Mwl. Philipo Mulugo yatima aliyeukwaa uwaziri;Wazazi wake walifariki kwa kuliwa na mamba

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Mwl. Philipo Mulugo yatima aliyeukwaa uwaziri

lC.gif
Machi 16, 2011
rC.jpg

bul2.gif
Malezi ya kiroho siri ya mafanikio

bul2.gif
Wazazi wake walifariki kwa kuliwa na mamba


bul2.gif
Ajisomesha kwa kuvua samaki

UTEUZI wa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Philipo Mulogo, uliwashangaza wengi, hiyo ikitokana na ukweli kwamba hakuwa anafahamika, hakuwa miongoni mwa wanasiasa wenye majina pengine kutokana na kutokana na hulka yake ya kutojikweza. Wiki hii Raia Mwema ilifanya mahojiano maalumu na mwanasiasa huyo mwandishi wetu FELIX MWAKYEMBE anatuletea yaliyojitokeza katika makala haya.
UNAPOKUTANAYE kwa mara ya kwanza unashawishika kuamini kuwa ni kasisi, hiyo ni kutokana na jinsi anavyosalimia, anavyozungumza, anavyotembea na anavyoonekana kwa ujumla.
Hata hivyo, kwa taaluma yeye ni mwalimu, japokuwa wengi inawachukua muda mrefu kidogo kuamini hivyo, lakini huo ndio ukweli wenyewe kuhusu Naibu Waziri Philipo Mulugo aliyezaliwa miaka 39 iliyopita katika Kijiji cha Udinde, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.
Baadhi wamekuwa wakihoji, ametokea wapi, kutokana na ukweli kwamba yeye si jina kubwa wala maarufu, pengine hiyo yaweza kuchangiwa zaidi na hulka yake ya unyenyekevu na kutopenda kujikweza. Na kutokana na hulka yake hiyo yamezungunzwa mengi na wale wenye kuamini wanamfahamu sana lakini wakiwa na lengo la kumchafua.
Mathalani akijibu swali kuhusu uteuzi wake kuwa Naibu Waziri, Mulugo anasema: “Kwanza sikuwahi kuwaza kuwa waziri. Sikutegemea kutokana na historia yangu. Mimi ni masikini. Sikuwa mwanasiasa mwenye jina. Sikuwa nafahamika. ”
Anaongeza: “Kisha nilipata taarifa ya uteuzi nikiwa maeneo ya Ilula mkoani Iringa nikielekea jimboni kwangu kuwashukuru wananchi baada ya kutoka kuapishwa Dodoma. Nilipigiwa simu na kijana mmoja pale Mbeya, anaitwa Gunza Mwasote, yupo TEKU. Akaniambia nimeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri. Kwa kweli Mungu anatenda maajabu.”
Tangu alipoonyesha nia ya kuingia kwenye siasa za ushindani, yamesemwa mengi na wale wenye kudhani wana haki ya kuongoza kuliko wengine, wenye matamanio ya kupata wao na si wengine. Lakini wakati wote wamejikuta wakiadhirika mbele ya jamii kutokana na kuthibitika kwa nia zao mbaya.
Pengine ni vema kufahamu kwanza mtiririko wa baadhi ya matukio katika historia ya mwanasiasa huyu ambaye wengi hawakumfahamu hadi hivi karibuni pale Rais Kikwete alipomuibua na kumteua kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Maisha ya utoto ya Waziri Mulugo ni ya machungu. Ni kijana anayetoka kwenye familia ya uvuvi na kilimo, jamii ambayo inathamini zaidi uvuvi kuliko elimu. Lakini zaidi ya hilo, anatoka katika Wilaya ya Chunya ambayo upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile shule na maji ni shida.
Mazingira aliyokulia, watoto walilazimika kutembea zaidi ya kilometa nane kufika shuleni na kina mama walitembea zaidi ya kilometa tatu kufuata maji.
Anayazungumziaje maisha yake ya utoto?
