Mume, mke na watoto wawili wafa moto chumbani

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
moto%282%29.jpg

Baadhi ya ndugu, wakiangalia mabaki ya vitu mbalimbali katika ajali ya watu watano wa familia moja kuteketea kwa moto ndani ya nyumba yao eneo la Kisiwani Mkwajuni, Kata ya Vijibweni, Wilaya Temeke mkoani Dar es Salaam juzi usiku.



Mume, mke, watoto wao wawili pamoja na shemeji yao, wamekufa baada ya moto kuteketeza chumba walichokuwa wakiishi katika mtaa wa Kisiwani-Mkwajuni uliopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Waliokufa katika tukio hilo ni baba wa familia, John Onesmo (32), mke wake, Catherine John (25), watoto wao, Joyce John (5) na Oliver John (2).
Mwingine aliyekufa katika tukio hilo ni mdogo wa Catherine aliyetajwa kwa jina la Ester Amosi (20), aliyefika kwenye nyumba hiyo siku chache akitokea kwa mume wake. Inadaiwa Ester alikuwa mjamzito.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kamishna wa Polisi, David Msime, alithibitisha kutokea kwa janga hilo na kwamba uchunguzi unaendelea. Pia alisema polisi inamfuatilia mtuhumiwa mmoja, anayedaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo.
Baba wa familia, Onesmo alikuwa mfanyabiashara wa samaki katika soko la Feri wakati mke wake, Catherine, alikuwa mchuuzi wa mboga wakati Joyce alikuwa mwanafunzi wa shule ya Chekechea iliyopo Kigamboni.
Familia hiyo ambayo ilikuwa ikiishi kwenye chumba kimoja, imekutwa na maafa hayo usiku wa kuamkia jana, wakiwa wamelala.
Wakizungumza na gazeti hili majirani wa familia hiyo, walisema wakati wa tukio, walisikia sauti ya mwanamke akilia huku akiomba msaada.
Moshi Omar ambaye ndiye aliyemuuzia marehemu John eneo alipojenga nyumba yenye chumba kimoja, alisikia sauti ya mwanamke ikiomba msaada.
"Nilitoka nje na kukuta nyumba ya John ikiteketea na moto, nilishtuka sana, nilipiga kelele na majirani wengine walifika, tulijaribu kubomoa mlango ili kuwaokoa, lakini hatukufanikiwa, moto ulizidi na moshi mzito mweusi ulitanda," alisema huku akiwa ameshika tama.
Omar alisema jitihada za kuiokoa familia hiyo hazikuzaa matunda kwa sababu moshi ulikuwa mzito.
Alisema moto huo ulidumu kwa takriban saa tatu, ndipo polisi walipofika katika eneo hilo.
"Wakati tukio likitokea chanzo hatukukijua, lakini asubuhi baadhi ya wapita njia walikuta chupa ya maji ya uhai ya lita tano, ikiwa inanukia mafuta ya petroli,”
“Chupa hii ilikuwa imetupwa mita chache kutoka kwenye eneo la tukio, tuliwataarifu polisi na walifika mara moja kuichukua kama moja ya kielelezo," alisema.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana katika eneo la tukio, zilieleza kuwa huenda mmoja wa marehemu hao alikuwa amegombana na mtu mmoja ambaye hajatajwa.
Mmoja wa majirani wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazeti aliiambia Nipashe kuwa, siku chache kabla ya tukio hilo kutokea, alisimuliwa na mmoja wa marehemu juu ya ugomvi huo.
"Huyu … aliniambia kuwa … aligombana na ugomvi ulikuwa mkubwa ambao ulisababisha kupigwa," alisema jirani hiyo.
Aliendelea kueleza kuwa, baada ya tukio hilo, polisi walifika nyumbani kwa anayetuhumiwa lakini walikuta mlango wa nyumba yake ukiwa wazi na ndani hapakuwapo mtu yeyote.
Baada ya kumkosa, polisi wanadaiwa kwenda eneo analofanyia kazi ambapo pia walimkosa.
Mdogo wa marehemu John, Jesse Onesmo, alipata taarifa za msiba huo kutoka kwa baba yao mzazi.
"Kwa kweli sikuamini, baba alimtaja kaka peke yake, lakini baadaye nikagundua kumbe ni familia yake yote imeteketea, inauma, inaumiza, sijawahi kushuhudia tukio kama hili," alisema.
Naye, mfanyabiashara wa samaki soko la Feri, Hamisi Mazengo, alisema kuwa alipata taarifa za tukio hilo kutoka kwa mfanyabiashara mwenzao anayeishi jirani na eneo hilo.
Hata hivyo, Mazengo alisema mpaka sasa hajahafahamu sababu na chanzo cha moto huo.
Alisema kwa upande wa eneo lao la kazi marehemu John hakuwahi kugombana na mtu zaidi alichosikia mtaani ni kwamba chanzo kinasadikiwa kuwa ni ugomvi na mmoja wa marehemu. Hata hivyo, Msime alisema hadi kufikia jana jioni, hapakuwa na taarifa kuhusu kukamatwa kwa mtuhumiwa wa tukio hilo.
Alisema moto huo ulizimwa na wananchi wa eneo hilo na kwamba kikosi cha zima moto cha halmashauri ya jiji, kilichelewa kufika eneo hilo.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema kuwa miili ya marehemu hao ambayo imehifadhiwa hospitali ya Vijibweni, Kigamboni inatarajia kuzikwa leo saa 10:00 jioni maeneo ya Kigamboni.




CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom