Shairi: Mwanakijiji Shambani Hanang Kunani Pale?

Companero

Platinum Member
Jul 12, 2008
5,604
1,704
Namshukuru sana Jalia,
Kurejea Darisalama;
Arusha mpaka Manyara,
Mtafiti sikukwama.

Nimejawa na bashasha,
Mrejesho kuutuma;
Wanazuoni wa Taifa,
Usikilizeni umma.

Ardhi yao Wadatoga,
Iligeuzwa chauma;
Nafko lo ikajitwalia,
Ngano kuilima.

Barbaig do akacharuka,
Kortini akasimama;
Dola ikajitetea kijanja,
Sheria ikazifuma.

Ikaleta Operesheni Sogeza,
Wananchi kuwasukuma;
Vijijini wakaswekwa kisasa,
Wakache kuhamahama.

Ujima uendeshwao kiusasa,
Kikaazimia chama;
Utumike kujenga Tanzania ,
Maendeleo kupima.

Mwalimu akauita Ujamaa,
Tukaukubali pima;
Ukahubiriwa kwa harara,
Tukatazamia mema.

Tukalima kwa ushirika,
Pato kulichuma;
Ranchini tukafuga pia,
Kujipatia nyama.

Hatamu chama kikashika,
Utawala ukauma;
Nacho kikaihodhi Katiba;
Watu kuwazima.

Wafugaji wao wakaswagwa,
Kama wanyama;
Mpaka leo wanatangatanga,
Kutafuta neema.

Uchumi nao ukayumbayumba,
Shilingi ikazama;
Wakalisaliti Azimio Zanzibara,
Likapata kiyama.

Hatimaye Nafko ikafilisiwa,
Ikaupoteza uzima;
Wafugaji ardhiyo wakaililia,
Msafara wakatuma.

Kwao Wakuu wakafikia,
Risala wakaisoma;
Wakasihi ardhi kupewa,
Iwahifadhi daima.

Baadhi yao mashamba,
Wakuu wakasema;
Tutawapa enyi wazawa;
Mgawane mazima.

Ila mengine watayawekeza,
Hao wachuma;
Bila ajizi yakabinafsishwa,
Tena himahima.

Wakayanadi pia matirekta,
Navyo vyuma;
Hata maji wakayabinafsisha,
Nao wakachuma.

Wawekezaji yote hawajaweza,
Mashamba kuyalima;
Heri Nafko walivyoyakwatua,
Wanateta wakulima.

Tambua we mwanasiasa,
Unaleta zahama;
Kama kanzu kuichuuza,
Rasilimali mama.

Warudishieni rasilimali wana,
Nao ndama;
Wananchi tuweze kujifugia,
Na kulima.

Chanzo: UDADISI: The Act of Rethinking
 
Back
Top Bottom