Nahisi mikono yangu imelowa damu!

vukani

JF-Expert Member
Dec 30, 2009
245
165
Ni kweli mikono yangu imeloa damu. Nahisi damu ya dhuluma, tena dhuluma ya uhai wa kiumbe ambacho kilihitaji kuishi. Aaah! Moyo unaniuma sana lakini walisema Wahenga kuwa maji yakimwagika katu hayazoleki na pia majuto ni mjukuu. Sisi ni binadamu, kuna matukio ambayo hututokea na kamwe hatuwezi kuyasahau kutokana na kuguswa na matukio hayo hasa unapogundua kwamba wewe ndiwe chanzo cha hayo yote.

Je wewe unayesoma hapa hujawahi kumwaga damu? Je mikono yako haijaloa damu? Kama jawabu lako ni hapana basi utakuwa unajidanganya, kwani ukweli ni kwamba umeshwahi kumwaga damu, labda tu ujitie hamnazo ila ukweli umeshawahi kumwaga damu. Ni tukio ambalo siwezi kulisahau. Daima naliwaza,katu halitoki. Nakumbuka ilikuwa mwaka 1995, tukio lilijiri. Tukio ambalo lilinitokea kwa bahati mbaya sana, yaani sikulitarajia. Ilikuwa ni majira ya jioni nilikuwa nimekaa sebuleni na mama tukiangalia runinga.

Mara mama akaniambia niende jikoni kuandaa chakula cha usiku. Nilipoingia jikoni nikakuta paka ameinamia chunguni, huku anakula mboga, katika hali isiyotarajiwa nilijikuta nanyanyua kiji-mchi cha kutwangia viungo na kumpiga kichwani. Yule paka alikimbia mithiri ya mbio za nyika, huku akiyumba na kuingia katika bustani ya Maua. Wala sikuhangaika kumfuatilia, niliosha ule mchi na kuendelea na shughuli zangu za mapishi. Siku iliyofuata, ilikuwa asubuhi nikawa namwagilia maua maji ndipo nilipomkuta yule paka akiwa amekufa pale bustanini.

Nilishtuka sana, woga ulinijaa,f adhaa ikanitawala, nikahisi ni luya ya saba. Nilitazama mara nyingine ili kuthibitisha. Hakika ilikuwa kweli ingawaje sikutarajia kuwa pigo lile moja tena dhaifu kutoka kwa mwanamke, kama lingemtoa uhai Paka yule! Niliingiwa na hofu mara nyingine, kwani kuna simulizi nyingi kuhusiana na huyu mnyama Paka kuhusishwa na ushirikina. Imani hizi siyo haba, na zingine zimejengeka kuwa Paka anazo roho saba, sasa iweje afe kwa pigo dhaifu kama lile. Nilihisi mikono yangu kuloa damu, kwani kula vile vipande kadhaa vya samaki, sidhani kama alistahili adhabu ya kifo.

Naam, hilo limeshatokea na sina uwezo wa kumrejeshea uhai wake Paka yule ambaye daima nilimpenda. Naomba niweke wazi kuwa miongoni mwetu kuna idadi ya kutosha ya watu ambao wameshawahi kumwaga damu, iwe kwa kukusudia au bahati mbaya kama mimi. Hivi ni watu wangapi ambao wanaweza kusimama na kudai kuwa hawajawahi kusababisha kifo hata cha mnyama? Itakuwa ni unafiki kukanusha, lakini hebu nirejee kwenye uhalisia, hebu tuangalie kauli zetu, maamuzi yetu na kazi zetu, Je hakuna uwezekano ikatokea kusababisha vifo, iwe ni kwa wanyama au binadamu? Nitakupa mfano, Polisi akimhoji mtuhumiwa kwa mateso ili akiri kosa halafu ikatokea mtuhumiwa yule akafariki, je mikono yake haijaloa damu? Je daktari anapompa mgonjwa dawa isiyo sahihi akapoteza maisha au anapotoa mimba, Je mikono ya daktari huyo haijaloa damu. Viongozi wanapopitisha sheria au maamuzi kisha yakasababisha vifo vya wananchi, Je mikono yao haijaloa damu?

Dhahiri itakuwa imeloa damu, na kwa taarifa tu ni kwamba kuna sheria na maamuzi mengi yamefanyika hapa nchini na kusababisha vifo kwa wananchi wasio na hatia, hebu tuangalie kwa uchache tu sheria zinazowalinda wawekezaji wa madini. Wananchi wa maeneo yanakochimbwa madini hayo wameathirika na uchafuzi wa mazingira kutokana na wawekezaji hao. Lakini serikali imekaa kimya, huku wananchi wakiendelea kupoteza maisha. Katika kutibu malaria kuna dawa nyingi tu zimeidhinishwa na serikali kuwa ndizo zinazostahili kutumiwa katika kutibu malaria na zimesababisha vifo vya watu chungu mzima lakini hakuna anayejali.

Kuna utitiri wa madawa feki kuanzia madawa ya hospitalini na vipodozi ambapo watu wengi wameathirika na kupoteza maisha lakini hatuoni Juhudi zozote kutoka kwenye serikali yetu kudhibiti hali hiyo, je mikono ya viongozi hao ambao tumewapa dhamana ya kutulinda haijalowa damu? Vipi kuhusu kauli zetu tu? Kuna ukweli kwamba kuna watu wengi wamepoteza maisha kutokana na kauli. Kama hujui nitakukumbusha kiduchu, somo likolee! Unaweza kukuta mtu anaweza kumwambia mwenzie kuwa ameathirika na virusi vya ukimwi aidha kutokana na kudhoofika au kuugua mara kwa mara, na hiyo ikasababisha mtu huyo kujitoa roho.

Je mikono ya yule mtoa kauli haijaloa damu? Vipi kuhusu wale wanaowanyayasa wenzao kutokana na madaraka au nafasi walizonazo hadi kusababisha wenzao kujitoa roho. Mikono yao haijaloa damu? Kuna watu wamefuatilia haki zao katika vyombo vya kutoa haki, au kufuatilia mafao yao mpaka wakakata tamaa na kufa kwa sononi au kujitoa roho kutokana na kutitindikiwa na mawazo. Je mikono ya wahusika haijaloa damu? Kwa kifupi kama ukichunguza utagundua kuwa kuna watu wengi mikono yao imeloa damu, sio kwa kuua Paka tu, bali kwa kutoa roho za wanaadamu wenzao kwa aidha makusudi au bahati mbaya na hivyo mikono yao kuloa damu. Tunahitaji kubadilika na kutenda wema, na sio kwa wenzetu tu, bali hata kwa wanyama, kwani nao ni viumbe na wanaostahili kuishi. Je bado unakanusha kuwa hujamwaga damu?
 
Back
Top Bottom