“Natoka katika familia ya wavuvi na wakulima. Tunatoka kando kando ya Ziwa Rukwa kwa hiyo hizo ndiyo shughuli kuu za kiuchumi. Kuanzia mwaka 1980 nilijihusisha zaidi na uvuvi katika Ziwa Rukwa. Ni kama kilometa mbili hivi kutoka kijijini kwetu pale Udinde, kitongoji cha Rukwa. Sasa kitongoji hicho ni kijiji kamili. Nimevua samaki hadi nikiwa kidato cha sita. Samaki ndio walionisomesha.”
Anaongeza: “Shule kule nyumbani ilikuwa si lazima sana. Awali shule ilikuwa kijiji cha Kapalala, ipo kilometa zaidi ya nane kutoka kijijini kwetu, Udinde. Lakini mwaka 1983 sisi tulikuwa wanafunzi wa kwanza katika shule ya kitongojini kwetu pale Rukwa, ilifunguliwa na Mwalimu Kipata.
“Umbali ulisababisha watoto wengi kutokwenda shule. Badala yake walikwenda kuvua samaki. Ni watoto wachache sana waliovumilia kusoma. Mimi kilichonivutia ni baada ya baba yangu kuhamia Mlowo kwenye Chuo cha Ukatekista. Pale niliona watoto wakienda shule. Nikavutiwa, tuliporudi kijijini nikawa na hamu ya kuanza shule.”
Milango katika maisha ya Mulugo ilianza kujifungua mara baada ya kuhitimu sekondari, kidato cha sita, ambapo kutokana na hali ya kiuchumi ya familia yake, alilazimika kuanza kazi badala ya kuendelea na masomo ya juu. Alianza kufundisha katika Shule ya Sekondari Southern Highlands iliyopo eneo la Block T jijini Mbeya mwaka 2002.
Mwaka huo huo wa 2002 aliteuliwa kuwa Kaimu Mkuu wa Shule na kuanzia mwaka 2005 akawa ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa shule hiyo, ikiwa na maana ya mmiliki. Hii ni baada ya kukabidhiwa na wamiliki wake wa awali.
Nyota ya Mulugo iliendelea kung’ara na mwaka 2010 alijitosa kuwania ubunge Jimbo la Songwe lililopo katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya na kufanikiwa kuibuka mshindi kwenye kura za maoni kabla ya kupita bila kupingwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, na mwezi mmoja baadaye akateuliwa kuwa Naibu Waziri.
Ni mtiririko huu wa matukio yake kuanzia kuanza kazi ya ualimu hadi uwaziri, unaowafanya baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa mkoani Mbeya wayaone mafanikio ya kijana wao huyo kuwa yenye baraka za Mungu zaidi ya nguvu ya mwanadamu katika kutafuta madaraka na utukufu.
Wanaomfahamu wanaamini kuwa Mungu ameamua kujidhihirisha kwake baada ya kupitia matatizo mazito angali na umri mdogo, na miongoni mwa matukio yatakayodumu katika kumbukumbu zake milele ni lile la wazazi wake wote wawili kufariki kwa aina moja ya kifo: kuliwa na mamba.
“Wazazi wangu wote wawili walifariki kwa kuliwa na mamba. Mama alifariki mwaka 1991 nikiwa kidato cha pili. Alikuwa anakwenda kuchota maji mtoni akakamatwa na mamba. Ilikuwa ni kama kilometa nne hivi kufuata maji mtoni. Baba yeye alifariki mwaka 2006 nikiwa Mkurugenzi Southern Highlands. Naye alikamatwa na mamba ziwani wakati akifua nguo,” anasimulia Waziri Mulugo.
Pamoja na matukio hayo, Mulugo amekulia katika mazingira ya dini, na katika mahojiano anabainisha kwamba mazingira yalimshawishi atamani maisha ya utawa, alitamani sana kuwa padre.
“Nimekulia katika mazingira ya dini. Baba alikuwa katekista, yamenifundisha kuwa mtiifu, kuishi kwa kufuata ratiba, inaanzia asubuhi kwa kwenda kusali. Nimeishi na watawa. Nimekulia kwenye kwaya. Nimejifunza vitu vingi, nikatamani maisha ya upadre,” kisha anaelezea sababu zilizomfanya asitimize ndoto yake hiyo ya upadre:
“Nilitamani kuwa padre lakini baada ya mama yangu kufariki na ambaye alikuwa na msukumo mkubwa wa ajenda hiyo nikaamua kuwa mwalimu na hatimaye siasa kwani kazi ya ualimu ni kufundisha na kazi ya upadre ni kufundisha pia.
“Uongozi wa siasa na uongozi wa dini naona vyote vinashabihiana kimalengo, hasa katika kuleta amani, utulivu, uwajibikaji, upendo, kujikosoa, malengo na kufanya kazi kwa bidii pia kupiga vita uvivu, ujambazi, uwongo, udhalimu, nk. Dini na siasa vinaungana katika kuzalisha viongozi wacha Mungu, waadilifu na wenye moyo wa kutenda na wanyenyekevu.”
Maisha yake ya utoto yana msukumo gani katika maisha yake ya sasa, hususani baada ya kufanikiwa kimaisha?
“Ninaamini maisha yangu ya utoto ndiyo yenye kunisukuma kufanya maamuzi yangu mengi kuhusu ndugu zangu kule nyumbani, hasa hasa yatima. Labda kwa sababu na mimi mwenyewe ni yatima, ninaamini wengi wamenisaidia katika maisha yangu hadi kufika hapa nilipo.”
Miongoni mwa matukio yanayoakisi historia ya Waziri huyo ni hatua yake ya kusomesha watoto. Anasomesha watoto yatima 516 kutoka Jimbo lake la Songwe katika shule mbalimbali za sekondari za kata wilayani Chunya.
Mpango wake huo wa kusomesha watoto yatima na wenye kutoka kwenye familia masikini jimboni humo aliuanza tangu akiwa Shule ya Sekondari Southern Highlands ya jijini Mbeya.
“Nikiwa Southern Highlands nilikuwa nikisomesha vijana kutoka nyumbani na hivi sasa baadhi wako vyuo vikuu. Nilianzisha kituo katika Shule ya Sekondari Mkwajuni kwa ajili ya vijana waliokosa kwenda sekondari. Vijana wote wanaofaulu kwenda sekondari katika Vijiji vya Udinde, Rukwa, Kapalala, Iboma, Kininga, Ngwala, Gua, Songwe na Manda, nawalipia ada hadi wanapomaliza kidato cha nne,” anasema Waziri Mulugo.
Pamoja na kusaidia wanafunzi hao walioko sekondari, Mulugo hajawasahau wenzake, aliosoma na kuvua nao samaki. Hawa aliwashauri kwanza kuunda kikundi chao kisha akawapatia nyavu 100 za kuvulia.
Changamoto za wizara na Watanzania watarajie nini kutoka kwa Waziri?
“Nipo kumsaidia Waziri mwenye dhamana. Napangiwa kazi na Waziri, Dk. Shukuru Kawambwa. Nina imani tutafanya kazi nzuri pamoja. Naelewa wananchi wanatarajia mengi kutoka kwetu, kama unavyofahamu elimu ni eneo nyeti.
“ Tulipoingia tu tulikutana na changamoto ya migomo vyuo vikuu, inayosababishwa na mfumo mzima wa utoaji mikopo kwa wanafunzi. Hilo sasa Rais ameunda tume tayari, linashughulikiwa. Ipo changamoto ya matokeo mabaya ya kidato cha nne, yamelishitua Taifa, yanasababisha elimu yetu ionekane yenye matatizo.
“Kuna kazi ya kuboresha elimu ya sekondari nchini, miundombinu ya shule, walimu na vifaa. Kuna changamoto ya madai ya watumishi wa wizara wakiwemo walimu, yale ya kuanzia mwaka 2008 kurudi nyuma. Tunayashughulikia pale wizarani na tunaelekea kuyamaliza. Lakini yale ya kuanzia 2009 kuja mbele madai yako TAMISEMI.
