Mwalimu wetu Makini

Ndahani

Platinum Member
Jun 3, 2008
18,119
9,049
Mtu kwao anatunzwa, hata kama hana dini,
Mtu kwao anatunzwa,ili apate thamani,
Mtu kwao anatunzwa, mfanowe halingani,
Nyerere kweli mwalimu, kwa mengi alotufunza

Uongozi msimamo, bila kutaka makuu,
Uongozi ni masomo, uwezo uwe wa juu,,
Uongozi mitizamo, yenye tija na nafuu,
Nyerere kweli mwalimu, kwa mengi alotufunza

Tanzania uliyounda,haikujari ni nani,
Wote uliwapenda, kama watoto nyumbani,
Sheria hukuzipinda, ili tukujue nani,
Nyerere kweli mwalimu, kwa mengi alotufunza

Nchi ulivyoipenda, tena na kuithamini,
Nchi yako ukalinda, kwa akili na makini,
Pamoja na kukuwinda, ila ulijiamini,
Nyerere kweli mwalimu, kwa mengi alotufunza

Leo tunakukumbuka, kama shujaa makini
Toka umetuondoka, mambo hayawezekani,
Kama ungeliamka, usingeweza amini,
Nyerere kweli mwalimu, kwa mengi alotufunza

Leo tumekusaliti, kama hatuwa wako,
Toka upate mauti, ni kama haukuwako,
Tumeuza hata miti, ya pale shambani kwako,
Nyerere kweli mwalimu, kwa mengi alotufunza

Ulale pema peponi, mwalimu shujaa wetu,
Tuliopo humu ndani, twakumbuka enzi zetu,
Ujamaa vijijini, kauli na mbiu yetu,
Nyerere kweli mwalimu, kwa mengi alotufunza

“We must never cease from exploring. At the end of all exploring, will be to arrive at where we began and know the place for the first time” …
 
Aksante sana Ndahani.Kumbuka tu kuweka kwenye vitendo hayo aliyoyaamini!
 
Back
Top Bottom