifu huu dhidi ya raia wake.


Ni kwa kutambua ukweli huu tunaitaka serikali ichukue hatua za haraka kujisafisha dhidi ya hisia hizi kwa kusimamia uchunguzi madhubuti ili kujua ni nani hasa alihusika katika kumteka nyara Dk. Ulimboka, kumpiga na kisha kwenda kumtupa porini bila hata kumpora chochote?


Tunajua serikali imejiweka mbali na kuhusika kwake, lakini katika mazingira ya tukio la hili hali inakuwa ngumu na ya mchanganyiko sana.


Tunajua kila raia wa nchi hii ana uhuru wa kufanya atakalo, kwenda atakako, endapo kwa sababu yoyote ile ya kizembe, ya bahati mbaya au ya kujitakia tu atavunja sheria yoyote ile, basi mahali pekee pa kupelekwa ni mahakamani.


Taifa hili haliwezi kuruhusiwa kuendekeza na kulea tabia ya vikundi vya kihuni, vya kupanga au kutumwa kuwafanyia wengine uhalifu kama huu aliofanyiwa Dk. Ulimboka.


Kwa hakika hata hawa wanaotumwa kutekeleza ushenzi huu wajue tu damu wanazomwaga zitakuwa juu ya vichwa vyao na vizazi vyao, haijalishi ni kwa kutii nguvu gani, za giza au vinginevyo.

unasikitika kwamba tunaelekea kubaya kama taifa, tunataka kuona uwajibikaji katika hili.

CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom