Muuza jeneza

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,282
1472582184092.jpg


Kuna jambo latatiza, leo nikupe maana,
Wahenga walitujuza, kuwa kufa kufaana,
Biashara ya jeneza, jua haina laana.
Hutuombea shufaa, mtengeneza jeneza.

Kabla kifo kutokeza, kulianza kuzaana,
Dunia wakaijaza, wawili walo twaana,
Haiwi tusi kuuza, kulete kukataana,
Hutuombea shufaa, mtengeneza jeneza.

Pia auzaye sanda, hutuombea shufaa,
Tupate pona madonda, yatuepuke mabaa,
Ile safari tukenda, pesa hatazikataa,
Hutuombea shufaa, kila auzaye sanda.

Imetoka kwa kiwanda, kuwa bure tashangaa
Kila siku tunaranda, sanda hatuja andaa,
Mwenda zake akienda, akili zinatupaa,
Hutuombea shufaa, kila auzaye sanda.

Mwisho si kwa muhimu, yupo mchimba kaburi,
Hapendi umaamumu, hutuombea Qahari,
Ukweli yatulazimu, maiti kuzisitiri,
Hutuombea shufaa, kila mchimba kaburi.

Dua zake kwa Rahimu, zituepuke shari,
Hatogusa tarasimu, kutufanyia sihiri,
Sababu anafahamu, mauti yana kadari,
Hutuombea shufaa, kila mchimba kaburi.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/Whatspp 0622845394 Morogoro.
 
Back
Top Bottom