Mwalimu aliyefariki aendelea `kula` mshahara, apanda cheo

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Halmashauri ya wilaya ya Bunda, imeingia kwenye kashfa kubwa baada ya kubainika kumlipa mshahara mwalimu aliyekufa mwaka 2007.
Aidha, mwalimu huyo pia alipandishwa daraja mwaka 2009 na mshahara wake haijulikani unachukuliwa na nani .
Kashfa hiyo iliyoibuliwa juzi kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani na kuwaacha wajumbe wakiwa wameduwaa, inazidi kuonyesha wazi kuwa tume iliyopita kuhakiki watumishi hewa haikufanya kazi kama ilivyotarajiwa.
Akizungumza katika kikao hicho, diwani wa Kata ya Kibara, Venance Kamonyore, alisema anashangazwa na kitendo cha ofisi ya
Mkurugenzi kuendelea kupokea mshahara wa marehemu mwalimu Charles Mwijarubi aliyekuwa akifundisha katika Shule ya Msingi Namibu, Kata ya Kibara ambaye alikufa mwaka 2007.
“Niliwahi kumuuliza Mkurugenzi inakuwaje mtu amekufa mwaka 2007 mshahara wake unaendelea kuja mpaka sasa, la kushangaza mwaka 2009, alipandishwa daraja na mshahara kuongezeka...ndugu zake wanataka kujua nani anachukua fedha zao,” alihoji diwani.
Alisema ndugu zake walikuwa tayari kwenda wizarani kudai fedha hizo na ufisadi wa kutumia jina la marehemu kujipatia fedha ambazo familia yake hazijazipata.
“Toka nimeongea na Ded, sijapata majibu. Hivi kweli fedha hizo zinarudishwa Hazina na kwa nini jina hilo liendelee kuonekana kama yuko kazini wakati alishafariki dunia sasa ni mwaka wa nne,” alizidi kuhoji.
Hoja hiyo iliyosisimua baraza ilimfanya Mkurugenzi Mtendaji, Cyprian Oyier, kujitutumua kuijibu, akikiri kuwa aliambiwa na diwani na kufuatilia ili jina hilo liondolewe na mshahara usije.
“Nilimweleza ahakikishe wanawaandikia Hazina jina hilo liondolewe, yuko hapa atajibu kama mshahara huo unakwenda wapi, maana kama jina halijaondolewa utaendelea kuja,”alisema Mkurugenzi.
Hata hivyo Kaimu Mweka Hazina, Stella Msangya, hakuweza kujibu tuhuma hiyo mpaka mwisho wa kikao hali ambayo inazidisha mashaka juu ya tuhuma hiyo iliyoibuliwa ghafla.
Kaka wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la mwalimu mstaafu Wijarubi, akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema wao wanafuatilia kuona ufisadi huo wa kutumia majina ya marehemu kupata fedha.
Alidai kuwa mpaka risti za mishahara ya Januari, mwaka huu ipo na wanayo na kuwa mrithi wa mali za marehemu ambaye ni kijana wake, James Mwijarubi, alimfikia diwani Februari, mwaka huu baada ya kupata taarifa na katika ufuatiliaji walibaini ukweli wa mambo.
Baadhi ya madiwani walisikitishwa na mchezo huo ambao walidai ni kashfa kubwa kwa halmashauri huku wakidai kuwa tume zinazoundwa kuchunguza watumishi hewa hazijazaa matunda kwa kuwa majina hewa bado yapo sekta za elimu na afya.
 
Back
Top Bottom