“ Katika madai ya watumishi hapa kuna mkanganyiko. Wengi hawaelewi, kwa hiyo wizara itaanza kutumia vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi waelewe kazi zinazofanywa na wizara, na vile vile tunayo changamoto ya wanafunzi kukwepa masomo ya sayansi, hii si nzuri kwa ustawi wa Taifa, tutafika wakati tutalazimika kuajiri wataalamu toka nje.
Vituo vya kujiendeleza
Waziri Mulugo ana mtazamo tofauti kuhusu vituo vya kujiendeleza nchini: “Kuna vituo hivi vya QT. Watu wanasoma miaka miwili kuhitimu kidato cha nne. Hii si sawa.
“Mfumo wa elimu unamhitaji mtu kusoma miaka mine. Lakini huyu aliyeshindwa darasa la saba anasoma miaka miwili, tena hayuko kwenye mfumo rasmi, na anafanya mtihani wa kidato cha nne, yule aliyefaulu anasoma miaka mine. Hii inabidi kuangaliwa upya, au aliyefeli kidato cha nne anaenda kwenye hizo centre kuandaliwa afanye kidato cha tano na sita kwa mwaka mmoja badala ya miaka miwili, si sawa kabisa.”
Msingi wa hoja ya Waziri Mulugo ni ukweli kwamba awali vituo hivi vilianzishwa kwa lengo la kuwaendeleza walimu wa daraja la IIIC wafikie kiwango cha kidato cha nne na kuendelea. Hawa tayari walikuwa na miaka mitatu ya vyuoni hivyo kuwa na maandalizi ya sekondari tofauti na hawa wanaojiunga sasa ambao hawana mafunzo yoyote zaidi ya elimu yao yamsingi tena wengi wakiwa wamemaliza muda mrefu au waliofeli kidato cha nne.
Mulugo katoka wapi?
Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi ya Rukwa wilayani Chunya na kuhitimu mwaka 1989 na kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mbeya alikohitimu mwaka 1993. Mwaka 1994 alijiunga kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea ambako alihitimu kidato cha sita mwaka 1996.
Mwaka 2002 alianza kufundisha Shule ya Sekondari Southern Highlands ya Mbeya na mwaka huo huo akajiunga na Chuo Kikuu Huria kwa shahada ya ualimu na uchumi aliyohitimu mwaka 2008.
Historia yake inamuonyesha kuwa kijana mwenye kipaji cha uongozi kwani akiwa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mbeya alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti UVCCM pamoja na kuwa Kaka Mkuu shuleni hapo.
Katika kipindi chake chote cha miaka sita ya sekondari alikuwa Mwenyekti wa Jumuiya ya Vijana wanafunzi wa Kanisa Katoliki (TYCS), Jimbo la Mbeya na Jimbo la Songea pale alipojiunga na kidato cha tano Shule ya Wavulana ya Sekondari Songea ambako pia alichaguliwa kuwa Makamu Rais wa Shule hiyo.
Miongoni mwa nafasi anazozishikilia ndani ya CCM ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Chunya, Mjumbe Mkutano Mkuu Taifa Wazazi, Katibu wa Uchumi, Elimu, Malezi na Mazingira Wazazi Chunya, Mjumbe Kamati ya Maadili ya Viongozi wa CCM Wilaya ya Chunya na Meneja Timu ya soka Wilaya ya Chunya.
Mwaka 2005 alikusudia kuingia kwenye kinyang’anyiro kuwania jimbo hilo lakini akachelea na ndipo mwaka jana alipoingia ambapo alipata ushindi mkubwa kuanzia kura za maoni ndani ya CCM zilizokuwa na wagombea sita na yeye kuzoa kura zaidi ya 6,900 huku akifuatiwa na Mbunge wa kwanza wa Jimbo hilo la Songwe, Paul Ntwina aliyeambulia kura 1,060. Alipita bila kupingwa katika Uchaguzi Mkuu.
Waziri Mulugo ni wa saba kuzaliwa katika familia ya watoto 12 ya mzee Augustino Mulugo na mama Christina Kadyango. Ameoa, ana mke na watoto.
hs3.gif
 
Back
Top Bottom