Mzimu wa Ballali’ waitesa Ikulu

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
‘Mzimu wa Ballali’ waitesa Ikulu

na Tamali Vullu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

MZIMU wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Daudi Ballali, bado unaisumbua Ofisi ya Rais (Ikulu), ambayo imetoa kauli nyingine mpya kuhusiana na gavana huyo.

Hali hiyo ilibainika jana baada ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, kueleza kuwa wakati gavana huyo anaugua alifanyiwa upasuaji mara mbili, jambo ambalo halijapata kuelezwa na kiongozi yeyote wa serikali.

Rweyemamu, aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, alisema gavana huyo alifanyiwa upasuaji mkubwa mwaka 2002 nchini Afrika Kusini na upasuaji mwingine mdogo alifanyiwa mwaka 2007.

Mkurugenzi hiyo alisema baada ya hapo, Ballali alikuwa akipatiwa matibabu Boston, nchini Marekani.

“Ballali alifanyiwa upasuaji mkubwa mwaka 2002 Afrika Kusini na mwaka jana alifanyiwa ‘minor operation’ (upasuaji mdogo), halafu akawa anaendelea na matibabu Boston (Marekani),” alisema Rweyemamu alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na mwandishi mmoja wa habari.

Alisema suala la kifo cha Ballali limefanywa kisiasa na kukuzwa na vyombo vya habari, na akawasihi Watanzania kuiacha familia yake kuomboleza msiba huo.

Aidha, mkurugenzi huyo alisema serikali haijafanya siri suala la gavana huyo na kueleza kuwa Agosti mwaka jana aliposafiri kwenda nchini Marekani kwa matibabu ilitangaza, alipovuliwa ugavana ikatangazwa na hata alipofariki dunia serikali ilitoa taarifa.

“Vyombo vya habari vinavuka mipaka. Dhamana yenu ni kubwa… jadilini vitu vya msingi kama kupanda kwa bei ya mafuta na chakula,” alisema Rweyemamu ambaye wakati akiwa Mhariri Mtendaji katika magazeti ya Habari Corporation, alikuwa mstari wa mbele kuandika habari mbalimbali kuhusu viongozi serikalini.

Alisema kutokana na msiba huo kwa hapa nchini, serikali iligharamia chakula, ubani, viti, vinywaji na mahema na kuongeza kuwa kuhusu mzazi wa Ballali kupewa ulinzi mkali nyumbani kwake, alisema hafahamu ulinzi huo amepewa na nani.

Alisema anachofahamu ni kwamba katika nyumba hiyo iliyopo Boko, uliwekwa ulinzi wakati wananchi walipovamia.

Jana, gazeti hili liliripoti kuhusu kuzuiwa kwa watu wasio na kibali kuingia katika nyumba hiyo ya Ballali ambayo sasa anaishi mama yake mzazi mwenye umri wa miaka 94.

Ballali alifariki dunia Mei 16 mwaka huu, Washington nchini Marekani na si Boston kama inavyoelezwa na serikali kila mara na akazikwa huko huko Ijumaa iliyopita katika makaburi ya Wakatoliki ya Gate of Heaven, Silver Spring.

Ballali amekuwa akiripotiwa kuugua muda mrefu, lakini muda wote serikali haikuwahi kutoa taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya kiafya ya gavana huyo wa zamani wa BoT hadi baada ya kufariki dunia.

Hata alipofariki, serikali haikuwahi kutangaza kifo chake kwa muda wa siku nne na ikalazimika kufanya hivyo baada ya Tanzania Daima kutoa taarifa hizo.

Habari za kifo hicho cha Ballali, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Jakaya Kikwete Januari 8 mwaka huu, zimekuja siku chache baada ya serikali kupitia Ofisi ya Rais Ikulu, kutangaza kwamba ilikuwa haimtafuti gavana huyo wa zamani wa BoT na wala haifahamu alipo kwa wakati huo.
 
Back
Top Bottom