Mwakalebela aigaragaza Takukuru mahakamani

Manyanza

JF-Expert Member
Nov 4, 2010
8,861
12,496
Friday, 25 February 2011 21:22
Tumaini Msowoya, Iringa
KESI ya pili ya kupokea rushwa kwenye mchakato wa kura ya maoni ndani ya CCM iliyokuwa ikimkabili Frederick Mwakalebela (41), imeondolewa mahakamani na mshtakiwa kuachiwa huru.

Kuondolewa kwa kesi hiyo kunafuatia pingamizi la awali lililowekwa na wakili wa Mwakalebela, Basil Mkwata.

Mwakalebela alikuwa mshindi wa kwanza kura za maoni za CCM nafasi ya ubunge wa Iringa Mjini mwaka jana, lakini jina lake liliondolewa na nafasi yake kupewa Monica Mbega, ambaye alishindwa na mpinzani wake, Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Mkwata, uliwasilisha pingimizi la awali la kisheria ukiomba kesi hiyo iondolewe mahakamani kutokana na upungufu wa kisheria uliofanywa na upande wa mashtaka, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (Takukuru).

Upungufu huo ni mtuhumiwa kushtakiwa kwa kutumia sheria mbili tofauti kwenye hati moja ya mashtaka, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Akiondoa shauri hilo mahakamani, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Festo Lwila, aliyekuwa anasikiliza shauri hilo alisema mahakama imeridhia pingamizi hilo.

Hakimu Lwila alisema mshtakiwa alishtakiwa kwa kutumia sheria mbili tofauti kwenye hati moja ya mashtaka, suala ambalo ni kinyume cha sheria na kinaweza kumsababisha ashindwe kuandaa utetezi wake ipasavyo.

Pia, Lwila alisema hapakuwa na sababu ya kuweka sheria mbili tofauti kwenye hati moja na kwamba, usahihi wa hati ya mashtaka unapaswa kuwa makini tangu awali inapoandaliwa, tofauti na hivyo ndio umemfanya Mwakalebela kuwa huru.

“Kutokana na sababu hii, mshtakiwa anakuwa huru na upande wa mashtaka mna hiari ya kuleta tena kesi hii ikiwa haina 'duplicate',” alisema.

Katika pingamizi hilo, Mkwata alisema tayari mshtakiwa ameshaadhibiwa baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kumwengua kwenye uchaguzi, hivyo kuomba shtaka hilo liondolewe mahakamani.

Awali, akisoma shtaka hilo Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Imani Mizizi, alidai kuwa Juni 20, mwaka jana, Mwakalebela alidaiwa kutoa hongo ya Sh100,000 kwa Hamis Luhanga ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoga, ili awagawie wajumbe 30 wa CCM walioitwa kwenye kikao.

Mizizi alidai kuwa, Mwakalebela anadaiwa kutoa rushwa kinyume cha sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15(1)(b) kinachokwenda sambamba na sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010, kifungu cha 21 (1) (a) na kifungu cha 24(8).

Pia, Mahakama ya Mkoa wa Iringa Jumatatu ijayo inatarajia kutoa uamuzi iwapo kesi ya kwanza inayomkabili Mwakalebela (41) na mkewe Selina, iendelee kusikilizwa au iondolewe.

Source:Mwananchi
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom