Nakumbuka siku za mwanzo za utawala wa JK

JoJiPoJi

JF-Expert Member
Aug 8, 2009
2,907
3,261



blank.gif


Hii ilikuwa th. 8 June 2006


RAIS Jakaya Kikwete amesema nchi haitaongozwa kwa matakwa ya watu wenye madaraka, wenye nguvu au wenye umaarufu katika jamii.
Amesema serikali yake itahakikisha hakuna mtu anayekuwa juu ya sheria na haki za msingi za raia.Rais Kikwete alisema hayo jana mjini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Kikristu Tanzania .
"Tutajitahidi kuhakikisha kuwa nchi inaendeshwa kwa utaratibu wa sheria, na siyo matakwa ya wenye madaraka au wenye nguvu au watu maarufu katika jamii.
"Tunataka kuona kuwa hakuna mtu anayekuwa juu ya sheria. Pia, tutahakikisha kuwa haki za msingi za raia zinaheshimiwa. Moja ya haki hiyo ni haki ya kuabudu.
"Kuwepo na kuheshimiwa kwa haki hiyo kumesaidia nchi kuwa tulivu. Tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha haki hiyo haichezewi.
"Kadhalika, tutaendelea kuhimiza uhusiano mzuri baina ya dini zote, madhehebu yote na waumini wao. Ninaomba ushirikiano wenu na msaada wenu," alisema Rais Kikwete.
Kuhusu rushwa, alisema serikali yake inaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya adui huyo, hasa miongoni mwa watumishi wa umma.
"Nimetumia miezi kadhaa kuwahimiza na kuwakumbusha watumishi wa umma kuheshimu maadili ya kazi zao, wasiwe wavivu na wasiombe wala kupokea rushwa.
"PCB nimewaagiza waendeshe mkakati kabambe wa kupambana na rushwa bila woga, wasikubali kutishwa na mtu yeyote kwani mimi sitafanya hivyo na katika vita hiyo nimewaahidi kuwapa msaada wa aina yoyote wanaouhitaji.
"Kanisa halina budi kushirikiana na serikali katika kupiga vita rushwa, dhuluma na uonevu, uwe unafanywa na serikali, watu binafsi au vikundi mbalimbali," alisema.
Akizungumzia Umoja wa Kitaifa, Rais Kikwete alisema serikali ya awamu ya nne imeamua kutoa kipaumbele kwenye suala hilo kwa kutambua kuwa ndiyo nguzo ya taifa.
"Natambua uzito wa kuendeleza umoja nchini, kwanza ni taifa linalotokana na nchi mbili huru, sasa tumekubaliana kuwa njia ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu katika umoja wa nchi mbili, ni kuyazungumza kwa uwazi ndani ya mifumo na taratibu tulizojiwekea.
"Ugumu wa pili kuendeleza umoja nchini unatokana na hali halisi ya watu wa nchi yetu ambao wako makabila 120 yanayotofautiana kwa mambo mbalimbali ikiwemo lugha, mila na desturi na ni watu wa rangi na dini mbalimbali.
"Pia, watu wa siku hizi wanatofautiana hata kwa viwango vya maendeleo na mapato kiasi cha kuanza kuibuka matabaka katika jamii.
"Pamoja na ugumu unaoonekana, kazi ya kujenga umoja imepunguzwa makali na kazi iliyofanywa na Rais wa Kwanza , Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wetu wa pili Mzee Ali Hassan mwinyi na Rais wetu wa tatu, Mzee Benjamin Mkapa.
"Nami nimekusudia kufuata nyayo zao ili umoja wetu uzidi kudumu," alisema Rais Kikwete.
Alisema migogoro inayosababisha watu kugawanyika, husababishwa na viongozi wa siasa mabarakara au viongozi wa dini wenye mtazamo usioona mbali, ambao hudhani kuwa anayestahili kuthaminiwa na kupewa fadhila ni wa dini yao .
Kuhusu ukuaji wa uchumi, alisema serikali yake inajitahidi kuongeza mapato ya serikali na kusimamia vizuri matumizi ya serikali.
Alisema serikali inaendelea kutafuta marafiki nchi za nje na katika mashirika ya kimataifa ili kusadia jitihada za serikali.
Akizungumzia ushirikiano wa serikali na kanisa, Rais Kikwete alisema ili serikali ifanikiwe katika azma yake ya kutokomeza umaskini, ushirikiano wa makanisa na misikiti ni muhimu.
Alitoa mwito kwa viongozi wote wa dini kuendeleza kasi ya kuwafanya Watanzania wawe wazalendo kwa taifa lao.
Alisema viongozi na waumini wana jukumu kubwa la msingi katika mapambano dhidi ya umasikini.
Rais Kikwete alisisitiza uadilifu na maadili katika jamii, akisema madhehebu yana haki na wajibu wa kuijenga jamii yenye maadili.
Pia alisisitiza umuhimu wa madhehebu mbalimbali ya dini kuendelea na dhima yake ya kutoa huduma za kijamii, ikiwamo elimu.
 
Back
Top Bottom